PAPA FRANSISKO APONGEZWA POLAND
Bi Beata Maria Szydlo, Waziri mkuu wa Poland katika mahojiano maalum na Radio Vatican anapenda kumshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa uwepo na ushiriki wake wa dhati katika maadhimisho ya Siku ya XXXI ya Vijana Duniani sanjari na Jubilei ya Miaka 1050 ya Ukristo nchini Poland. Katika mazungumzo yake ya faragha na Baba Mtakatifu ameonesha kuguswa zaidi na maisha na utume wa familia; shida, fursa na changamoto zinazowakabili wananchi wa Poland, lakini pia amewashukuru waamini wa Poland kwa ushuhuda wa imani yao kwa Kristo, Kanisa na Ibada kwa Bikira Maria. Mwezi Agosti, ni kipindi cha hija kwa waamini wengi.
Waziri mkuu wa Poland anapenda kumshukuru Mungu kwa ujio na uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko uliomwezesha kuwafahamu kwa karibu zaidi wananchi wa Poland pamoja na kusijikia kuwa nyumbani nchini Poland. Kwa namna ya pekee, ameguswa na hotuba na mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu katika matukio mbali mbali. Ni kiongozi anayefahamu kutumia lugha ya nyepesi ili kufikisha ujumbe wake kwa walengwa.
Sala na ukimya ulioneshwa na Baba Mtakatifu kwenye kambi za mateso na kifo huko Auschwitz na Birkenau ni mambo yaliyoacha mwangwi mkubwa katika nyoyo na akili za watu kwani hapa ni mahali panapogusa utu na heshima ya binadamu. Huko ni mahali alipozaliwa Waziri mkuu wa Poland, kumbe historia ya maeneo haya anaifahamu na inamgusa kwa karibu sana. Alibahatika kutembelea kambi hizi wakati Mtakatifu Yohane Paulo II na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI na sasa Papa Francisko alipotembelea na kusali huko.
Mwaka huu, tukio hili limekuwa na uzito wa pekee kwani ni kumbu kumbu ya miaka 70 tangu alipouwawa kikatili Mtakatifu Marximilliano Maria Kolbe, aliyejisadaka kufa ili kuokoa maisha ya mfungwa mwenzake, ili aweze kuendelea kuwajibika kwa ajili ya kutunza familia yake. Baba Mtakatifu Francisko, mwanzoni kabisa mwa hija yake ya kitume nchini Poland amezungumzia kwa kina na mapana kuhusu changamoto ya wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi Barani Ulaya na umuhimu wa kuonesha mshikamano wa kimataifa; amekazia tunu msingi za maisha ya familia na umuhimu wa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha Injili ya uhai tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu.
Waziri mkuu wa Poland Beata Maria Szydlo anasema anapenda kuunga mkono juhudi za Baba Mtakatifu Francisko katika kutetea na kushuhudia tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, dhidi ya utamaduni wa kifo unaoendelea kusambaa sehemu mbali mbali za dunia. Raia wengi wa Poland bado wanathamini maisha ya ndoa na familia na kwamba, wanaendelea kusimama kidete kutetea tunu msingi za ndoa, familia na utu wema. Baba Mtakatifu ametoa changamoto kubwa kwa vijana wa kizazi kipya katika safari ya maisha yao ya ujana, kuwa na ujasiri wa kuamua kujenga na kudumisha familia.
Wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi ni changamoto kubwa na haina majibu ya mkato, bali inahitaji ushirikiano na mshikamano wa kimataifa ili kutoa huduma na hifadhi kwa wakimbizi na wahamiaji. Kuna haja ya kuonesha moyo wa upendo na mshikamano kwa maskini na wale wanaoteseka kutokana na vita, nyanyaso na dhuluma mbali mbali kadiri inavyowezekana, sanjari na kusimama kidete kulinda na kudumisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao dhidi ya vitendo vya kigaidi vinavyoweza kutekelezwa na watu wasiokuwa wema.
Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko imeacha changamoto nyingi ambazo zinapaswa kufanyiwa kazi pole pole kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu nchini Poland. Vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia wameacha historia, furaha, ari na mwamko wa imani, matumaini na mapendo. Waziri mkuu wa Poland anasema, vijana hawa wameonesha kwamba, wanayo ndoto kubwa ya maisha inayopaswa kutekelezwa kwa kujikita katika kanuni maadili na utu wema; maisha ya kiroho na kijamii.
Ni matumaini ya Serikali ya Poland kwamba, vijana wataufanyia kazi utajiri na urithi mkubwa walioupata wakati wa maadhimisho ya Siku ya XXXI ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016 nchini Poland. Vijana wamesali, wametafakari na kusherehekea zawadi ya maisha katika hali ya umoja, upendo na mshikamano. Serikali inawapongeza wananchi wa Poland kwa kuonesha upendo na ukarimu; vijana waliojitolea katika huduma mbali mbali kwa ajili ya wageni. Ni matumaini ya Serikali ya Poland kwamba, vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia wataweza kusimulia matendo makuu ya Mungu katika maisha yao kutoka nchini Poland.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Comments
Post a Comment