VIJANA WAACHA GUMZO POLAND
Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 30 Julai 2016 ameongoza Ibada ya Mkesha wa Sala kwa ajili ya kufunga maadhimisho ya Siku ya XXXI ya Vijana Duniani. Muda wa masaa matatu umekuwa ni kipindi cha kusherekea zawadi ya imani, kusali na kutafakari. Baba Mtakatifu akiwa ameandamana na baadhi ya vijana wawakilishi walipitia katika lango la huruma ya Mungu, wakasikiliza shuhuda, akatoa tafakari na hatimaye, akafunga mkesha kwa Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, chemchemi ya huruma ya Mungu.
Baba Mtakatifu katika tafakari yake amekazia umuhimu wa sala katika kuombea amani, upendo na mshikamano kati ya watu. Vijana waliokuwa wanahudhuria maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani ni watu wanaotoka katika maeneo salama na yenye amani, lakini wengi wao ni wale wanaotoka maeneo ya vita, kinzani na dhuluma, mambo ambayo kwa sasa yanatawala katika vyombo vya habari duniani. Lakini kwa vijana waliokuwa kwenye mkesha, Baba Mtakatifu anawaambia kwamba, mateso, mahangaiko si tena kipaumbele chao, bali wao wanataka kujenga historia ya umoja na udugu.
Baba Mtakatifu anasema, umefika wakati wa kusimama kidete kupinga vita kwa nguvu zote kwani inaendelea kusababisha umwagaji wa damu na madhara makubwa katika maisha na maendeleo ya watu! Hakuna sababu msingi inayoweza kuhalalisha vita kwani maisha ya kila mtu yana thamani kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anawashukuru vijana waliofanya mapambano ya maisha ya kiroho, hadi kuupata ushindi, kielelezo cha huruma ya Mungu inavyowagusa na kuwabadilisha watu katika maisha yao.
Baba Mtakatifu anasema, vijana wanataka kupinga vita, chuki na uhasama kati ya watu; kushinda vitendo vya kigaidi kwa kujikita katika utamaduni wa umoja na udugu; upendo na mshikamano, ili kujenga familia ya binadamu. Vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaadhimisha Sherehe ya imani, wanaungana kwa ajili ya sala ili kuwa kweli ni chachu ya mabadiliko katika maisha ya vijana wengi duniani. Hawa ni vijana wanaotambua na kuthamini tunu msingi za maisha ya kifamilia; Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo na kushikamana katika umoja, licha ya tofauti msingi zinazojitokeza kati ya vijana.
Baba Mtakatifu anawataka vijana kushinda woga na wasi wasi ili kuleta mabadiliko katika maisha, kama ilivyokuwa Siku ile ya Pentekoste, Roho Mtakatifu alipowashukia mitume, wakatoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia kwamba, Kristo Yesu, alikuwa amefufuka kwa wafu! Vijana wakithubutu, mabadiliko yanawezekana duniani! Woga na wasi wasi vinawafanya vijana wengi kujisikia kwamba, hawathaminiwi, hawapendwi na wala hawana fursa za maisha bora na matokeo yake ni vijana kujifungia katika upweke hasi, dalili za kukata tamaa na hatimaye, kutumbukia katika kifo! Lakini vijana watambue kwamba, mbele yao kuna fursa za kuweza kubadilika, kukua na kukomaa na hatimaye, kufurahia maisha ya ujana wao unaosimikwa katika urafiki, ndoto, upendo na mshikamano wa dhati.
Baba Mtakatifu anawaonya vijana kutopenda mno starehe na anasa katika maisha; kwa kupenda na kumiliki vitu kwa kudhani kwamba, haya ni mambo msingi yanayowakirimia furaha ya kweli katika maisha, lakini haya ni mambo hatari kabisa yanayobomoa furaha ya maisha ya ujana kwa kuwatumbukiza katika uzee hata kabla ya kuzeeka, kuanza kula pensheni hata kabla ya kuanza kazi. Baba Mtakatifu anawataka vijana kuchangamkia maisha na kamwe wasibweteke kwa kupenda raha na starehe za mkato.
Vijana waliohudhuria maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani huko Cracovia wanapaswa kuacha alama ya kudumu katika maisha yao, kwa kuwa wakweli, waaminifu na wachamungu. Vijana ambao wako tayari kukataa kishawishi cha kutumbukizwa katika matumizi haramu ya dawa za kulevya na utumwa mamboleo pamoja na kumezwa na malimwengu. Vijana wawe ni mashuhuda na vyombo vya furaha, huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Vijana wawe ni majembe makini ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili, ushuhuda unaofumbatwa katika mshikamano na ushuhuda wa Injili ya huruma ya Mungu.
Vijana wanapaswa kusimama kidete kutekeleza dhamana na wajibu wao katika maisha na kwa njia hii, wataweza kuleta mageuzi makubwa duniani. Vijana wakimtumaini Mungu, wataweza kuona maajabu, kwani atawasaidia kuvunjilia mbali malango ya maisha yaliyofungwa kutokana na mwelekeo finyu. Vijana wanapaswa kuwa ndoto ya maisha bora zaidi, tayari kucheza fainali za maisha yao bila mzaha, ili kuamua mustakabali wa maisha yao kwa siku za usoni. Vijana wawe ni vyombo vya upatanisho, umoja na uumbaji kwa kuendelea kushiriki katika ujenzi wa dunia iliyo bora zaidi.
Vijana wanaposikia wito na mwaliko kutoka kwa Mwenyezi Mungu, wawe wepesi kuchangamkia kwani anawafahamu kwa kina na mapana; wema na uzuri wao; mapungufu na dhambi zao. Vijana wasikubali kuwa ni majumba ya makumbusho katika maisha, bali wachakarika daima ili kuacha chapa katika historia. Wawe na ujasiri wa kusimama kidete kulinda na kudumisha umoja na mshikamano; kwa kuendeleza majadiliano katika ukweli na haki; kwa kujenga na kudumisha madaraja ya watu kukutana badala ya kuta zinazowatenga watu kwa vita, nyanyaso na dhuluma. Daraja la kwanza lijengwe katika maisha, utu na heshima ya binadamu. Daraja la udugu ni muhimu sana na vijana waoneshe jeuri ya kuacha chapa katika maisha kwa kujikita katika imani, matumaini na mapendo!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Comments
Post a Comment