MKAKATI WA KUIMARISHA USHUHUDA WA INJILI YA FAMILIA
Baraza la Maaskofu Katoliki Singapore limeanzisha mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji kwa ajili ya utume wa maisha ya ndoa na familia, ili kusaidia mchakato wa majiundo makini kwa wanandoa watarajiwa, dhamana itakayotekelezwa kwa umakini mkubwa na wanandoa ambao wamefunga pingu za maisha walau kwa takribani miaka mitano, ili kutoa ushuhuda kuhusu: maisha, utume, changamoto, fursa na matatizo ambayo wanandoa wanaweza kukabiliana nayo katika maisha, ili tangu mwanzo waweze kuwa “ngangari” ili kukabiliana nayo katika mwanga wa Injili na Mafundisho ya Kanisa.
Mama Caroline Theseira, Mratibu wa mradi huu anasema, una mwelekeo wa pande mbili kwanza kabisa, Kanisa nchini Singapore limeona kwamba, kuna haja ya kuwa na wanandoa ambao ni mfano wa kuigwa, ili kusaidia majiundo awali na endelevu kwa wanandoa watarajiwa ili kutambua dhamana, wajibu, changamoto, fursa na matatizo wanayoweza kukumbana nayo katika uhalisia wa maisha ya ndoa na familia. Majiundo haya kwanza kabisa yatajikita katika safari ya wanandoa watarajiwa kwa kuwapatia ushauri makini katika maisha na utume wao.
Sehemu ya pili ni majiundo makini juu ya mafundisho tanzu ya Kanisa kuhusu ndoa na familia, somo litakalotolewa kwa njia ya video kuhusu: Sakramenti ya ndoa, taalimungu ya mwili wa mwanadamu na saikolojia ya mahusiano kati ya wanandoa. Mbinu mkakati huu una pania pamoja na mambo mengine ni kutoa ushauri wa kisaikolojia kwa matatizo maalum, ili kuwawezesha wanandoa watarajiwa kujifahamu na kufahamiana zaidi, ili waweze kuwa na mawasiliano bora zaidi.
Bwana John Hui, Rais wa tume ya ndoa na familia anasema, ili kweli wanandoa watarajiwa waweze kuwa na uzoefu wa maisha kadiri ya mwanga wa Injili ya Kristo na Mafundisho ya Kanisa, ili kuwasaidia wanandoa watarajiwa kujikita katika urafiki na ushuhuda wa Injili ya familia, inayopasa kukita mizizi yake katika akili na nyoyo za watu.
Baraza la Maaskofu Katoliki Singapore limeamua kutekeleza kwa makini changamoto inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa kitume “Furaha ya upendo ndani ya familia” “Amoris laetitia” unaokazia umuhimu wa Jumuiya ya Wakristo kuzama zaidi katika majiundo makini: awali na endelevu kwa wanandoa watarajiwa, ili waweze kusimika maisha yao katika mwanga wa Injili na Mafundisho ya Kanisa.
Vijana wanapaswa kujifunza namna ya kupenda na kupendwa, ili kuondokana na upendo wa “ghafla bin vu”! ambao matokeo yake ni ndoa za mpito zinazovunjika hata kabla ya kuanza safari. Ikumbukwe kwamba ndoa ni wito unaojikita katika: upendo, imani na matumaini; uvumilivu, udumifu na ukarimu; mambo yanayopaswa kububujika kutoka katika undani wa maisha ya wanandoa, wanaotaka kusakata rumba la maisha ya ndoa na familia kwa kujikita katika matumaini kwa Kristo na Kanisa lake!
Vatican.
Comments
Post a Comment