BENKI YA MKOMBOZI YAZINDUA MIKOPO YA NHIF


Benki ya Biashara Mkombozi , ambayo ni moja ya benki zinazokuwa kwa kasi nchini, imezindua rasmi huduma ya mikopo ya Mfuko wa Bima ya Afya kwa vikundi vya wajasiriamali wadogo wadogo na wa kati.

Huduma hiyo imezinduliwa rasmi  katika ukumbi wa Msimbazi Centre huku wanufaika wakigawiwa kadi zao na uanachama wa NHIF.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Mkombozi, Bi. Edwina A.  Lupembe alisema benki yake imetoa mkopo kwa wanachama hao wapya wa NHIF ambao pia ni wateja wazuri wa benki yake kupitia vikundi vyao vya akiba na kukopa.

“Wote hawa sasa wataweza kupata huduma katika hospitali zilizoainishwa na NHIF kwa kiasi cha Tsh 76,800 kwa mwaka,” alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara ya Mkombozi  amesema huduma hii ni kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali wadogo kupata huduma za afya kwa bei nafuu  ambazo gharama yake ni kubwa.

“Sisi kama Benki ya Mkombozi tumeona umuhimu huu kwani wateja wetu wengi ni wa ngazi za chini na baadhi yao wanapata shida ya huduma za afya na tulipowapa wazo hili la kupata mkopo wa kujiunga na NHIF walilipokea vizuri na leo hii tuko hapa kuzindua rasmi huduma hii na kukabidhi kadi kwa wateja 60 wa awali,” alisema.

Alisema walengwa wa huduma hii ni Wajasiriamali wadogo,wanaojishughulisha na shughuli mbalimbali za kuingiza kipato kama mama lishe, ushonaji, uselemara, genge, kiosk, duka, uuzaji wa mbogamboga, ufugaji.

Wajasilia mali hawa wana lazimika kuunda vikundi vya watu watanowatano ili waweze kwanza kufaidika na  elimu ya ujasiliamali inayotolewa na benki na pia kufaidika na huduma hii ya kujipatia kadi ya matibabu kupitia mikopo kutoka benki.alisema

Naye Bw. Salvatory Okumu wa NHIF aliipongeza Benki ya Mkombozi kwa kubuni huduma hii ambayo imesaidia kutanua wigo wa mfuko huo kwani sasa watu wengi zaidi wataweza kufikiwa hasa wale wa sekta binafsi.

“Wanachama hawa wawaweza kupata huduma kama vile x ray, kujifungua na matibabu mengine kwa mwaka mzima kwa Tsh 76,800 tu ambayo benki imeshakubali kuwakopesha, ni wajibu wa vikundi mbalimbali kutumia fursa hii ili wanachama wake wanufaike na huduma hii,” alisema.

Mkombozi Commercial Bank Plc ilianzishwa mwaka 2009 na kanisa  Katoliki Tanzania na taasisi zake kwa madhumuni ya kusaidia wafanyabiashara wadogo, wa kati na wakubwa kupata huduma za kifedha. 

Ili kutanua wigo zaidi, waanzilishi wa benki hiyo walitoa nafasi kwa watanzania wengine wakiwemo wafanyabiashara na wawekezaji ili kuongeza nguvu. 

Pichani
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara Mkombozi, Edwina Lupembe (kushoto) akimkabidhi kadi ya bima ya Afya, Asia Bakari ( wa pili kushoto) wakati wa hafla ya uzinduzi wa huduma ya mikopo ya NHIF, jijini Dar es Salaam jana ikiwa ni ushirikiano kati ya benki hiyo na NHIF.  Wengine kutoka kulia ni mwakilishi wa mfuko huo, Salvatory Okumu na Meneja wa Tawi la Msimbazi wa benki hiyo, Rigobertus Msuba.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI