SHEREHE YA BIKIRA MARIA KUPALIZWA MBINGUNI


Tarehe 1 Novemba 1950, Baba Mtakatifu Pio wa kumi na mbili katika waraka wake wa kitume “Munificentimus Deus” alitangaza kuwa fundisho la imani kwamba “Imakulata, Mama wa Mungu ambaye daima ni Bikira, amepalizwa mbinguni mwili na roho baada ya kuhitimisha safari yake ya hapa duniani”. Hii ilitokana na sababu kwamba tangu mwanzo Kanisa limekuwa linamwadhimisha Mama Bikira Maria kama Eva mpya huku akihusianishwa na Adam mpya, mwanaye Bwana wetu Yesu Kristo. Hii ndiyo sherehe ambayo tunaiadhimisha leo hii ambapo mmoja ambaye ni binadamu kama sisi anachukuliwa moja kwa moja mbinguni baada ya maisha ya hapa duniani.
Ujio wa Kristo hapa ulimwenguni na kupitia mahubiri na maisha yake ya kila siku kadiri Injili inavyoshuhudia ni udhihirisho kwamba sisi wanadamu tumepewa uwezo ambao umefichika ndani mwetu wa kuishi kwa kufuata mapenzi ya Mungu na hivyo kuepa mienendo ya kidunia. Ni ufafanuzi juu ya hulka yetu ambayo ilikusudiwa na Mwenyezi Mungu tangu mwanzo wa Ulimwengu wa kuwa watoto wake na kutenda kadiri ya mpango wako mahsusi. Mtume Paulo anatuambia kwamba: “... aliyetubariki kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu war oho, ndani yake Kristo, kwa vile alivyotuchagua katika yeye kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, ili tuwe watakatifu na watu wasio na hatia mbele zake katika pendo. Kwa kuwa alitangulia kutuchagua, ili tufanywe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo, sawasawa na uradhi wa mapenzi yake” (Ef 1:3 – 5).
Hivyo ujio wake Kristo unatufanya tuweze kuvumbua tena uwezo huo uliofichika ndani mwetu na hivyo kuwa na mahusiano mapya na Mungu. Mtume Paulo anaonesha katika somo la pili jinsi ambavyo tuliipoteza hadhi hiyo baada ya dhambi ya Adamu lakini katika Kristo, Adamu wa pili tunaipokea tena hadhi hiyo. Kristo anaturudisha tena katika utukufu wa Mungu. Kwa sababu ya “ndiyo” ya Mama yetu Maria, Bikira daima ndipo tunaupokea upya huu wa maisha. Kwa utii wake Mama yetu Bikira Maria tunaletewa wokovu. Ni tukio la kutafakarisha kwamba Mwenyezi Mungu anaponuia kupyaisha tena ubinadamu wetu anamtumia mwanadamu aliye tayari kushirikiana na neema ya Mungu ili kumfanya Mungu autwae ubinadamu wetu na kuupyaisha tena. Mwanadamu huyu ni Mama yetu Bikira Maria, binti huyu wa Yuda anaibuka shujaa na kustahilishwa kuchukuliwa juu mbunguni mwili na roho.
Naye heri aliyesadiki; kwa maana yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana”. Hii ni shangilio la Elizabeti, shangazi yake Mama yetu Bikira Maria kwa sababu ya utii wa binamu yake kwa mapenzi ya Mungu. Imani yake kubwa na kamilifu daima iliujaza moyo wake furaha kuu na hivyo daima alitafuta kuyatimiza yaliyo mapenzi ya Mungu. Utii huu kwa wito wa Mungu ni tendo ambalo humwelekeza mwanadamu kutoa kipao mbele kwa neno la Mungu. Ni kwa tendo hili la utii ndipo mwanadamu anaweza kuujenga ufalme wa Mungu hapa duniani.
Jukumu kubwa alilonalo mwanadamu ni kuweka uwiano mzuri kati ya mahitaji yake ya kimwili na yale ya kiroho. Mara nyingi hutokea kuyapiga teke mahitaji ya kiroho kwa kuvutiwa na tama za kimwili ambazo hazijali kabisa matakwa ya kiroho. Matakwa ya kiroho yanamjali mwanadamu mzima kimwili na kiroho kwa kuwa “roho ndiyo itiayo uzima na mwili haufai kitu”. Roho hupokea maagizo ya Mungu  aliye fundi mkuu na kuyaelewa. Roho inapokuwa na utii kwa sauti ya Mungu ndipo hapo ufalme wa Mungu unaanza kustawishwa hapa duniani. Dhambi iliutenganisha mwili na roho na kuusadikisha mwili kwamba unao uwezo binafsi wa kutenda na kuamua kadiri unavyotaka. Mwili ulisadikishwa kuwa na uwezo wa ajabu wa kujiamulia mambo yake kinyume na matakwa ya Mungu kwa kuwa tangu mwanzo shetani alimsadikisha mwanadamu kuwa akiacha kumtii Mungu atakuwa na uwezo wa kujua mema na mabaya.
Ndiyo ya Mama yetu Bikira Maria iliufanya utukufu wa Mungu uanze tena kung’ara katika mwanadamu kwa sababu utii wake huu ulitupatia Mkombozi Bwana wetu Yesu Kristo. Utayari wake wa kushirikiana na mpango wa Mungu ulimfanya afaulu na hivyo kutakatifuzwa. Somo la kwanza linatudokezea kwamba alipokuwa karibu kumzaa mwanae wa pekee Bwana wetu Yesu Kristo, Mwana wa Mungu na Mfalme wa utukufu, Bikira Maria alikuwa anameremeta mno na Bwana alikuwa pamoja naye. “Ishara kubwa imeonekana mbinguni, mwanamke aliyevikwa jua, na mwezi chini ya miguu yake, na taji la nyota kumi na mbili juu ya kichwa chake”. Shetani alikuwa anatafuta namna ya kumnyakuwa lakini alishindwa kwa sababu Bwana yu pamoja naye.
Mwisho wa maisha yetu hapa duniani hututamanisha kuunganika na Mungu katika utukufu wake. Hali hii inawezekana pale tunapokuwa tayari kuyaekeza maisha yetu katika mapenzi ya Mungu. Tuyakumbuke maneno ya Kristo kwamba “mtu hataishi kwa mkate tu, ila ni kwa kila neno litokalo kinywani mwa Mungu”. Maisha yetu hapa duniani yanapata maana si katika kula, kunywa na kuvaa au katika kuufurahisha mwili bali ni katika kuyafanya yote kwa ajili ya sifa na utukufu mkuu wa Mungu. Sherehe hii ya leo inatukumbusha kwamba wajibu wetu wa kikristo ni kuwa tayari katika kisikiliza sauti ya Mungu. Utakatifu si tunu tunayoipokea mwisho wa maisha yetu tu bali ni jumla ya matendo yetu yote wakati maisha ya hapa duniani. Mwisho wa yote haya ni kupokea taji ya utukufu mbinguni. Hivyo ili kuipokea taji hii ya utukufu tunapaswa kuufuata mfano wa mama yetu Bikira Maria, daima kusadiki juu ya mapenzi ya Mungu na daima kusema “na iwe kwangu kama ulivyosema”
Tutaweza kufanikisha hili kwa kulisikiliza daima Neno lake. Hii ni kwa usomaji wa daima wa Maandiko matakatifu, maandishi mbalimbali ya kiroho na kufuatilia mahubiri mbalimbali ya Neno la Mungu. Pia kwa njia ya sala ambayo hutuunganisha daima na Mungu. Mwishoni ni kwa njia ya Masakramenti hususani Sakramenti ya Kitubio ambayo hututasa dhambi zetu na kutuunganisha tena na Mungu na Sakramenti ya Ekaristi Takatifu ambamo tunaunganishwa Kristo na kutufanya wamoja pamoja naye na hivyo kutenda pia pamoja naye. Tuombe katika adhimisho la sherehe hii, kwa kupitia maombezi ya Mama yetu aliyepalizwa mbinguni kusudi tuweze kushikiana na neema ya Mungu, tunu tunayoipokea hapa duniani, na kwa njia hiyo tuweze kuuonja utukufu wa Mungu. Tujifunze kwa Mama yetu Bikira Maria kusema “Ndiyo” kwa mapenzi ya Mungu ili kuufanya utukufu wa Mungu utung’arie tungalipo bado hapa duniani.

Kwa hisani ya redio Vatican

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI