KANISA LINAPANIA KUENDELEZA INJILI YA FAMILIA


Kardinali Christoph Schonborn, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Vienna, Austria ambaye alikuwa ni kati ya wawezeshaji wakuu wakati wa uzinduzi wa Wosia wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, "Furaha ya upendo ndani ya familia", “Amoris laetitia” anasema, Wosia huu wa kitume umekuwa na mvuto mkubwa katika vyombo vya mawasiliano ya jamii kwani unagusa maisha na utume wa familia. Baba Mtakatifu katika wosia huu anaonesha jinsi anavyotekeleza dhamana na wajibu wake wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu.
Baba Mtakatifu ameonesha uwezo mkubwa kama mchungaji mkuu wa familia ya Mungu, mwalimu wa imani na maadili baada ya kusikiliza kwa makini tafakari na changamoto zilizoibuliwa na Mababa wa Sinodi wakati wa maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu kwa ajili ya familia. Kardinali Shonborn katika mahojiano maalum na Jarida la Civiltà Cattolica anasema, Baba Mtakatifu Francisko amepyaisha mafundisho ya Kanisa mintarafu “Furaha ya Injili” “Evangelii gaudium” na Kanisa katika ulimwengu mamboleo “Gaudium et spes” nyaraka ambazo zinagusia maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo.
Kuna mabadiliko makubwa katika maisha ya watu, kumbe hapa kuna haja ya kusoma alama za nyakati na kujibu changamoto hizi kadiri ya Mafundisho ya Kanisa, Neno la Mungu na Mapokeo hai. Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake kuhusu maisha na utume wa familia anayaangalia Mafundisho ya Kanisa kama uelewa mpana wa Neno wa Mungu aliyefanyika mwili katika maisha na historia ya binadamu, kwa kusikiliza maswali na changamoto za familia ya Mungu, Baba Mtakatifu ameibuka na wosia wa Furaha ya upendo ndani ya familia, ili kuwawezesha waamini kukutana na Kristo Yesu katika hija ya maisha yao, tayari kuguswa na huruma na upendo wake, ili kuanza hija ya toba na wongofu wa ndani.
Baba Mtakatifu anazungumzia hali halisi ya maisha ya ndoa na familia kwa watu wanaofahamika na kuguswa na maisha na utume wa Kanisa na wala si kama anavyosema mwenyewe watu wa kuchongwa! Familia za kufikirika. Kanisa haliwezi kufumbia macho matatizo, changamoto na fursa zilizopo katika maisha na utume wa ndoa na familia kwa nyakati hizi. Wosia huu unapembua kwa kina na mapana hali ya familia katika uzuri, utakatifu na mapungufu yake yanayohitaji toba na wongofu wa ndani ili kuambata utakatifu wa maisha kadiri ya mpango wa Mungu.
Baba Mtakatifu anatambua uwepo wa dhambi na mazingira yake, anawataka waamini kutubu na kumwongokea Mungu, ili kweli wanandoa waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya familia. Anawaambia waamini kwamba, umefika wakati wa kumwilisha Injili ya huruma ya Mungu kwa kutambua kwamba, watu wote ni wadhambi wanahitaji huruma, upendo na msamaha kutoka kwa Mungu. Anasema, yule anayedhani kwamba, hana dambi awe wa kwanza kumtupia mdhambi jiwe! Ikumbukwe kwamba, mtu anatenda dhambi kwa mawazo, kwa maneno, matendo na kwa kutotimiza wajibu. Mafundisho tanzu ya Kanisa kuhusu Sakramenti ya Ndoa na Familia yamefafanuliwa kinaga ubaga, kwa kuonesha uwezo wa kuwasiliana na watu wa kawaida katika masuala magumu ya maisha, huku akifafanua nidhamu ya Sakramenti za Kanisa. Baada ya maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu kuhusu familia, Baba Mtakatifu anasema, Wosia huu hautoi Sheria na Kanuni za jumla katika mchakato wa kushughulikia matatizo na changamoto za maisha ya ndoa na familia katika ulimwengu mamboleo, bali kinachotakiwa ni uwajibikaji wa kina kwa wahusika katika masuala ya shughuli za kichungaji.
Baba Mtakatifu Francisko katika wosia huu analielekeza Kanisa kujikita zaidi katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa kuendelea kusoma alama za nyakati na kuangalia hali halisi ya wanandoa na mambo ambayo yamesababisha ndoa zao kuvunjika na hatimaye, kujikuta wakiwa katika hali kama hii. Kuna wanandoa wanapoachana wanaamua kuoa au kuolewa, wakati mwingine kwa ajili ya mafao ya watoto wao. Ndoa nyingine zimefungwa pasi na wahusika kuwa na uelewa mpana na wa kina kuhusu mafundisho tanzu ya Kanisa.
Mtakatifu Yohane Paulo II alikwisha kuzungumzia changamoto hizi na kuwahamasisha viongozi wa Kanisa kuwasaidia waamini wanaoogelea katika shida na magumu ya maisha ya ndoa na familia kuendelea kujisikia kuwa ni sehemu ya maisha na utume wa Kanisa. Kwa mwelekeo huu, Papa Yohane Paulo II alikuwa anaanza kufungua ukurasa mpya ili kuwawezesha waamini ambao ndoa zao zilikuwa na mgogoro kutambua kwamba, hata katika dhambi ya mauti, bado wanaweza kuonja: umoja, huruma na upendo wa Kristo Yesu kwa Kanisa lake.
Baba Mtakatifu Francisko baada ya kusikiliza majadiliano ya kina kutoka kwa Mababa wa Sinodi za Maaskofu amependa kuimarisha msimamo huu wa Kanisa wa kuwasaidia waamini kujisikia kuwa ni sehemu ya maisha na utume wa Kanisa licha ya dhambi na mapungufu yao katika maisha ya ndoa na familia. Baba Mtakatifu Francisko anatafsiri na kutekeleza kwa vitendo mafundisho ya Kanisa ambayo tayari yalikwishagusiwa katika nyaraka mbali mbali, ili kuwasaidia waamini kuguswa na neema ya Mungu inayookoa na kuponya.
Kuhusu kupokea Ekaristi Takatifu kwa wana ndoa waliotalakiana na hatimaye kuoa au kuolewa tena baada ya kuzungumza na muungamishaji wake ili kutosababisha kashfa na makwazo kwa waamini wengine, wakati huo Kardinali Joseph Ratzinger akiwa Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa alikaza kusema hakuna sheria za jumla zinazoruhusu mwamini kupokea Ekaristi Takatifu katika hali na mazingira maalum. Huu pia ndio msimamo wa Baba Mtakatifu Francisko hata kwa wakati huu, msimamo ambao ameuonesha katika Wosia wake “Furaha ya upendo ndani ya familia” anasema Kardinali Christoph Schonborn katika mahojiano maalum na Gazeti la “Civilta Cattolica”.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI