TANZIA: MAMA MKUU WA KWANZA WA SHIRIKA LA MT. AGNES CHIPOLE AFARIKI DUNIA
Waamini
wametakiwa kutokata tamaa wanapopatwa na magonjwa, dhiki, mateso na misiba
katika maisha. Hayo yamesemwa hivi karibuni na Padre Camilius Haule naibu wa Askofu mkuu wa jimbo kuu Katoliki Songea wakati wa adhimisho la misa
takatifu ya mazishi ya Sista Ester Mwali OSB aliyekuwa mama mkuu wa kwanza wa
shirika la Mtakatifu Agnes Chipole.
Padre
Camilius amesema kuwa,” tunaguswa na mateso na misiba kwa sababu sisi ni binadamu
tunaonja maumivu, na mateso kwa sababu kifo hakizoeleki na mtu yoyote kati
yetu”. Amesema kutokana na hali hiyo waamini hawana budi kushikamana na
Mungu ili wapate nguvu ya kumwendea Yesu kwa pamoja. Amesema Mungu
ndiye anayejua kwa nini ametuumba na kutupa uzima na kuutwaa tena na Mungu peke
yake ndiye mwenye uwezo wa kumrejeshea mtu maisha yake tena kama alivyofanya
kwa kumfufua Lazaro.
Padre
Camilius amesema, “imani yetu itufanye tuamini kuwa, mateso na misiba
tunayopata hapa duniani yatufanye tutambue kwamba tunapomaliza maisha yetu hapa
duniani tunapokufa na kuzikwa bado kuna uzima, na Yesu Kristu
anatufufua kwani ndiye anayeshika uzima wakila mmoja wetu”.
Amesema Sister Ester alikuwa kielelezo thabiti cha ukomavu wa imani katika kanisa
mahalia, hususani katika jimbo kuu Songea na amekuwa moja ya mafanikio
ya kazi ya uinjilishaji ya wamisionari Wabenediktini toka Ujerumani
katika ukanda wa Kusini mwa Tanzania. Sista Ester alikuwa mtu wa
mang”amuzi na muhimili katika shirika la Mtakatifu Agnes Chipole.
Amesema
kanisa linamzika mtawa aliyekubali kudhihirisha imani yake kwa kuishi mashauri
ya injili, aliyeyatolea maisha yake ya imani katika mikono ya Yesu Kristu na
utume kadiri ya roho ya kibeneiktini. Ameongeza kuwa, Sister Ester alikubali
kuwa kiongozi kwa miaka tisa {9} aliyekuja kutumikia na kutoa maisha yake kwa
ajili ya kanisa.
Ameongeza
kuwa, kanisa na shirika limeondokewa na mmoja aliyekuwa kiungo katika
mwili wa fumbo la Yesu Kristu katika nafsi ya Sister Ester , amewataka waamini
kumwombea Sister Ester kwa mwenyezi Mungu ili aweze kusamehewa makosa yake na
apokelewe katika uzima wa milele.
Sista
Ester Mwali alizaliwa mnamo mwaka 1934, amefariki akiwa na umri wa miaka 82 ya
kuzaliwa na miaka 55 ya nadhiri za kitawa, Aidha alikuwa mtu mwenye
mapendo kwa Mungu na watu, mwaminifu, mvumilivu, mnyenyekevu, hodari mpenda
kupokea na kutoa ushauri.
Sister Tuzo Nyoni, Songea
Comments
Post a Comment