Sakramenti ni alama wazi zinazoonekana na
zenye nguvu ya kuleta neema ambazo aliziliweka Yesu Kristo Mwenyewe na kuzikabidhi
kwa Kanisa ili ziweze kuwaletea wanadamu uzima wa kimungu.
Sakramenti hizo za Kanisa zipo saba ambazo
zimegawanyika katika makundi makuu matatu, kundi la kwanza linahusisha
Sakramenti za Mwanzo ambazo zinamwingiza mwandamu katika kupokea imani kwa Ubatizo,
Kipaimara na Ekaristi Takatifu.
Kundi la pili lina ni Sakramenti za
Uponyaji ambazo ni Kitubio na Mpako wa Wagonjwa na kundi la tatu linaundwa na Sakramenti
za Ushirika na Huduma ambazo ni sakramenti ya Ndoa na Daraja Takatifu.
Kulingana na taratibu na misingi ya
Kanisa Katoliki, Sakramenti ya Daraja Takatifu ni Sakramenti ambayo utume wake ulikabidhiwa
na Kristo kwa mitume wake ambao unaendelea kutekelezwa katika Kanisa hadi
mwisho wa nyakati.
Hivyo, hiyo ni Sakramenti ya huduma ya
Kitume ambayo inajengwa kwa ngazi kuu tatu ambazo ni Uaskofu, Upadre na
Ushemasi.
Sakramenti hiyo humfanya mpokeaji
afanane na Kristo ili ahudumie kama chombo cha Kristo kwa ajili ya wokovu wake
na wa kundi analokabidhiwa kwa kuwekwa wakfu kwa ajili ya kuihubiri Injili,
kuwachunga waamini na kuadhimisha ibada kwa Mungu.
Kwa malengo hayo ya Kristo, Padre Mhango
Thomas Mangi ni miongoni mwa chombo cha Kristo kwa Sakramenti ya Upadre katika
kuadhimisha makuu ya Mungu na kumtangaza Kristo duniani.
Kwa Upadre wake amefanywa kuwa walimu
wa imani kwa muunganiko na Askofu wa Jimbo la mahalia kwa msaada wa waumini na
kanisa zima.
Katika Karamu ya Mwisho, Yesu akiielezea
ibada ya Sakramenti hiyo wakati alipokuwa akila pamoja na Mitume wake Kumi na
Wawili ikiwa ni ishara ya urafiki uliopo kati yao na kuwapa maagizo ya kufanya
katika utume wao, (Mt. 26:26–28; Lk. 22:19–20).
Ni dhahiri wakati wa karamu hiyo, Yesu
aliwapa Mitume mamlaka ya kuendeleza kazi ya yake ndiyo maana baada ya kutwaa
mkate, alishukuru, aliumega na kuwapa wanafunzi wake akisema “Huu ndio mwili
wangu unaotolewa kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu”, vivyo hivyo
baada ya kula alitwaa kikombe akisema, “Kikombe hiki ni agano jipya katika damu
yangu, inayomwagika kwa ajili yenu”.
Mama Kanisa anasisitiza kuwa Mitume
waliyapata mafundisho hayo Siku ya Alhamis Kuu kutoka kwa Yesu Kristo mwenyewe akiwa
katika ukamilifu wake na kuweka Sakramenti ya Daraja Takatifu la Upadre.
Padre ni kiongozi wa kanisa anayehitajiwa
na kundi la Mungu, ndiyo maana Mwinjili Yohane anasema kwa kinywa chake anaweza
kutamka maneno ya Bwana “Mimi ni njia, ukweli na uzima. Hakuna ajaye kwa Baba
ila kwa njia ya mimi” (Yoh. 14:6).
Ni mwaka wa 40 sasa kwa Padre Thomas
Mangi wa Jimbo Katoliki la Singida tangu apate Daraja la Upadre Agosti 01, 1976
na miaka 71 tangu alipozaliwa 1945 ndiyo maana anamshukuru Mungu kwa mema mengi
aliyomjalia.
Katika maadhimisho hayo, Padre Thomas
amemshukuru Mungu na kutumia fursa hiyo kuwaasa Mapadre wawe na ari zaidi
katika utume na uchungaji wao ili waweze kuwatumikia watu vizuri kwa furaha na kwa
kujitoa kama Yesu Kristo alivyowatumikia watu.
Wosia huo unaendana na maneno ya Yesu
Kristo mwenyewe (Yoh.10:11, Marko 10:45) “Mimi ni Mchungaji Mwema, Mchungaji
Mwema hutoa maisha yake kwa ajili ya kondoo, Kwa maana Mwana wa Adamu naye
hakuja kutumikiwa, bali kutumika na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.”
Aidha, amewataka Mapadre wawe macho na
mienendo ya ulimwengu wa utandawazi na mitandao ya kijamii isije kuwachanganya
katika Uchungaji wao na wawasimamie vijana wasijewakamezwa na utandawazi.
Kwa upande wa familia ambayo ndiyo
msingi wa kanisa, Padre Thomas awataka wanafamilia wawe na upendo wa kweli
kuanzia kwa wazazi na watoto.
“Wanafamilia wawe watu wa sala, ndio
maana familia ni msingi wa kanisa, kwa sala tutapata watu wengi kwenye miito
mbalimbali ikiwemo Upandre na Ndoa” alisema Padre Thomas.
Amesema kuwa wazazi waangalie watoto
wao kwa karibu na kuwakinga na ulevi, madawa ya kulevya na makundi yasiyofaa
ambayo yameharibu maadili ya vijana na jamii na wawajenge kulingana na hatari
na changamoto maisha zinazowakabili.
Padre Thomas alipewa Daraja hilo na
Mwasisi wa Jimbo hilo Mhashamu Askofu Bernard Mabula mnamo Agosti 01, 1976
katika kanisa la Parokia ya Itamka (kwa sasa Parokia ya Ilongero) ambapo ndipo
alipoanzia kufanya kazi yake ya kichungaji hadi 1977 ambapo alihamishiwa
Parokia ya Chemchem na kwa ya Mungu hadi 1978.
Mwaka 1979 hadi 1980 Askofu wa Jimbo
wakati huo alimpa fursa ya kwenda kusoma masomo ya Upashanaji habari katika Chuo
cha Maendeleo ya Jamii Nyegezi (NSTI).
Baada ya masomo yake alirudi Jimboni
Singida na kupangiwa kufanya kazi yake ya
kichungaji katika Parokia ya Ntuntu akiwa Paroko kuanzia mwaka 1980 hadi
1989 na baada ya hapo alipangiwa Parokia ya Kiomboi akiwa Paroko Msaidizi
kuanzia mwaka 1989 hadi 1997.
Mbali na kutoa huduma Parokiani, mwaka
1996, Padre Thomas alipata fursa ya kwenda nchini Israel kwa kazi mbili, ya
kwanza ilikuwa ni hija Takatifu na kazi ya pili ilikwenda kwa kusoma kozi ya
Biblia katika Chuo cha Mtakatifu Anna kilichopo Yerusalemu.
Baada ya hija yake nchini Israel, Padre
Thomasi alipangiwa kufanya kazi katika Parokia ya Itaja kuanzia Mwaka 1997 hadi
2004 akiwa Paroko.
Kulingana na mahitaji ya Jimbo,
alihamishiwa katika Chuo cha Katekesi cha Jimbo kilichopo Misuna Singida akiwa
mwalimu na mlezi wa chuo hicho kuanzia mwaka 2004 hadi 2009.
Kulingana na wito wake wa kuhubiri
Injili popote, Padre Thomas alihamishiwa tena Parokia ya Kiomboi kuanzaia mwaka
2009 ambapo alitoa huduma ya kichungaji hadi Agosti 11, 2016. Tarehe hiyo hiyo
alihamia Parokia ya Singida ambapo anaendelea na kazi yake ya Kichungaji.
Zaidi ya hayo, amefanya kazi mbalimbali
za Kitume ndani na nje ya Jimbo Katoliki la Singida ikiwemo kuwa Mkurugenzi wa
Upashanaji Habari Jimbo, Katibu wa Mikutano Baraza la Kichungaji Jimbo,
Mwenyekiti na Katibu wa Umoja wa Mapadre Wazalendo Tanzania (UMAWATA),
Mwenyekiti Dekania ya Singida na Mkurugenzi Katekesi Jimbo.
Kwa kutimiza majukumu yake ipasavyo anamshukuru
Mungu kwa mema mengi anayomjalia, ndiyo maana anasema “Kwa Neema, Upendo na
Huruma ya Mungu nimefika hapa. Nimrudishie Bwana nini kwa ukarimu wake wote
alionitendea?” (Zab.116:12).
Hakika Padre ni Mtumishi wa Mungu
anayejitoa sadaka kwa ajili ya wokovu wa watu wa Mungu, “Kila padre ni kristo
mwingine”. Ni mwanadamu kama wandamu wengine, aiyetwaliwa kati ya watu kwa
mambo yamuhusuyo Mungu (Ebr. 5:1-3).
Katika utume wa Upadre, wakristo wanapaswa
kufahamu kuwa Padre yupo kama Wakristo katika kipindi cha kuzaliwa kama
wanadamu, katika maisha ya kila siku ya furaha na wakati wa huzuni pia, katika
nyakati na sehemu muhimu za maisha ya mkristo Padre yupo, ndiyo maana Mungu
amempatia Padre uwezo wa kuwatakatifuza watu.
Katika mlima wa mizeituni Kristo
aliwapa Mitume wake uwezo wa kuondolea watu dhambi, kubatiza na kufundisha
habari njema kwa watu wote kwa msingi huo, Padre Thomas anaendeleza wajibu huo
wa Kristo ambaye ni Kiongozi wa mataifa yote.
Wanajimbo Katoliki la Singida wanamshukuru
Mungu kwa kuwapa zawadi ya Padre Thomas, katika miaka yake ya Kichungaji
amekuwa mwalimu na kiongozi wa mfano wa kuigwa kwa tabia yake ya uchapa kazi na
kuwapenda watu wote hadi kufika hatua ya kuwaita watoto na vijana “Mzalendo” na
“Mwaananchi”.
Hakika, huu no upendo wa kipekee wa
kuwafanya watu wote kuwa rafiki ambao wanaweza kujifunza kutoka kwake kwa upendo
mkuu alionao kwao.
Upendo huo umemsaidia kufanikiwa kuwajali
anaowafundisha, hasa anapotoa mahubiri kwenye ibada anayoongoza kwa kuwavutia waumini
kwa uwezo aliopewa na Mungu wa kilihusisha neno la Mungu na maisha ya kawaida,
hatua hiyo imewafanya waumini kujenge tabia ya kupenda mahubiri yake yenye
mvuto na hivyo kufanya ibada kuwa hai.
Katika maadhimisho
hayo kumshukuru
Mungu, Ibada ya Misa Takatifu imeongozwa na Askofu wa Tatu Mzalendo wa Jimbo
hilo Mhashamu Askofu Edward Mapunda na kuhudhuriwa na Mapandre, Masista,
viongozi mbalimbali wa Serikali, waumini na wananchi waliofurika katika Kigango
ch a Mvae ambapo ndipo alipozaliwa Padre Thomas Mangi.
Askofu Mapunda alitumia
maadhimisho hayo kwa kutoa neno kwa Mapadre ambapo aliwaasa watumie siku hiyo
ya kumpongeza Padre Thomas kama njia ya kutafakari maisha yao ya kichungaji ili
waweze kuwa wapatanishi na njia ya kuwapeleka waumini kwenye maisha ya
utakatifu waweze kuwamona Mungu kupitia upadre wao.
“Nilikuwa naongea na
Padre Thomas nikamuuliza, nikitaka kukuhamisha unapenda nikupange Parokia gani?
Yeye alinijibu, nipangie Parokia yeyote, mimi kesho yake utanikuta hapo”.
Alisema Askofu Mapunda.
Askofu Mapunda
aliongeza kuwa maneno hayo ya Padre Thomas ni ya hekima ya kupenda kujituma na
kufanya kazi ya Mungu mahali popote.
Ndivyo ilivyotokea
Askofu Mapunda amempa uhamisho Padre
huyo kutoka Parokia ya Kiomboi na kuhamia Parokia ya Singida na
ametimiza ahadi aliyomwambia Askofu wakati wa mazungumzo yao.
Hakika palipo na
mafanikio, hapakosekani kuwa na changamoto, Katika utume wake Padre Thomas
amesema kuwa kuna uvuguvugu wa imani ambapo waumini hawachangamkii imani yao ya
Kikristo kwa kutokupokea sakramenti mbalimbali ikiwemo Kitubio na Ekaristi
Takatifu, maisha ya suria, badala yake wamejikita kwenye siasa na kusahau mambo
ya kanisa.
Ili kukabiliana na
hali hiyo, waumini na watu wenye mapenzi mema wanapaswa kuchangamkia imani yao
ya Kikristo na kutimiza yanayotakiwa na mama kanisa na Mungu.
Changamoto nyingine
ni kuhusu maendeleo ya kanisa, ambapo walei wanatakiwa kushirikiana na Mapadre
katika kulijenga na kutegemeza kanisa katika kutoa huduma, kusimamia na
kutekeleza miradi mbalimbali kwa manufaa ya kanisa.
Jubilee ya miaka 40
ya Padre Thomas imeenda sanjari na Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa huruma ya
Mungu uliotangazwa na Baba Mtakatifu
Francisko Desemba 8, 2015 ambapo kwa namna ya pekee Mwenyezi Mungu ameonesha anavyojali
na kumshirikisha mwanadamu huruma na upendo wake usiokuwa na mipaka.
Ndiyo maana katika
picha yake ya kumbukumbu ya miaka 40 ya Upadre wake, Padre Thomas amenukuu
Barua ya Paulo kwa Wafilipi kuwa dira yake katika utumishi wake “Nayaweza mambo
yote katika yeye aniniaye nguvu” (Fil. 4:13) akionesha ni kwa msaada wa Mungu
tu ndiyo ameweza kufikia hatua hiyo.
Katika kipindi chote
hicho, amekuwa ni Mhudumu wa Neno la Mungu, mtoa Sakramenti za Kanisa na
matendo ya huruma yanayojengwa katika msingi imara wa shughuli na mikakati ya
kichungaji.
Jubilei hiyo imekuwa mwaliko
kwa Padre Thomas kukumbuka kuwa, yeye ameteuliwa kati ya watu kwa ajili ya
mambo matakatifu na kuwekwa wakfu ili kuwa ni chombo cha huruma ya Mungu kwa
watu wake, (Mathayo. 22:14).
Ni neno jema
kumshukuru Mungu kwa kuwajalia Wanasingida mema mengi katika maisha yao amabayo
ni zawadi kutoka kwa Mungu na kuendelea kulibariki Jimbo la Singida ambalo
linaloongozwa na Askofu Edward Mapunda ambaye ni Mwanajimbo na lina jumla ya Mapadre
76.
Mapadre 69 wanatoa
huduma katika Parokia ziapatazo 24 ndani ya jimbo na wengine wanafanya kazi
katika Seminari Kuu mbalimbali nchini na Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) na
Mapadre wengine saba wametangulia mbele ya haki “Raha ya milele uwape Ee Bwana
na Mwanga wa milele uwaangazie, wapumzike kwa amani, Amina.
Na Eleuteri Mangi, MAELEZO
|
Comments
Post a Comment