WIZI WA DAWA:WAZIRI MKUU AONYA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri nchini kuwachukulia hatua watumishi wote wa sekta ya afya wanaojihusisha na wizi wa dawa.

“Fuatilieni na kuwachukulia hatua watumishi wa Zahanati wanaoiba dawa. Hawa hawana nafasi ya kuendelea kufanya kazi kwa sababu ni wauaji,” alisema. 

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo juzi jioni (Jumamosi, Agosti 20, 2016) wakati akipokea taarifa ya mkoa wa Katavi mara baada ya kuwasili mkoani hapa kwa ziara ya kikazi ya siku tatu.

Alisema kila kiongozi kwenye eneo lake ahakikishe dawa zinazopelekwa na Serikali kwa ajili ya kuwahudumia wananchi zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa. Pia ameitaka Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kujenga duka la dawa mkoani Katavi kwa ajili ya kurahisisha upatikanaji wa dawa katika mkoa huu pamoja na mikoa jirani.

Wakati huo huo Waziri Mkuu aliwataka Waratibu wa Elimu katika ngazi ya Kata na Wakuu wa shule za sekondari wasiokuwa na shahada waende wakasome kama wanahitaji kuendelea kuwa na wadhifa huo. 

Alisema Mratibu wa Elimu katika ngazi ya Kata ni lazima awe na shahada ili aweze kutekeleza majukumu yake ya kusimamia utolewaji wa elimu katika shule za sekondari na msingi.

Kwa upande wa walimu wakuu katika shule za msingi, Waziri Mkuu alisema ni lazima wawe na diploma, hivyo aliwataka walimu wakuu wote wasiokuwa na diploma kwenda kusoma kabla hawajaondolewa kwenye wadhifa huo.

Alisema Serikali imetenga zaidi ya sh. bilioni tano kwa mwezi ambazo ni posho ya madaraka, ambapo Waratibu Elimu Kata wanapewa sh 250,000 kwa mwezi huku Wakuu wa shule za sekondari na walimu wakuu katika shule za msingi wanapewa sh. 200,000.
 
Awali Mkuu wa Mkoa wa Katavi Meja Jenerali (Mstaafu) Raphael Muhuga alisema mkoa umeendelea kuongeza bajeti ya dawa ili kuhakikisha dawa zinapatikana katika ngazi zote za kutolea huduma.

“Mwaka 2012 bajeti ya dawa na vifaa tiba ilikuwa sh. Milioni 558 ambayo ilitosheleza upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa asilimia 70. Katika bajeti ya mwaka 2016/2017 mkoa umetengewa jumla ya sh bilioni 1.3 ambayo tunaamini itamaliza tatizo la upatikanaji wa dawa na vifaa tiba,” alisema.

Mkuu huyo wa mkoa alisema mfumo mpya wa usambazaji dawa kupitia MSD umesaidia dawa, vifaa tiba na vitendanishi kupelekwa moja kwa moja hadi katika ngazi ya zahanati hali iliyosaidia dawa kufika kwenye vituo vya kutolea huduma kwa asilimia 100.

Mapema jana Waziri Mkuu alifanya ziara katika hospitali ya Manispaa ya Mpanda ambapo alisema Serikali itahakikisha hospitali hiyo inaongezewa huduma zaidi kwa sababu ni ya wilaya ila inahudumia wagonjwa wa mkoa wote.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, AGOSTI 21, 2016.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI