WAONYESHENI JIRANI ZENU MSAMAHA NA HURUMA YA MUNGU
Maaskofu Katoliki kutoka Umbria, Kaskazini mwa Italia wanampongeza na kumshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwatembelea na kuwatia shime ili waweze kuwa kweli ni vyombo vya huruma na msamaha katika ulimwengu mamboleo, Kanisa linapoadhimisha Jubilei ya miaka 800 ya Msamaha wa Assisi. Baba Mtakatifu amekuwa ni kati ya mahujaji walioshiriki maadhimisho haya ambayo yalifungwa rasmi kwa Ibada ya Misa Takatifu hapo tarehe 2 Agosti, 2016.
Baba Mtakatifu ameonesha kwa mara nyingine tena ile Njia ya Msamaha ambayo inapaswa kuvaliwa njuga na watu wote, kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa dunia kadiri ya mpango wa Mungu na ustawi wa binadamu. Maaskofu wanasema, Baba Mtakatifu Franciko kwa kutembelea Kikanisa cha Porziuncola, Assisi, hapo tarehe 4 Agosti, 2016 ameshiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 800 ya “Msamaha wa Assisi”; rehema kamili iliyoombwa na Mtakatifu Francisko wa Assisi kwa Papa Onorio III kunako tarehe 2 Agosti 1216, yaani miaka 800 iliyopita.
Maaskofu wanaendelea kusema, uwepo wa wakimbizi, wahamiaji na wageni kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria wa Malaika na kwenye Shirika la Caritas Jimbo Katoliki la Assisi ni changamoto kwa wote kuonesha wema na ukarimu kwa watu wanaoteseka na kusumbuka katika maisha yao, ili kuwaonesha uso wa huruma na mapendo. Baba Mtakatifu amewaachia ujumbe wa huruma, msamaha pamoja na kuwaungamisha baadhi ya waamini, kuwa ni kielelezo cha mpango mkakati wa maisha na utume wa Makanisa mahalia. Maaskofu kwa mara nyingine tena, wanapenda kumshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa zawadi ya uwepo na neno lake huko mkoani Umbria.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Comments
Post a Comment