Mapadri msiogope kusema na kusimamia ukweli -Askofu Niwemugizi
“DAIMA
msiogope kuusema ukweli ambao utawaweka watu wa Mungu huru na kutoka katika
mwenendo mbaya usiompendeza Mungu.”
Askofu Severine NiweMugizi wa Jimbo Katoliki
Rulenge Ngara ametoa mwito huo kwa
mapadri wakati wa Misa maalumu ya kutoa Daraja Takatifu la Ushemasi kwa Shemasi
Alex Blandi.
Akiwatia moyo Mapadri, Askofu Niwe-Mugizi
amesema kuwa, msemakweli daima maisha yake yako hatarini lakini wajue utume wao
wameukabidhi mikononi mwa Mungu ambaye atawaongoza na kuwavusha kwa kila
vikwazo hasa vitokanavyo na kusema ukweli.
"Mpendwa Shemasi Alex na Mapadri
kuweni wajasiri kwa kusema ukweli. Najua kuna watu wasiopenda kuusikia ukweli
na mkweli daima huchukiwa na maisha yake yamo hatarini, yawekeni maisha yenu
mikononi mwa Mungu matahifadhiwa naye," amesema.
Aliwahimiza mapadri daima kuwa wavumulivu,
wenye subira, wenye kusamehe wasiokata tamaa . Pia kuwa wabunifu kwa kuwa na muda wa kusema na
muda wa kunyamaza.
Aidha Askofu Niwemugizi alielezea hali
ambayo iliandikwa kwenye vyombo kadhaa vya habari kuwa yeye anaonekana wazi
kumpinga Rais Magufuli juu ya suala la kutangaza uwepo wa njaa au ukame .
Alisema yeye binafsi hana ugomvi na
Magufuli na kwamba anampenda sana kutokana kuwa miongoni mwa watu wanaosema
ukweli na pia kusema wazi kuwa anapendezwa naye na utendaji kazi wake
Amesisitiza juu ya miito huku akisema
kuwa, wazazi wengi hawatambui miito ya watoto wao na hivyo wamekuwa wakishindwa
kuwaendeleza hasa wanapoelekea kuwa na wito wa kumtumikia Mungu kama Mapadri.
Alihimiza familia kuwa chanzo cha miito
mitakatifu ya Upadri na Utawa na kuacha kutamani wito wa ndoa.
"Nawasihi wazazi heshimuni miito
ambayo Mungu amewaitia watoto wenu na hasa miito hii ya Upadri na Utawa ambayo
wengi wenu hamuipi kipaumbele kwa kudhani kuwa mtoto akiwa Padri au Mtawa
mtakosa wajukuu. Kumbukeni miito hii ni sadaka yenu kwa Mungu," amesema.
Comments
Post a Comment