Miaka 100 ya upadri Tanzania Bara imewaunganisha waafrika
Askofu wa Jimbo Katoliki Morogoro Mhashamu Telesphor
Mkude amesema kuwa kufikia miaka 100 ya upadri tangu kuingia Tanzania Bara,
kumeleta mafanikio ya kufahamiana, kuimarishana na kufikiri pamoja katika
masuala ya imani kujenga Kanisa la Mungu.
Amesema hayo
ofisini kwake hivi karibuni alipokuwa akizungumza na gazeti hili juu ya
maadhimisho ya Jubilei ya miaka 100 ya Upadri Tanzania Bara, ambayo kilele
chake kitaadhimishwa kitaifa katika Jimbo Kuu Katoliki Dodoma katikati ya mwezi
Agosti mwaka huu.
Askofu Mkude
amesema kuwa kufuatia jubilei hiyo ya miaka 100, imekuwepo idara maalumu
inayohusika na Mapadri nchi nzima, (UMAWATA) ama Umoja Wa Mapadri Wazalendo Tanzania
ili kuendeleza na kufwata misingi iliyoachwa na wamisionari, na kukabili yaliyopo
kwa sasa ili kujenga imani ya kweli ya Kanisa na sheria zake
Hata hivyo Askofu
Mkude amesema moja ya majukumu ya mapadri ni utumishi katika kuratibisha,
kuhubiri, kutoa masakramenti, kuongoza waamini, kuelekeza waamini ndani ya Kanisa,
hasa jumuiya na makundi mbalimbali katika Kanisa ili viweze kuwa ndani ya
mchungaji mmoja
Sambamba na hayo
amefafanua kuwa si vyema Kanisa kutawaliwa na Maaskofu na Mapadri pekee.
“Kanisa linapaswa
kutawaliwa na walei wenyewe ndani ya Kanisa kwa kupewa maelekezo, kushirikishwa
mambo mbalimbali ndani ya Kanisa ili kueneza uinjilishaji wa kina,” amesema
Askofu Mkude.
Amesema kuwa
wazo la mapadri kuendelea kushirikiana katika mambo ya kiroho, nchi za AMECEA
yaani Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Afrika Mashariki na Kati ikiwemo nchi
ya Kenya, Uganda, Madagascar, Ethiopia, Malawi, Zambia, Tanzania, Sudan na
Somalia.
Hawa ni waafrika
ambao wameungana kufanya mambo mbalimbali katika uinjilishaji wa kina kufikisha
mwanga wa injili ulimwenguni pote kwa lengo la kuwatumikia watu.
Wakati huohuo
Askofu mkude ametoa pongezi kwa waamini kwa jitihada zao za kuwaombea viongozi
wa dini, akisema kuwa sala za waamini ni muhimu sana bila sala hizo hawawezi
kusimama imara katika imani, kwani mchungaji anapoanguka kiroho anaanguka na
watu kadhaa.
“Msichoke
kuwaombea viongozi wa dini, kwani sala zenu waamini ni muhimu sana, bila sala
hizo hatuwezi kusimama imara katika imani, kwani mchungaji anapoanguka kiroho
anaanguka na watu kadhaa,” amesema Askofu Mkude.
Kufikia miaka
100 ya upadri Tanzania Bara, kumeongeza idadi ya Maaskofu na Mapadri waafrika
kuwa wengi zaidi na uwepo wa seminari ndogo na kubwa kama kielelezo cha kuendelea
kufahamiana zaidi kiasi kwamba uwepo wa seminari hizo humsaidia padri
anaposafiri kwenda Jimbo jingine hukutana na mapadri wengine anaofahamiana nao.
Comments
Post a Comment