Maridhiano baina ya walezi huleta ufanisi katika malezi
KUMEKUWA
na hulka tofauti tofauti za walezi kuhusu matokeo ya malezi wanayowapatia
watoto wao. Mtoto anapokuwa na mafanikio huwa ni mali ya Baba ila anapokuwa
hajafanya vizuri anakuwa ni mali ya Mama.
Kwa mfano, utamsikia Baba
akitoa kauli unaona huyu mtoto wako alivyo
mkorofi! ila akiwa ni afisa fulani kwa maana ya mafanikio bora baba
atajigamba kila kona mnamwona mtoto wangu, pale nimetoa jembe
bwana!
Ni katika maana hii nadiriki kusema
kuwa malezi ni suala mfungamano, yaani ni maridhiano ya mama na baba kuhusu
namna ya kutoa malezi ili matokeo yawe ni mali ya wazazi wote wawili.
Kulea: Ni
kazi ya wote wawili. Hakuna mwenye majukumu hayo alafu mwingine afurahie au
achukie matokeo yake. Mara nyingi malezi ya watoto kwa maana ya kugombeza, kufundisha
kazi, na hata kuhangaikia elimu limekuwa ni jukumu la mama kwa walio wengi.
Ni lazima kutambua kuwa kazi ya
kulea ni ya wote wawili iwe ni wakati wa kufaa au la, yaani isiwe baba yuko kimya
anayeadhibu ni mama peke yake, hapo ni rahisi kwa mtoto kuelewa kuwa ni mama
ndiye aliyenilea kwa hiyo baba si mlezi wangu.
Kuwapatia
watoto majina: Hili nalo pia ni suala muhimu katika malezi. Ni
taratibu katika mila nyingi kuwapa watoto majina ya wazazi wao. Kwa mfano kama
baba yako aliitwa Samweli ukizaa mtoto utamwita Samweli. Ni maridhiano katika
kutoa majina haya kutakapoleta tija katika malezi kwani kumekuwa na mvutano kwa
walio wengi kuita majina mengi ya upande mmoja bila kufikiria mwingine.
Hii inachangia malezi hafifu
kwani upande mmoja utaona haukuthaminiwa hivyo mwenye watoto alee mwenyewe
watoto wake.Ni suala la kukubaliana kwa haki kabisa kugawana wazao kwa maana ya
kuwapa majina ya pande zote mbili kwa makubaliano maalumu la sivyo mmoja ataona
hana haki ya kulea.
Dini
kwa watoto ni makubaliano: Watoto wanaelekezwa dini fulani waifuate na wazazi wao. Suala hili ni muhimu
katika malezi kwani kumekuwa na kasumba ya upande mmoja kuvutia watoto upande
wake bila kukaa na kukubaliana watoto wawe katika msingi gani wa imani ili kuwa
rahisi kuwafuatilia.
Ni mshangao kuona familia moja
kuwa na dini zaidi ya nne au madhehebu zaidi ya manne. Je mtawaleaje watoto
hawa? humo ndani si itakuwa ni mafarakano ya kidini tu ? ”wasabato hawali
kambale, waislamu hawali nguruwe ,wahindu hawali ngombe..je wakatoliki ndani ya
nyumba hiyo wataishije” alisema rafiki yangu mmoja Aloisi nilipomhoji ]
Je itakuwaje humo ndani?Ni
vyema kukubaliana kuwa watoto wakue katika maadili Fulani ya kidini ili wote
muweze kuelekeza nguvu katika imani hiyo mnayotaka watoto wenu wawe nayo.
Kutembelea
familia ya upande mwingine: Kuna utaratibu mzuri katika jamii nyingi
kutembeleana. Utaratibu huu unashirikishwa pia kwa watoto pale wanaporuhusiwa
kulala kwa bibi au babu. La kushangaza ni pale watoto wanaporuhusiwa kutembelea
upande mmoja tu na kukatazwa upande mwingine.
Hii haifai kwa malezi kwani
lengo la kuwaruhusu kutembeleana ni ili wafahamu ndugu wa pande zote mbili. Unapowakataza
upande mmoja basi wanaanza kukua na chuki kuwa upande wa mama kwa mfano ndugu
zake ni wabaya na haturuhusiwi kuwatembelea na kukaa nao. Walezi jitahidini
kuwa na mfumo mmoja, kama ni kuwakataza wakatazeni pande zote mbili kama ni
ruhusa toeni kwa pande zote mkizingatia kiasi na uhuru wenye mipaka.
Malezi ni suala la pamoja baina
ya pande mbili,ni vyema kujenga mfumo wa pamoja ili kuwafanya watoto wasiegemee
upande mmoja na kudharau mwingine. Hili linawajengea walelewa uwezo wa kutambua
kuwa katika maisha zipo pande mbili yaani malezi toka kwa mama na Baba ambayo
kamwe hayatengani, hivyo si rahisi kwa watoto kupinga malezi wakiona
wanayoelekezwa yanatoka kwa wote wawili [baba na mama]
Mwandishi
ni Paroko wa Parokia ya Ndungu
Jimbo
Katoliki la Same.
Comments
Post a Comment