Elimu ndogo ya katekesi chanzo cha uchanga wa imani kwa waamini
IMEELEZWA
kuwa katekesi ndogo na isiyotosha ya sakramenti na maadhimisho ya liturujia ni
chanzo cha uchanga wa imani kwa waamini na hata kupelekea kuhama makanisa.
Hayo yamebainishwa na Padri
Titus Amigu wa Jimbo Katoliki Lindi wakati akitoa mada katika mkutano wa siku
tatu wa Mapadri wanaounda Umoja wa Mapadri Tanzania (UMAWATA), uliofanyika
katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).
Padri Amigu amewataka mapadri
kufundisha katekesi ya kina ili kuwasaidia waamini waelewe vyema badala ya
kuwaachia makatekista pekee. Amekumbusha kuwa katekesi ni muhimu kwa waamini
hasa kujifunza kuhusiana na sakramenti na maadhimisho ya liturujia kwa jumla.
“Sisi wenyewe tunasomea vyema
huko Seminari Kuu na bado hatufanyi vizuri, je, kwa ndugu wasioelewa? Watu wetu
huambulia katekesi ndogo kwa ajili ya ubatizo, kipaimara na komunio ya kwanza
na kidogo tu kabla ya kufunga ndoa. Zaidi ya hapo katekesi yenyewe hufanywa kwa
uzimamoto na pengine kwa kuachiwa katekista tu. Mkasa huu unabakiza watu wetu
katika utoto wa imani na hivyo kuwa wahanga wa mafundisho ya kigeni na
kuhamahama makanisa kwa vile hawaoni tofauti yoyote kati ya makanisa” ameeleza
Padri Amigu.
Ametaja madhara ya waamini
kukosa elimu ya katekesi kuwa ni pamoja na kudharaulika kwa sakramenti hususan
Ubatizo, Ekaristi Takatifu, Kitubio, Mpako wa Wagonjwa, Ndoa na Upadri.
“Lakini siku hizi, pengine kwa
sababu ya sisi kutoeleza na kufanya katekesi ya sakramenti, sakramenti kadhaa
zinadharaulika. Hazijulikani faida yake wala umuhimu wake. Ukichanganya na
teolojia ya Martin Luther, sakramenti saba zinashambuliwa kwa kejeli nyingi.
Matokeo yake ni kudharaulika. Ubatizo unaonekana hauna uzito mbele ya “ubatizo katika
Roho”. Mahali pengine watu hawaithamini Ekaristi Takatifu wakati ndiyo kiini cha maisha ya padre na
maisha ya Mkatoliki yeyote” amesema.
Aidha Padri Amigu ametoa wito
kwa mapadri kutoogopa kuonya kwa kuwa Nabii hapaswi kuwa mwoga kwa sababu
anasimamia ukweli. Amesema kuwa kama mlinzi wa kundi la wafuasi wa Kristo na
mtu anayewajibika kuwafikisha sala mbinguni kondoo wake, padri anapaswa
kutimiza ofisi yake ya unabii pasipo kuogopa.
Lakini siyo uongo mapadri mara
kadhaa tunarudi nyuma katika unabii kwa
kuchelea kuharibu uhusiano wetu na watu. Tunafumbwa vinywa na kutengenezwa
mabubu na matokeo yake tunakuwa viwete mbele ya yote yanayohatarisha
mustakabali wa kiimani katika parokia au taasisi tulizopewa dhamana” ameeleza.
Pia amewaomba mapadri kuwekeza katika
watoto na vijana akisema kuwa hiyo ni busara ya kutaka kuvuna mavuno mazuri na
makubwa siku za usoni. Amesema kuwa kushindwa au kudharau kuwekeza katika
watoto na vijana, kwa kujua au kwa kutokujua, ni kufanya kosa kubwa.
Comments
Post a Comment