LINDENI IMANI YENU-PAPA FRANSISKO
Wazazi wanapowaombea watoto wao Ubatizo wanapaswa kufahamu wajibu wanaoupokea, yaani kuwafundisha imani ili wapate kushika Amri za Mungu na kuwapenda jirani zao kama Kristo alivyowapenda na kuwafundisha wafuasi wake. Wasimamizi wa Ubatizo wanayo dhamana ya kuwasaidia wazazi wa watoto waliobatizwa kutekeleza dhamana na wajibu wao barabara na kwamba, Padre kwa niaba ya familia ya Mungu anawapokea watoto na kuwatia ishara ya Kristo Mkombozi!
Kwa njia ya Fumbo la Msalaba, watoto wanazaliwa upya kwa maji na Roho Mtakatifu tayari kutembea katika Mwanga wa Kristo Mfufuka, kwa kumkataa Shetani na mambo yake yote! Lengo ni kuwawezesha watoto hawa baadaye, kusikiliza kwa makini Neno la Mungu, kuungama Imani kwa Kristo na Kanisa lake kwa sifa na utukufu wa Mungu! Baba Mtakatifu Francisko, katika maadhimisho ya Siku kuu ya Ubatizo wa Bwana, Jumapili, tarehe 8 Januari 2017 ametoa Sakramenti ya Ubatizo kwa watoto 28 wa wafanyakazi wa Vatican. Ibada hii imeadhimishwa kwenye Kikanisa cha Sistina, kilichoko mjini Vatican.
Baba Mtakatifu katika mahubiri yake, amewakumbusha wazazi na wasimamizi wa watoto waliobatizwa kwamba, watoto wao wamepewa imani kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo! Hii ni imani inayopaswa kuendelea kumwilishwa katika maisha si tu kwa kukiri Kanuni ya imani wakati wa maadhimisho ya Misa Takatifu, bali imani inapaswa kuwa ni kielelezo cha maisha ya Mkristo. Hii ni imani inayofumbatwa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, Sakramenti za Kanisa, Amri za Mungu na Maisha ya Sala! Kwa ufupi huu ni muhtasari wa Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki inayopaswa kuwa ni dira na mwongozo wa maisha ya waamini. Ni imani kwa Mungu Baba Muumbaji, Mungu Mwana Mkombozi na Mungu Roho Mtakatifu anayelitegemeza na kulitakatifuza Kanisa la Kristo! Wazazi na walezi wa watoto waliobatiza wanapaswa kuwafundisha watoto wao mafundisho tanzu ya Kanisa kwa njia ya ushuhuda wa imani tendanji, ushuhuda wenye mvuto na mashiko!
Watoto waliobatizwa wamepewa na wazazi wao mshumaa unaowaka, kielelezo cha Kristo Yesu, Mwanga wa Mataifa! Imani inapaswa kuyaangazia maisha ya watu, ili kuona matukio ya maisha ya mwanadamu kadiri ya mwanga wa Injili. Mama Kanisa amewakirimia watoto waliozaliwa kwa maji na Roho Mtakatifu zawadi ya imani, kumbe, sasa ni wajibu na dhamana ya wazazi na wasimamizi wa Ubatizo kuhakikisha kwamba, imani hii inalindwa, inakuzwa na kudumishwa, ili iweze kuzaa matunda ya utakatifu unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha!
Baba Mtakatifu anakaza kusema, wanapaswa kulinda, kukuza na kushuhudia imani yao kwa wale wanaowazunguka! Watoto wanaolia Kanisani anasema Baba Mtakatifu ni tamasha la muziki mtamu, kwani pengine wameamshwa mapema ili kuhudhuria Ibada ya Ubatizo! Watoto wengine wanalia kwa vile tu wamesikia kilio cha watoto wenzao. Baba Mtakatifu anasema, mahubiri ya kwanza ya Yesu, kilikuwa ni kilio chake kwa mara ya kwanza alipozaliwa! Watoto wanalia kwa sababu wana njaa, mwaliko kwa akina mama kuhakikisha kwamba, wanawanyonyesha watoto wao kwa raha zote kama alivyofanya Bikira Maria kwa Mtoto Yesu! Baba Mtakatifu Francisko amewakumbusha wazazi kwamba, wamewaombea watoto wao imani inayopaswa kulindwa, kukuzwa na kushuhudiwa kwa familia yote ya Mungu, kama kielelezo cha imani tendaji!
Comments
Post a Comment