SIKUKUU YA UBATIZO WA MKOMBOZI WETU YESU KRISTO


Katika maadhimisho ya Siku kuu ya Ubatizo wa Bwana, Mwinjili Mathayo anamwonesha Yesu akiwa mtoni Yordani kati kati ya wadhambi! Akiwa amejipanga mstarini ili kupata Ubatizo wa toba uliokuwa unatolewa na Yohane Mbatizaji ambaye alitaka kumkataza Yesu asibatizwe naye, lakini, Yesu akang’an’ania, ili kuweza kuwa ni daraja linalomuunganisha Mungu na binadamu! Yesu anamua kubatizwa ili kutimiza haki yote, yaani kutekeleza mpango wa Mungu kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu, kwa njia ya utii na mshikamano na binadamu mdhaifu na mdhambi; njia ya unyenyekevu na utimilifu wa uwepo wa karibu wa Mungu kwa watoto wake wapendwa!
Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili, tarehe 8 Januari 2017 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Yesu Kristo alipokuwa anabatizwa, mara ikasikika sauti kutoka mbinguni ikisema, “Huyu ni mwanangu mpendwa wangu, ninayependezwa naye” na mara Roho Mtakatifu kwa mfano wa hua, akamshukia kama mwanzo wa utekelezaji wa utume wake wa wokovu kwa binadamu; utume ambao unamwonesha Yesu kama Mtumishi mnyenyekevu na mpole aliyevikwa nguvu ya ukweli kama anavyosema Nabii Isaya kwamba, hatalia, wala hatapaza sauti yake, mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi utokao moshi hatauzima; atatokeza hukumu kwa kweli. Baba Mtakatifu anakaza kusema, mtindo wa maisha ya Mmissionari ambaye ni Mtume wa Yesu ni kutangaza Injili kwa upole na uthabiti bila kiburi, majivuno au kuwalazimisha watu. Utume wa kweli kamwe haufumbatwi katika wongofu wa shuruti, bali kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa Kristo na Kanisa lake; kwa njia ya muungano thabiti na Kristo Yesu, unaofumbatwa katika sala; Ibada na matendo ya huruma kwa Kristo Yesu anajionesha kati ya ndugu zake wadogo na wanyonge. Huu ni mwaliko wa kumfuasa na kuiga mfano wa Kristo mchungaji mwema na mwenye huruma! Kwa njia ya neema, Wakristo wanahamasishwa kwa njia ya maisha yao ya furaha kuwa ni mwanga unaoangazia mapito yanayowaelekeza katika matumaini na upendo.
Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwamba, Siku kuu ya Ubatizo wa Bwana inawafanya waamini kung’amua uzuri wa kuwa ni watu waliobatizwa, yaani wadhambi waliokombolewa kwa njia ya neema ya Kristo na kuingizwa katika kazi ya Roho Mtakatifu inayowafanya kuwa ni ndugu zake Kristo kwa njia ya Baba wa milele kwa kupokelewa katika Tumbo la Mama Kanisa na hivyo kujenga udugu usiokuwa na mipaka wala mwisho! Bikira Maria, awasaidie Wakristo kutunza dhamiri hai inayotambua Ubatizo na kuendelea na safari ya wokovu iliyoanzishwa kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, mwanzo mpya wa maisha ya Kikristo!
Baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Baba Mtakatifu aliwaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kuwaombea wazazi na watoto 28 aliowabatiza wakati wa Siku kuu ya Ubatizo wa Bwana. Amewakumbuka na kuwaombea wazazi wanaowaandaa watoto kwa ajili ya Ubatizo au ambao tayari wamekwisha wabatiza. Anawaombea Roho Mtakatifu ili waweze kuishi Sakramenti ya Ubatizo katika imani na furaha. Baba Mtakatifu pia anawaalika waamini kuungana pamoja naye katika Mtandao wa Utume wa Sala unaosambaza nia zake kila mwezi hata kwa njia ya mitandao ya kijamii, ili kujenga na kudumisha umoja wa Kanisa kwa njia ya Utume wa Sala. Kwa vijana waliopokea Sakramenti ya Kipaimara wanakumbushwa kwamba, huu si mwisho wa maisha yao kwa kuanza kubweteka, bali ni mwanzo wa maisha ya Kikristo, changamoto ya kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI