WANAKWAYA, WATUNZI SOMENI HATI YA LITURUJIA YA MTAGUSO MKUU VATIKANI II
Konstitusio juu ya liturujia
SACROSANCTUM CONCILIUM
Paulo Askofu
Mtumishi wa Watumishi wa Mungu
pamoja na Mababa wa Mtaguso mkuu
ataka haya yakumbukwe daima
Mtumishi wa Watumishi wa Mungu
pamoja na Mababa wa Mtaguso mkuu
ataka haya yakumbukwe daima
UTANGULIZI
1. Mtaguso Mkuu (Sacrosanctum
Concilium) umeazimu kukuza kila siku zaidi na zaidi maisha ya kikristo kati
ya waamini; kuzilinganisha taratibu zile zinazobadilika na mahitaji ya siku
hizi; kuyahimiza mambo yale yote yanayosaidia kuleta umoja kati ya wote
wanaomwamini Kristo; kuyaimarisha yale yote yanayofaa kwa kuwaita wote kundini
mwa Kanisa. Mtaguso huu Mkuu unaona ni wajibu wake kujali kwa namna ya pekee
kurekebisha na kukuza Liturujia.
Nafasi ya Liturujia katika fumbo la
Kanisa
2. Maana kwa njia ya Liturujia, hasa
Sadaka takatifu ya Ekaristi, “latimizwa tendo la ukombozi wetu”[1].
Liturujia inasaidia kikamilifu waamini waonyeshe katika maisha yao na
kuwadhihirishia wengine fumbo la Kristo na pia maumbile halisi ya Kanisa la
kweli. Kanisa kwa undani kabisa ni la kibinadamu na pia la kimungu,
linaloonekana lakini lenye yasiyoonekana ndani yake, lenye bidii kubwa katika
matendo na uradhi katika kutafakari, lililopo ulimwenguni lakini kama mwenye
kuhiji. Hayo yote yamo ili yale ya kibinadamu ndani yake yaelekezwe kwa yale ya
kimungu, yaonekanayo kwa yasiyoonekana, matendo kwenye kutafakari, yaliyopo
yaelekee mji ujao tunakoelekea[2].
Hivyo Liturujia kila siku inawajenga wale waliomo katika Kanisa wawe hekalu
takatifu la Bwana, makao ya Mungu katika Roho[3],
mpaka kuufikia utimilifu wa Kristo[4].
Wakati huohuo kwa namna ya ajabu Liturujia inaimarisha nguvu za waamini
kumhubiri Kristo; na kwa njia hiyo inawaonyesha wale walio nje [nalo,] Kanisa
lililo ishara iliyoinuliwa juu kati ya mataifa[5],
ambayo chini yake watoto wa Mungu waliotawanyika wakusanyika katika umoja[6],
mpaka liwepo zizi moja na mchungaji mmoja[7].
Hati hii juu ya Liturujia na Riti
mbalimbali
3. Kwa hiyo Mtaguso Mkuu unadhamiria
kwamba inabidi kukumbusha kanuni zifuatazo kuhusu ukuzaji na marekebisho ya
Liturujia, na kutoa miongozo ya utekelezaji.
Kati ya kanuni na sheria
hizo, zipo nyingi zinazoweza kutumika na lazima zitumike katika Riti*[,
au madhehebu,] ya Kiroma (Ritum romanum) na pia Riti nyinginezo.
Miongozo ya utekelezaji ifuatayo, lakini, ni kwa ajili ya Riti ya Kiroma tu,
isipokuwa kama ni mambo ambayo, kwa maumbile yake yenyewe, yanahusu pia Riti
nyingine.
Heshima kwa Riti zote zilizo halali
4. Mwishowe, Mtaguso Mkuu, kwa
kuheshimu kiaminifu Mapokeo, unathibitisha kwamba Mama Kanisa anastahi kwa
heshima moja Riti zote (omnes Ritus) zilizokubaliwa kuwa halali. Tena
Mtaguso unatamani kwamba [Riti hizo] zihifadhiwe kwa baadaye na kuendelezwa kwa
hali na mali. Aidha, Mtaguso unatamani zitengenezwe upya, kama ni lazima, kwa
utaratibu na kadiri ya Mapokeo halisi na pia zipewe nguvu mpya kulingana na
mazingira ya sasa.
Sura
ya Kwanza
KANUNI
ZA JUMLA ZA MAREKEBISHO NA UKUZAJI WA LITURUJIA TAKATIFU
I - MAUMBILE YA LITURUJIA NA UMUHIMU
WAKE KATIKA MAISHA YA KANISA
5. Mungu, “ambaye hutaka watu wote
waokolewe na kupata kujua yaliyo kweli” (1Tim 2:4), “ambaye alisema zamani na
baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi” (Ebr 1:1),
ulipofika utimilifu wa nyakati akamtuma Mwanawe, Neno wa Mungu aliyefanyika
mwili, aliyetiwa mafuta kwa Roho Mtakatifu, ili awahubiri maskini habari njema,
awagange waliovunjika moyo[8],
yeye aliye “mganga wa mwili na wa roho”[9],
Mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu[10].
Maana ubinadamu wake, katika kuungana na Neno, ulikuwa chombo cha wokovu wetu.
Kwa hiyo “katika Kristo ulitokea utimilifu halisi wa upatanisho wetu, nasi
tulipewa ukamilifu wa ibada kwa Mungu”[11].
Tendo hilo la ukombozi wa wanadamu
na la kutukuzwa kwake kamili, lenye utangulizi wake katika miujiza iliyotendeka
kwa taifa la Agano la Kale, lilitimizwa na Bwana Yesu hasa kwa njia ya fumbo la
Pasaka ya mateso yake yenye heri, ufufuko wake kutoka kuzimu, na kupaa kwake
mbinguni kwa utukufu; fumbo ambalo kwa ajili yake “kwa kufa aliangamiza mauti
na alipofufuka akaturudishia uzima”[12].
Maana, kutoka ubavuni mwa Kristo akilala msalabani ilitoka sakramenti ya ajabu
ya Kanisa lote[13].
Tendo la wokovu linaloendelezwa na
Kanisa hutimizwa katika Liturujia
6. Kama vile Kristo alivyotumwa na
Baba, kadhalika naye aliwatuma Mitume, waliojaa Roho Mtakatifu.Alifanya hivyo
sio tu ili watangaze, kwa kuhubiri Injili kwa kila kiumbe[14],
kwamba Mwana wa Mungu, kwa kifo na ufufuko wake, ametuokoa kutoka mamlaka ya
shetani[15]na
ya mauti na kutuleta katika ufalme wa Baba yake; bali, pia alitaka kazi hiyo ya
ukombozi, ambayo walikuwa wakiitangaza, waitekeleze kwa njia ya Sadaka na
Sakramenti, ambazo ni kiini cha maisha ya kiliturujia. Hivyo, kwa njia ya
Ubatizo, wanadamu wanaingizwa katika fumbo la Pasaka ya Kristo: wanakufa pamoja
naye, wanazikwa na kufufuka pamoja naye[16],
wanapokea roho ya kufanywa wana “ambayo kwa hiyo twalia: Aba, yaani Baba” (Rum
8:15); na hivyo wanapata kuwa wale waabuduo halisi ambao Baba awatafuta[17].
Kadhalika, kila wailapo karamu ya Bwana, waitangaza kifo cha Bwana hata ajapo[18].
Kwa hiyo, siku ileile ya Pentekoste, ambapo Kanisa lilidhihirishwa ulimwenguni,
“wale waliolipokea neno” la Petro “wakabatizwa”. Nao “wakawa wakidumu katika
fundisho la Mitume, na katika ushirika, na katika kuumega mkate, na katika
kusali ... wakimsifu Mungu kwa pamoja, na kuwapendeza watu wote” (Mdo
2:41-42.47 Vulg.). Tokea hapo, Kanisa halijaacha kamwe kujumuika pamoja
ili kuliadhimisha fumbo la Pasaka: kwa kuyasoma yote “katika Maandiko
yanayomhusu Yeye [Kristo]” (Lk 24:27), kwa adhimisho la Ekaristi, ambapo
“vimefanyika wazi tena mafanikio na ushindi mkuu wa kifo chake”[19],
na kwa kumshukuru “Mungu kwa sababu ya kipawa chake tusichoweza kukisifu kama
ipasavyo” (2Kor 9:15), katika Yesu Kristo, “kwa sifa ya utukufu wake” (Efe
1:12), kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.
Uwepo wa Kristo katika Liturujia
7. Kusudi kutimiza tendo kubwa namna
hii, Kristo yupo daima katika Kanisa lake, kwa jinsi ya pekee katika
maadhimisho ya kiliturujia. Yupo kwenye Sadaka ya Misa katika nafsi ya kasisi,
“Yeye ambaye, akijitoa mara moja msalabani, anajitoa tena mwenyewe kwa huduma
ya mapadre”[20].
Yupo hasa chini ya maumbo ya Ekaristi. Yupo kwa nguvu yake katika sakramenti,
ili kwamba mtu anapobatiza, ni Kristo mwenyewe anayebatiza[21].
Yupo katika Neno lake, kwa kuwa ni Yeye anayesema wakati Maandiko Matakatifu
yanaposomwa katika Kanisa. Yupo, tena, wakati Kanisa linaposali (supplicat)
na kuimba zaburi (psallit), kwa vile aliahidi: “Walipo wawili watatu
wamekusanyika kwa jina langu nami nipo papo hapo katikati yao” (Mt 18:20).
Kwa kweli, katika tendo kubwa namna
hii, ambalo kwa njia yake Mungu hutukuzwa kikamilifu na wanadamu
wanatakatifuzwa, Kristo daima hulishirikisha Kanisa; naye Kanisa ni Bibiarusi
yake mpendwa sana, ambaye anamwomba Bwana wake na kwa njia yake anamwabudu Baba
wa milele.
Kumbe, kwa haki Liturujia hutazamwa
kama utekelezaji wa kazi ya kikuhani ya Yesu Kristo. Katika Liturujia, kwa
ishara zinazoonekana, huo-nyeshwa na kutendeka kutakatifuzwa kwake binadamu,
kila ishara ikiwa na maana ya pekee. Katika Liturujia, ibada halisi za hadhara
huadhimishwa na Mwili wa fumbo wa Yesu Kristo, yaani na Kichwa na viungo vyake.
Kwa hiyo kila adhimisho la kiliturujia,
kwa kuwa ni tendo la Yesu Kristo Kuhani na la Mwili wake, ndilo Kanisa, ni
tendo takatifu kupita yote na hakuna tendo jingine la Kanisa linalofanana nalo
kwa manufaa kwa kiwango kilekile na kwa daraja ileile.
Liturujia ya duniani na ile ya
mbinguni
8. Katika Liturujia ya hapa duniani
sisi tunashiriki, tukiionja, Liturujia ya mbinguni, iadhimishwayo katika Mji
Mtakatifu wa Yerusalemu, tunaouelekea kama wasafiri, ambako Kristo ameketi
mkono wa kuume wa Mungu kama mhudumu wa patakatifu na wa ile hema ya kweli[22].
Tunaungana na wapiganaji wa jeshi la mbinguni kumwimbia Bwana wimbo wa utukufu.
Tukiwakumbuka kwa heshima watakatifu, twatumaini kupata ushirika nao;
twamngojea kwa shauku Mkombozi, Bwana wetu Yesu Kristo, mpaka
atakapojidhihirisha, Yeye aliye uzima wetu, ndipo na sisi tutakapodhihirishwa
pamoja naye katika utukufu[23].
Liturujia takatifu haimalizi
utendaji wote wa Kanisa
9. Liturujia takatifu haimalizi
utendaji wote wa Kanisa. Maana, kabla wanadamu hawajaikaribia Liturujia, yabidi
waalikwe kwenye imani na toba: “Wamwiteje yeye wasiyemwamini? Tena wamwaminije
yeye wasiyemsikia? Tena wamsikieje pasipo mhubiri? Tena wahubirije
wasipopelekwa?” (Rum 10:14-15).
Kwa hiyo Kanisa laihubiri
habari njema ya wokovu kwa wale wasioamini, kusudi watu wote wamjue Mungu wa
pekee wa kweli, na Yesu Kristo aliyemtuma, na pia, wakitubu, waongoke kutoka
njia zao[24].
Aidha, Kanisa lazima lihubiri daima imani na toba kwa waamini; lazima pia
liwatayarishe kwa Masakramenti, liwafundishe kuyashika yote yaliyoamriwa na
Kristo[25],
na pia liwahimize kwenye matendo yote ya mapendo, ya ibada na ya utume, ambayo
huonyesha ya kuwa waamini wa Kristo si wa ulimwengu huu, lakini wao ni nuru ya
ulimwengu na lazima wamtukuze Baba mbele ya watu.
Liturujia ni kilele na chemchemi ya
maisha ya Kanisa
10. Hata hivyo Liturujia ni kilele
ambapo kazi ya Kanisa inaelekea, na papo hapo ni chemchemi zinamotoka nguvu
zake zote. Maana, bidii zote za kazi za kitume hukusudiwa ili wote, waliofanywa
watoto wa Mungu kwa njia ya imani na Ubatizo, wakusanyike pamoja, wamtukuze
Mungu katika Kanisa, washiriki sadaka na kuila karamu ya Bwana.
Kwa upande wake, Liturujia
huwasukuma waamini, waliolishwa kwa “sakramenti za kipasaka”, kuishi katika
“umoja wa utakatifu”[26].
Tena huwaombea “waonyeshe katika maisha yao yale waliyopewa katika imani”[27].
Aidha, kufanyika upya kwa agano la Bwana na wanadamu katika Ekaristi kuwavuta
na kuwasha ndani ya waamini upendo wenye bidii wa Kristo. Kwa hiyo kutokana na
Liturujia, hasa Ekaristi, humiminwa ndani yetu neema, kama toka chemchemi, na
pia hupatikana kikamilifu lengo la utendaji wote wa Kanisa ambalo ni utakatifu
ule wa wanadamu na tukuzo la Mungu, katika Kristo.
Umuhimu na maelekeo ya kila mtu
katika Liturujia
11. Lakini, ili kufikia lengo hilo
kamili, sharti waamini washiriki Liturujia takatifu kwa maelekeo ya moyo
mnyofu, walinganishe akili zao na sauti, wafanye kazi pamoja na neema ya Mungu
ili wasiipokee bure[28].
Kwa hiyo wachungaji watukufu wanapaswa kuangalia kuwa katika tendo la Liturujia
zishikwe sheria zifanyazo maadhimisho yawe thabiti na halali. Wachungaji pia
lazima wahakikishe kuwa waamini wanaelewa kinachofanyika na wanashiriki
kikamilifu na kufaidi matunda ya maadhimisho hayo.
Liturujia na sala ya binafsi
12. Lakini maisha ya kiroho
hayaishii katika kuishiriki Liturujia takatifu tu. Maana mkristo, anayealikwa
kushiriki sala ya pamoja, anapaswa pia aingie chumbani mwake kumwomba Baba
katika siri[29].
Aidha, kadiri ya mafundisho ya Mtume anapaswa kusali bila kukoma[30].
Naye Mtume mwenyewe hutufundisha kuchukua sikuzote katika mwili wetu mateso
yake Yesu, ili uzima wa Yesu nao hudhihirishwe katika mwili wetu wenye kufa[31].
Kwa sababu hiyo katika sadaka ya Misa twamwomba Bwana kwamba “anapopokea sadaka
ya dhabihu ya kiroho” atufanye sisi wenyewe kuwa kwake “sadaka ya milele”[32].
Ibada mbalimbali za wakristo
zielekee kwenye Liturujia
13. Ibada mbalimbali za watu
wakristo, mradi zilingane na kanuni na taratibu za Kanisa, zinahimizwa sana,
hasa zinapofanyika kwa agizo la Kiti cha Kitume.
Ibada mbalimbali za Makanisa maalum
(particularium) zina hadhi ya pekee, hasa zinapofanyika kwa agizo la
Maaskofu, kadiri ya desturi au vitabu vilivyoidhinishwa kihalali.
Ibada hizo, lakini, sharti zipangwe
kwa kulingana vipindi vya mwaka wa kiliturujia, zilingane na Liturujia
takatifu, zitokane nayo kwa namna fulani, na kuwaelekeza watu kwenye Liturujia
yenyewe, kwa sababu, kwa tabia yake, Liturujia ina hadhi ya juu zaidi kuliko
ibada za watu.
II - UMUHIMU WA KUHIMIZA MALEZI YA
KILITURUJIA NA KUSHIRIKI HAI KWA WAAMINI
14. Mama Kanisa anatamani sana
waamini wote waongozwe kwenye kuyashiriki maadhimisho ya kiliturujia kwa
utimilifu, kwa ufahamu na utendaji. Jambo hili linadaiwa na tabia ya Liturujia
yenyewe na pia – kwa sababu ya Ubatizo [wao], ni haki na wajibu wa watu
wakristo, ambao ni “mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa
milki wa Mungu” (1Pet 2:9; taz. 2:4-5).
Katika kurekebisha na kukuza
Liturujia lazima kujali kwa namna ya pekee kushiriki huko kwa utimilifu na
utendaji kwa waamini wote: maana [Liturujia] ni chemchemi ya kwanza na ya
lazima ambayo toka kwake waamini wanaweza kuchota roho kweli ya kikristo. Kwa
hiyo wachungaji wa roho, katika kazi zao zote za kitume, wanapaswa
kuishughulikia bila kukoma kwa njia ya mafundisho yafaayo.
Lakini haiwezekani kutumaini
kuyatimiza hayo, kama wachungaji wenyewe hawajawa na roho na nguvu ya
Liturujia, na kabla hawajajielimisha ili wawaelimishe na wengine. Kwa hiyo ni
muhimu kabisa, awali ya yote, makleri wapate mafundisho juu ya Liturujia. Kwa
sababu hiyo Mtaguso Mkuu unaagiza yafuatayo.
Malezi ya maprofesa wa Liturujia
15. Walimu wanaochaguliwa kufundisha
Liturujia katika seminari, katika vituo vya malezi ya kitawa, na katika vyuo
vya elimu ya Teolojia, ni lazima wapate elimu inayoifaa kazi yao katika vyuo
vinavyofundisha haya kwa namna ya pekee.
Ufundishaji wa Liturujia
16. Liturujia takatifu katika
seminari na nyumba za malezi ya kitawa, lazima ihesabiwe kati ya masomo ya lazima
na ya muhimu zaidi. Aidha, katika vyuo vya Teolojia ihesabiwe kati ya masomo ya
maana zaidi, na ifundishwe kadiri ya muono wa kiteolojia, wa kihistoria, wa
kiroho, wa kichungaji na wa kisheria. Aidha, walimu wa masomo mengine, hasa
walimu wa Dogma, Maandiko Matakatifu, Teolojia ya maisha ya kiroho na ya
kichungaji, wajitahidi kusisitiza, kila mmoja kadiri ya matakwa ya masomo yake,
fumbo la Kristo na historia ya wokovu ili uonekane wazi uhusiano wake na
Liturujia, na jinsi masomo hayo yanavyohusiana katika malezi ya kipadre.
Malezi ya waseminari kuhusu
Liturujia
17. Waseminari wakubwa, katika
seminari na katika nyumba za kitawa, waelimishwe juu ya Liturujia katika maisha
ya kiroho; yaani waingizwe polepole ili waweze kuelewa maana ya madhehebu
takatifu na kushiriki kwa moyo wote, na pia wapate kuadhimisha mafumbo
matakatifu na ibada nyingine zenye roho ya kiliturujia. Pia wajifunze kuzishika
sheria za kiliturujia, ili maisha katika seminari na katika nyumba za malezi za
kitawa zitawaliwe na roho ya kiliturujia.
Kuwasaidia mapadre mintarafu
Liturujia
18. Mapadre, wanajimbo na pia
watawa, wanaofanya kazi tayari katika shamba la mzabibu la Bwana, wasaidiwe kwa
kila namna ifaayo ili waelewe zaidi na zaidi yale watendayo katika ibada
takatifu, tena wasaidiwe kuishi maisha ya kiliturujia na kuwashirikisha waamini
waliokabidhiwa.
Kuwaelimisha waamini juu ya
Liturujia
19. Wachungaji wa roho wajitahidi,
kwa bidii na saburi, ili waamini waelimishwe juu ya Liturujia na pia waweze
kuishiriki kikamilifu, katika mwili na katika roho, kulingana na umri wao, hali
yao, aina ya maisha yao na elimu yao ya kidini. Kwa njia hii wachungaji hawa
watatimiza moja ya majukumu yao ya kwanza, yaani kuwa wagawaji waaminifu wa
mafumbo ya Mungu. Aidha, waliongoze kundi lao katika mambo hayo, si kwa maneno
tu, bali pia kwa mifano.
Vyombo vya upashanaji habari na
Liturujia
20. Kama zinatumiwa redio na
televisheni kutangaza ibada takatifu, hasa Misa, matumizi ya vyombo hivyo yawe
ya heshima na utaratibu, chini ya uongozi na udhamini wa mtu mwenye ujuzi,
ambaye ameteuliwa na Maaskofu kwa kazi hiyo.
III - MAREKEBISHO YA LITURUJIA
TAKATIFU
21. Mama Kanisa anatamani kufanya
kwa uangalifu marekebisho ya Liturujia yenyewe, ili kuhakikisha kuwa wakristo
wanapata wingi wa neema katika Liturujia takatifu. Katika Liturujia ipo sehemu
isiyobadilika, kwa sababu imewekwa na Mungu; na pia zipo sehemu zinazoweza
kubadilika, nazo ni zile ambazo, kufuatana na mwenendo wa nyakati, zinaweza au
pia zinapaswa kubadilika, endapo ndani yake yameingia mambo yasiyolingana na
maumbile halisi ya Liturujia yenyewe, au inapoonekana kutofaa tena.
Katika marekebisho hayo, inabidi
kuratibu matini na madhehebu za ibada ili zionyeshe kinaganaga zaidi mambo
matakatifu zinayoisharisha, nao wakristo waweze kuyaelewa kwa urahisi
iwezekanavyo na kuyashiriki kikamilifu, kwa bidii na kama jumuiya.
Kwa sababu hiyo, Mtaguso Mkuu
unaweka kanuni za jumla zifuatazo.
A) Kanuni za jumla
Kuratibu Liturujia ni juu ya
Hierarkia
22. § 1. Kuratibu Liturujia takatifu
ni juu ya mamlaka ya Kanisa tu, ambayo ipo katika Kiti Kitakatifu na, kadiri ya
sheria, kwa Maaskofu.
§ 2. Kwa uwezo unaotokana na sheria,
kuratibu Liturujia, kadiri ya mipaka iliyokubaliwa, ni juu ya Mabaraza
mbalimbali ya Maaskofu ya nchi fulani yaliyoundwa kwa mujibu wa sheria
kusimamia nchi hizo.
§ 3. Kwa hiyo, mtu mwingine yeyote
yule, hata akiwa padre, hawezi kuongeza, kuondoa au kubadili jambo lolote kwa
uamuzi wake mintarafu Liturujia.
Mapokeo na maendeleo
23. Ili kuyahifadhi mapokeo mema, na
hapohapo lakini kufanyiza maendeleo ya halali yasitawi, marekebisho ya kila
sehemu ya Liturujia lazima yatanguliwe na uchunguzi wa kina wa kiteolojia, wa
kihistoria na wa kichungaji. Aidha, marekebisho hayo yazijali kanuni za jumla
zinazohusu muundo na roho ya Liturujia. Tena yajali mang’amuzi yatokanayo na
marekebisho ya Liturujia ya hivi karibuni na ruhusa (indultis)
zilizokubaliwa mahali mbalimbali. Mwishowe, mabadiliko yasifanywe isipokuwa
inapodaiwa na manufaa ya kweli ya Kanisa, kwa uangalifu ili mambo mapya
yatokane kwa mpangilio na yale yaliyopo.
Pia, kadiri iwezekanavyo, kusiwe na
tofauti kubwa kati ya ibada katika nchi zilizo jirani.
Biblia na Liturujia
24. Jambo muhimu kuliko yote katika
adhimisho la Liturujia ni Maandiko Matakatifu, maana katika hayo huchukuliwa
masomo ya kusomwa na kufafanuliwa katika mahubiri, na pia zaburi zinazoimbwa.
Sala, maombi na nyimbo hupata uvuvio toka Maandiko, kama vile toka Maandiko
matendo na ishara hupata maana. Kwa hiyo, ili kufaulu kufanya marekebisho na
maendeleo na malinganisho ya Liturujia, ni lazima kuhimiza ule upendo mtamu na
hai wa Maandiko Matakatifu, ambao unashuhudiwa na mapokeo mastahiki ya Makanisa
ya Mashariki na ya Magharibi.
Marekebisho ya vitabu vya Liturujia
25. Vitabu vya kiliturujia
virekebishwe upesi iwezekanavyo; kazi hiyo ifanywe na watu wenye ujuzi, na
maoni ya Maaskofu wa nchi mbalimbali yasikilizwe.
B) Kanuni zitokanazo na tabia ya kidaraja na ya kijumuiya ya
Liturujia
26. Matendo ya kiliturujia si
matendo ya kila mmoja peke yake, bali ni maadhimisho ya Kanisa, ambalo ni
“sakramenti ya umoja”, yaani taifa takatifu linalokusanywa na kuratibishwa
chini ya uongozi wa Maaskofu[33].
Kwa sababu hiyo matendo hayo ni ya
mwili wote kabisa wa Kanisa, nayo huudhihirisha na kuuimarisha. Aidha, kila
mmoja wa wanakanisa anahusika kwa namna tofauti, kadiri ya utofauti wa daraja,
wa majukumu, na wa ushiriki kiutendaji
Ubora wa adhimisho la pamoja
27. Kila mara ibada, kulingana na
maumbile ya kila moja, zinapodai adhimisho la pamoja kwa mahudhurio ya waamini
wanaoshiriki kimatendo, ihimizwe kwamba adhimisho hilo ni la kupendelewa zaidi,
kadiri inavyowezekana, kuliko adhimisho la mtu peke yake, kana kwamba lingekuwa
ibada ya binafsi.
Hayo yanahusu hasa adhimisho la Misa
– hata kama kila Misa ni daima tendo la hadhara na la kijumuiya – na pia
maadhimisho ya sakramenti.
Nafasi ya kila mmoja katika
adhimisho la Liturujia
28. Katika maadhimisho ya liturujia
kila mmoja, mhudumu au mwamini, aliye na kazi ya kufanya, atekeleze yote na
sehemu zile tu zinazohusu wajibu wake, kulingana na maumbile ya ibada na kanuni
za Liturujia.
29. Pia watumishi wa altare,
wasomaji, wenye kueleza ibada na wanakwaya wote, wanatekeleza huduma kweli ya
kiliturujia. Kwa hiyo inawapasa watekeleze kazi yao kwa ule uchaji wa kweli na
adabu inayofaa huduma muhimu namna hii, na ambayo taifa la Mungu kwa haki
linadai kwao.
Hivyo inabidi wajawe kwa makini na
roho ya kiliturujia, kila mmoja kadiri ya hali yake; na pia wafundishwe kutenda
yote kufuatana na kanuni za utaratibu zilizowekwa.
Kushiriki kikamilifu kwa waamini
30. Ili kuwawezesha waamini
washiriki kimatendo, mashangilio ya waamini, maitikio, kuimba zaburi, antifona,
nyimbo, vitendo, ishara na mkao wa mwili vitiliwe maanani. Unyamavu mtakatifu
utumike pia, wakati unapodaiwa.
31. Katika marekebisho ya vitabu vya
kiliturujia, iangaliwe kwa makini kwamba maelekezo (rubricae)
yanayowahusu waamini pia yawekwe wazi kabisa.
Liturujia na usawa wa waamini
32. Katika Liturujia usiwepo
upendeleo wowote kwa watu binafsi ama cheo, iwe katika maadhimisho au katika
fahari ya nje, isipokuwa kwa cheo kitokanacho na kazi ya kiliturujia na Daraja
takatifu; au pia heshima zinazowapasa viongozi wa serikali kwa kadiri ya sheria
za kiliturujia.
C) Kanuni zitokanazo na tabia ya kiliturujia ya kuelimisha
na kuwalea waamini
33. Ingawa Liturujia takatifu ni
hasa ibada kwa Mungu Mkuu, yamo pia ndani yake mafundisho tele kwa waamini[34].
Maana katika Liturujia Mungu anaongea na watu wake; naye Kristo anaendelea
kuhubiri Injili. Waamini kwa upande wao wanamwitikia Mungu kwa nyimbo na sala.
Sala zinazoinuliwa kwa Mungu na
padre, aongozaye ibada katika nafsi ya Kristo, zinasemwa kwa niaba ya taifa
zima takatifu na wote waliopo. Na zile ishara zinazoonekana, ambazo Liturujia
huzitumia kwa kuyaashiria yale mambo ya kimungu yasiyoonekana, zilichaguliwa na
Kristo au na Kanisa. Kwa hiyo si yanaposomwa tu “yaliyoandikwa kwa kutufundisha
sisi” (Rum 15:4), lakini pia Kanisa linaposali au kuimba au kutenda, imani ya
wale wanaoshiriki inalishwa, akili zao zinainuliwa kwa Mungu, ili kumtolea heshima
ipasayo na kupokea kwa wingi zaidi neema yake.
Kwa hiyo, katika kufanya marekebisho
ya Liturujia kanuni za jumla zifuatazo hazina budi kuzingatiwa.
Ukamilifu na kueleweka kwa ibada
34. Ibada zing’ae kwa heshima na
urahisi, ziwe fupi, wazi na bila marudio ya bure. Zilingane na uwezo wa ufahamu
wa waamini, bila kuhitaji, kwa kawaida, maelezo mengi.
Biblia, homilia na katekesi kuhusu
Liturujia
35. Ili ionekane wazi kwamba
katika Liturujia matendo ya ibada na Neno vimeunganika kiundani:
1) Katika ibada takatifu,
masomo ya Maandiko Matakatifu yapangwe kwa wingi zaidi, kutoka sehemu
mbalimbali na kwa jinsi inayofaa zaidi.
2) Wakati ufaao zaidi kwa
mahubiri, kama sehemu ya adhimisho la Liturujia, kwa kadiri ya ibada yenyewe
inavyoruhusu, uwekwe na kutajwa pia katika rubrika (maelekezo). Huduma ya
kuhubiri itimizwe kwa uaminifu kamili na jinsi ifaavyo. Aidha, mahubiri
yachotwe hasa kutoka chemchemi ya Maandiko Matakatifu na ya Liturujia, kwani ni
tangazo la matendo makuu ya Mungu katika historia ya wokovu, iliyo fumbo la
Kristo, fumbo ambalo daima lipo na linatenda kazi ndani yetu, hasa katika
maadhimisho ya kiliturujia.
3) Mafundisho kuhusu
Liturujia yenyewe yatolewe kwa njia mbalimbali. Katika ibada zenyewe yatolewe
maelezo mafupi, ikiwa ni lazima. Hayo yafanywe kwa maneno yaliyotayarishwa au
kwa mengine yanayofanana nayo, na padre au mhudumu mwenye uwezo. Lakini hayo
yote yafanywe tu katika nafasi zifaazo zaidi.
4) Ibada ya Neno la Mungu ihimizwe,
hasa katika makesha ya sherehe, au siku za Majilio na Kwaresima, siku za
Dominika na sikukuu, hasa pale asipokuwepo padre. Ikiwa ni hivyo, ibada
iongozwe na shemasi au mtu mwingine aliyeruhusiwa na Askofu.
Lugha ya Liturujia
36. § 1. Matumizi ya lugha ya
kilatini yahifadhiwe katika madhehebu za ibada za kilatini, licha ya sheria za
pekee zikiwemo.
§ 2. Lakini, mara nyingi
zaidi itumike lugha ya nchi kwani yaweza kuwafaa sana waamini, iwe katika Misa,
katika kuadhimisha Sakramenti, na pia katika sehemu nyingine za Liturujia.
Katika masomo na maelekezo, katika baadhi ya sala na nyimbo, lugha ya nchi
ipate nafasi zaidi. Kanuni zinazohusu jambo hili zimetolewa peke yake katika
sura zifuatazo.
§ 3. Kadiri ya kanuni hizo,
kutoa uamuzi mintarafu matumizi ya lugha ya nchi ni juu ya mamlaka ya kikanisa
husika ya kila nchi, kama ilivyoandikwa katika ibara 22 § 2. Na ikiwa inafaa,
maoni ya Maaskofu wa nchi jirani zinazotumia lugha hiyo yasikilizwe. Maamuzi
hayo lazima yapate kibali, yaani idhini, cha Kiti cha Kitume.
§ 4. Tafsiri ya vitabu vya Liturujia
vya kilatini lazima ikubaliwe na mamlaka ya kikanisa husika ya nchi ile, kama
yalivyotajwa hapo juu.
D) Kanuni za marekebisho ya Liturujia kulingana na hali za
watu na mapokeo yao
37. Kanisa, katika yale
yasiyogusa imani au manufaa ya jumuiya nzima ya waamini, halipendi kuwabana
wote kwa mtindo moja, wala katika Liturujia. Kanisa huheshimu na kuhimiza
vipawa na tunu za mila za kila taifa na jamii. Katika tamaduni za mataifa, yale
ambayo hayafungamani kabisa na ushirikina au makosa, Kanisa huyachunguza kwa
wema na pia, kama inawezekana, huyahifadhi yalivyo. Na mara nyingine huyaingiza
hata katika Liturujia yenyewe, iwapo tu yanalingana na roho ya kweli na halisi
ya kiliturujia.
38. Pasipo kuvunja umoja wa
Riti ya Kiroma, katika marekebisho ya vitabu vya Liturujia, iachwe nafasi kwa
ajili ya tofauti zilizo halali na kwa marekebisho yanayoweza kufanywa na jamii,
nchi na mataifa mbalimbali, hasa katika nchi za misioni. Hayo yatiliwe maanani
katika mipangilio ya ibada na katika kuandaa maelekezo (rubricis) ya
jinsi ibada zinavyofanyika.
39. Kadiri ya maagizo yaliyomo
katika matoleo halisi (editionibus typicis) ya vitabu vya kiliturujia,
mamlaka ya kufanya marekebisho ni juu ya Mabaraza ya Maaskofu ya kila mahali,
kama ilivyoelezwa katika ibara 22 § 2; marekebisho hayo yahusu hasa utoaji wa
Sakramenti, visakramenti, maandamano, lugha na muziki na sanaa za kiliturujia
kadiri ya kanuni za msingi zilizomo katika hati hii.
Jinsi ya kufanya marekebisho ya
Liturujia
40. Kwa kuwa katika nchi
mbalimbali marekebisho ya kina ya Liturujia yanatakiwa upesi, nayo yanaleta
ugumu zaidi, basi, kwa sababu hiyo:
1) Mabaraza ya Maaskofu ya
kila mahali, kama ilivyoelezwa katika ibara 22 § 2, yachunguze kwa makini na
busara mambo yaliyomo katika mila na desturi ya kila jamii ambayo yanaweza
kuingizwa, kwa namna ifaayo, katika ibada kwa Mungu. Hatimaye, marekebisho
yanayodhaniwa kuwa ni ya kufaa au ya lazima, yapelekwe kwa Baba Mtakatifu
kusudi yaingizwe kwa idhini yake.
2) Kusudi marekebisho hayo yafanyike
kwa tahadhari inayotakiwa, Baba Mtakatifu atatoa idhini kwa Mabaraza ya
Maaskofu ili yaruhusu na kuongoza, ikiwa inafaa, majaribio ya kwanza yatakiwayo
katika vikundi vilivyoandaliwa kwa kusudi hilo na kwa muda wa kupangwa.
3) Kwa vile sheria za kiliturujia
mara nyingi huleta matatizo mintarafu marekebisho, hasa katika misioni, ni
lazima wataalamu wahusishwe katika kuzitunga sheria hizo.
IV - KUKUZA MAISHA YA KILITURUJIA
JIMBONI NA PAROKIANI
41. Askofu lazima atazamwe
kama kuhani mkuu wa kundi lake na ambaye maisha ya waamini wake katika Kristo
kwa namna fulani yanatoka kwake na yanamtegemea.
Kwa hiyo ni lazima waamini wote
wakaze sana umuhimu wa maisha ya kiliturujia ya jimbo pamoja na Askofu, hasa
katika kanisa katedrali (cathedrali): wote waelewe kwamba Kanisa
ladhihirika hasa katika ushirikiano kamili na wa kimatendo wa taifa lote
takatifu la Mungu katika maadhimisho yaleyale ya kiliturujia, hasa katika
Ekaristi ileile moja, sala ileile na altare ileile anapoongoza Askofu pamoja na
mapadre wake na watumishi[35].
Maisha ya kiliturujia katika parokia
42. Maadam Askofu hawezi
mwenyewe kuongoza daima na popote kundi lake zima katika Kanisa lake, basi
Askofu hana budi kuwagawanya waamini katika makundi mbalimbali, na kati ya hayo
yana umuhimu wa maana sana maparokia yanayoundwa kila mahali chini ya uongozi
wa mchungaji amwakilishaye Askofu; maana, hayo yanawakilisha kwa namna fulani
Kanisa lionekanalo ambalo limewekwa katika dunia nzima.
Kwa hiyo maisha ya kiliturujia ya
parokia na uhusiano wake na Askofu lazima visitawishwe katika roho na matendo
ya waamini na wakleri; pia lazima kufanya jitihada ili hisia ya jumuiya katika
parokia ichanue hasa katika kuadhimisha pamoja Misa ya Dominika.
V - KUKUZA KAZI YA KICHUNGAJI
MINTARAFU LITURUJIA
43. Hamasa ya kukuza na
kurekebisha Liturujia inatazamwa kwa haki kama ishara ya Maongozi ya Mungu
katika nyakati zetu, na pia kama mpito wa Roho Mtakatifu katika Kanisa lake;
tena inapiga chapa mahsusi kwa maisha ya Kanisa na pia kwa mwelekeo mzima wa
dini kimawazo na kimatendo kwa wakati huu.
Kwa sababu hiyo, kwa lengo la
kuongeza zaidi na zaidi katika Kanisa kazi hiyo ya kichungaji mintarafu
Liturujia, Mtaguso Mkuu unaamua yafuatayo:
Kamati ya Liturujia kitaifa
44. Yafaa Mabaraza ya Maaskofu ya
kila mahali, kama ilivyoelezwa katika ibara 22 § 2, yaunde kamati ya Liturujia
ambayo itafanya kazi ikisaidiwa na wataalamu wa Liturujia, muziki, sanaa
takatifu pamoja na uchungaji. Kama inawezekana, kamati hiyo isaidiwe na aina ya
taasisi ya kichungaji ya Liturujia yenye wataalamu katika uwanja huo, bila
kuwatenga walei pale inapotakiwa. Itakuwa ni wajibu wa kamati yenyewe, chini ya
uongozi wa Mabaraza ya Maaskofu, kama ilivyoelezwa hapo juu, kuratibu kazi ya
kichungaji mintarafu Liturujia katika sehemu yake iliyokabidhiwa, na pia
kuhimiza utafiti na majaribio yanayotakiwa kila panapokuwa na suala la kupeleka
kwa Baba Mtakatifu.
Kamati ya Liturujia ya jimbo
45. Vilevile katika kila
jimbo iundwe kamati ya Liturujia kwa lengo la kuhimiza, chini ya uongozi wa
Askofu, utume wa kiliturujia.
Ikiwa inafaa, majimbo kadhaa yaunde
kamati moja ili kuhimiza Liturujia kwa makubaliano ya pamoja.
Kamati nyinginezo
46. Licha ya kamati ya
Liturujia, kadiri iwezekanavyo, katika kila jimbo iundwe pia kamati ya muziki
na ya sanaa takatifu.
Kamati hizo tatu lazima zishirikiane
katika kazi zao, na, ionekanapo kuwa inafaa, ziunganike na kuunda kamati moja.
Sura ya Pili
FUMBO TAKATIFU LA EKARISTI
Misa na fumbo la Pasaka
47. Mwokozi wetu, katika Karamu ya
mwisho, usiku alipotolewa, aliweka sadaka ya Ekaristi ya Mwili wake na Damu
yake. Alifanya hivyo ili kuendeleza Sadaka ya Msalaba siku zote mpaka
atakaporudi, kusudi amwachie Bibiarusi mpendwa, yaani Kanisa, ukumbusho wa kifo
chake na ufufuko wake: sakramenti ya utakatifu (sacramentum pietatis),
ishara ya umoja, kifungo cha mapendo[36],
karamu ya Pasaka “ambamo Kristo huliwa, na roho hujazwa neema, na hutolewa
amana ya uzima wa milele”[37].
Kushiriki kiutendaji kwa waamini
katika Misa
48. Kwa sababu hiyo, Kanisa
anajibidisha kwa namna nyingi kusudi waamini wasihudhurie fumbo hilo la imani
kama wageni au watazamaji bubu, bali waishiriki ibada takatifu kwa akili, kwa
moyo na kwa matendo, wakielewa vizuri fumbo hilo kwa njia ya matendo ya
kiliturujia na sala. Waamini waelimishwe katika Neno la Mungu; walishwe katika
karamu ya Mwili wa Bwana; wamtolee Mungu shukrani; wakitolea hostia isiyo na
doa, siyo kwa mikono ya padre tu, bali pia pamoja naye, wajifunze kujitolea
wenyewe. Tena, siku kwa siku, kwa njia ya Kristo mshenga, wakamilishwe katika
umoja na Mungu na kati yao[38],
ili hatimaye Mungu awe yote katika wote.
49. Kwa hiyo, ili sadaka ya Misa
ilete manufaa kamili ya kichungaji pia kwa njia ya umbo la ibada, Mtaguso Mkuu
unaagiza yafuatayo kwa ajili ya Misa ziadhimishwazo pamoja na waamini, hasa
Dominika na Sikukuu.
Marekebisho ya kanuni ya Misa
50. Kanuni ya ibada ya Misa
itengenezwe upya ili kiini halisi cha kila sehemu ya ibada na uhusiano kati ya
sehemu mbalimbali vionekane wazi zaidi, na kuwawezesha waamini kushiriki kwa
moyo na kwa matendo.
Kwa sababu hiyo madhehebu za ibada
zirahisishwe, lakini kiini chake kihifadhiwe; yaachwe mambo yale ambayo
yalifanyika maradufu na yale yaliyoongezwa bila umuhimu, kadiri nyakati
zilivyopita; na mengine yaliyoachwa bila haki yaingizwe tena, kadiri ya kanuni
ya kale ya Mababa watakatifu, kadiri itakavyoonekana kufaa au kuwa lazima.
Masomo ya Biblia katika Misa
yaongezeke
51. Ili meza ya Neno la Mungu
iandaliwe kwa wingi zaidi kwa ajili ya waamini, hazina za Biblia zizidi
kufunguliwa, kusudi katika muda wa miaka kadhaa ya kuagizwa waamini wasomewe
sehemu kubwa zaidi ya Maandiko Matakatifu.
Homilia
52. Inatiliwa sana maanani homilia,
kama sehemu ya Liturujia yenyewe; kwani, kwa njia yake, katika mwaka wa
kiliturujia, mafumbo ya imani na miongozo ya maisha ya kikristo vinafafanuliwa
kutoka Maandiko Matakatifu. Katika Misa ziadhimishwazo pamoja na waamini siku
ya Dominika na Sikukuu zilizoamriwa, homilia isiachwe isipokuwa kwa sababu
nzito.
Sala ya waamini
53. “Sala za pamoja” au “sala za
waamini” ziingizwe tena baada ya Injili na homilia, hasa Dominika na Sikukuu
zilizoamriwa, kusudi, kwa ushirikiano na waamini, yatolewe maombi kwa ajili ya
Kanisa takatifu, wale wanaotuongoza, wanaosongwa na mahitaji mbalimbali, kwa
ajili ya watu wote na ukombozi wa ulimwengu mzima[39].
Matumizi ya kilatini na lugha ya
mahali katika Misa
54. Katika Misa
zinazoadhimishwa pamoja na waamini, matumizi ya lugha ya nchi inayohusika
yaruhusiwe kwa jinsi ifaavyo, hasa katika masomo na “sala za waamini”, na pia
katika sehemu ziwahusuzo waamini, kufuatana na mazingira ya kila nchi, kadiri
ya ibara 36 ya hati hii.
Lakini bidii ifanyike ili
waamini waweze kusali na kuimba pamoja sehemu za ibada ya Misa ziwahusuzo wao
pia katika lugha ya kilatini.
Aidha, ikionekana kwamba inafaa
katika nchi nyingine kutumia zaidi lugha ya nchi ile katika Misa, yafuatwe
maagizo yaliyotolewa katika ibara 40 ya hati hii.
Komunyo katika maumbo yote mawili
55. Njia kamilifu zaidi ya
kushiriki Misa inakazwa sana: nayo ni pale waamini wanapopokea Mwili wa Bwana
Yesu, baada ya komunyo ya Padre, kutoka katika sadaka ileile.
Bila kupingana na maagizo ya kidogma
ya Mtaguso Mkuu wa Trento[40],
inaruhusiwa komunyo katika maumbo mawili kwa makleri na watawa, na pia walei,
katika nafasi zinazopangwa na Baba Mtakatifu na kufuatana na maoni ya Askofu,
kama vile wanaopewa Daraja takatifu, katika Misa ya kupewa Daraja; wanaoweka
nadhiri za kitawa, katika Misa ya kuweka nadhiri; na wanaobatizwa (neophytis),
katika Misa ya Ubatizo wao.
Umoja wa Misa
56. Ibada ya Misa ina sehemu mbili,
yaani Liturujia ya Neno na Liturujia ya Ekaristi; hizo zote zimeunganika sana
kati yake kiasi kwamba zinafanya ibada moja tu. Kwa hiyo Mtaguso Mkuu unawasihi
kwa dhati wachungaji wa roho wawaelimishe kwa makini waamini wao, katika
katekesi, ili washiriki Misa nzima, hasa siku ya Dominika na Sikukuu
zilizoamriwa.
Konselebrasio
57. § 1. Misa ya kushirikiana
mapadre wengi pamoja, au ‘Konselebrasio’, ambayo huonyesha vizuri umoja wa
upadre, imebaki mpaka leo katika desturi ya Kanisa la Mashariki na pia la
Magharibi. Kwa sababu hiyo Mtaguso Mkuu umependa kutoa kibali chake kwa
konselebrasio katika nafasi zifuatazo:
1° a) Siku ya Alhamisi Kuu ya
Karamu ya Mwisho, katika Misa ya Krisma na pia katika Misa ya jioni;
b) katika Misa wakati wa
Mitaguso, mikutano ya Maaskofu na Sinodi;
c) katika Misa ya kumbariki
Abate.
2° Aidha, kwa idhini ya Mkuu
wa mahali anayehusika, ambaye tu anaweza kuamua kuhusu kufaa kwa konselebrasio,
[basi idhini inatolewa kwa nafasi hizi]:
a) katika Misa “ya shirikani”
(conventualem) na katika Misa kubwa makanisani, ikiwa manufaa ya waamini
hayahitaji mapadre wote waliopo waadhimishe Misa kila mmoja peke yake;
b) katika Misa wakati wa
mikutano mbalimbali ya Mapadre wa jimbo na pia wa mashirika.
§ 2. 1° Ni juu ya Askofu
kupanga utaratibu wa konselebrasio katika jimbo.
2° Lakini kila padre anaweza
kuadhimisha Misa bila mapadre wengine, ila si wakati uleule na mahali palepale
[konselebrasio inapofanyika]; wala Alhamisi Kuu.
58. Ibada mpya ya konselebrasio
itungwe na kuingizwa katika Pontifikale na katika Misale ya Kiroma.
Sura
ya Tatu
SAKRAMENTI
NYINGINE NA VISAKRAMENTI
Maana ya Sakramenti
59. Sakramenti zimewekwa ili
kuwatakatifuza wanadamu, kuujenga Mwili wa Kristo, na mwishowe kumtolea Mungu
ibada. Kwa kuwa ni ishara zinazowafundisha waamini, kwa upande moja zinadai
imani, na kwa upande mwingine zinalisha imani yenyewe kwa maneno na matendo ya
ibada; tena zinaimarisha na kuidhihirisha imani hiyo. Ndiyo sababu zinaitwa
“Sakramenti za imani”. Ni kweli kwamba zinawapatia waamini neema, lakini pia
maadhimisho yake yanawaandaa kikamilifu ili neema yenyewe wanayoipokea itoe
matunda; pia yawawezeshe kumheshimu Mungu jinsi ipasavyo na kufanya matendo ya
huruma.
Kwa sababu hiyo ni muhimu
sana waamini wazielewe kwa urahisi ishara za Sakramenti, nao wazikaribie kwa
makini sana Sakramenti zile zilizowekwa ili kuyalisha maisha ya kikristo.
Visakramenti
60. Mama Kanisa takatifu
aliweka pia visakramenti, ambavyo ni alama takatifu ambazo kwazo, kutokana na
kufanana kwa namna fulani na Sakramenti, vinaashiria matunda, hasa ya kiroho,
ambayo hupatikana kwa maombi ya Kanisa. Kwa njia ya visakramenti hivi watu
hutayarishwa kupokea tunda la msingi la Sakramenti, na mazingira mbalimbali ya
maisha hutakaswa.
61. Hivyo liturujia ya Sakramenti na
Visakramenti inawawezesha waamini wenye moyo mnyofu kuyatakatifuza matukio
karibu yote ya maisha kwa njia ya ile neema ya kimungu inayobubujika toka fumbo
la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Kutokana na fumbo hilo
Sakramenti na Visakramenti hupata nguvu yao; na kwa msaada wa nguvu hiyo
matumizi manyofu ya mambo ya kidunia yaweza kuelekezwa katika kumtakatifuza
binadamu na kumsifu Mungu.
Umuhimu wa marekebisho ya adhimisho
ya Sakramenti
62. Katika mwenendo wa nyakati
katika ibada ya Sakramenti na Visakramenti yameingizwa mambo kadhaa yaletayo
ugumu katika kuelewa maumbile na lengo la ibada hizo. Kwa hiyo marekebisho, ili
kulinganisha ibada na matakwa ya siku hizi, ni ya lazima. Kwa kusudi hilo
Mtaguso unaagiza yafuatayo.
Lugha katika ibada
63. Mara nyingi katika kutoa
Sakramenti na Visakramenti, kwa manufaa ya waamini, lugha ya nchi husika
inaweza kutumiwa katika nafasi kubwa zaidi kadiri ya mwongozo ufuatao:
a) Katika utoaji wa
Sakramenti na Visakramenti inawezekana kutumia lugha ya nchi husika kufuatana
na ibara 36.
b) Kufuatana na toleo jipya
la Rituale ya Kiroma, Mabaraza ya Maaskofu ya kila mahali, kama ilivyoelezwa
katika ibara 22 § 2 ya hati hii, yatayarishe upesi iwezekanavyo Rituale faridi
zinazolinganishwa na mahitaji ya kila nchi, pia kuhusu lugha; kisha Rituale
hizo zitatumika katika nchi zinazohusika baada ya kuchunguzwa na Kiti cha
Kitume. Katika kutunga Rituale hizo, au mikusanyo maalum mingine ya ibada,
yasiachwe maelezo yaliyomo kabla ya kila madhehebu katika Rituale ya Kiroma,
yale yenye tabia ya kichungaji au ya maelekezo (rubricis), na yale yenye
umuhimu wa pekee wa kijamii pia.
Ukatekumeni
64. Uwekwe tena ukatekumeni kwa watu
wazima, uliogawanywa katika hatua nyingi, wa kutekeleza kadiri ya mwongozo wa
Mkuu wa mahali. Hivyo, muda wa ukatekumeni, uliowekwa kwa ajili ya mafundisho
yafaayo, uweze kutakatifuzwa kwa njia ya ibada takatifu zitakazoadhimishwa kwa
nyakati mbalimbali.
Marekebisho ya adhimisho la Ubatizo
65. Katika nchi za misioni
iruhusiwe kuyapokea, sambamba na mambo yote ya mapokeo ya kikristo, pia yale ya
unyago ulivyo katika mila za kila taifa kwa kiasi kiwezekanacho kufungamana na
ibada ya kikristo, kadiri ya ibara 37-40 za hati hii.
66. Ibada zote mbili za
Ubatizo wa wakubwa zitengenezwe, ile ya kawaida na ile ya Ubatizo wa sherehe
zaidi, kwa kuzingatia kuwekwa tena kwa ukatekumeni. Katika Misale ya Kiroma
Misa maalum “katika utoaji wa Ubatizo” iingizwe.
67. Ibada ya Ubatizo wa
watoto itengenezwe upya, nayo izingatie hali halisi ya watoto. Katika ibada
hiyo jukumu na wajibu wa wazazi na wasimamizi vitiliwe mkazo zaidi.
68. Katika ibada ya Ubatizo
iwepo pia mibadala fulani ya utaratibu, ya kutumia wakati wanaobatizwa ni
wengi, kadiri ya mwongozo wa Mkuu wa mahali. Itungwe pia ibada iliyo fupi zaidi
ambayo wanaweza kutumia, hasa katika nchi za misioni, makatekista au pia,
katika hatari ya kufa, waamini, ikiwa anakosekana Padre au Shemasi.
69. Badala ya “Ibada ya kukamilisha
yaliyoachwa katika Ubatizo wa watoto”, itungwe ibada mpya ambayo nayo ionyeshe
waziwazi zaidi kwamba mtoto, aliyekwisha kubatizwa kwa ibada fupi,
ameshapokelewa katika Kanisa.
Itungwe pia ibada maalum kwa wale
ambao wameshabatizwa kwa halali na baadaye wanaliongokea Kanisa Katoliki.
Katika ibada hiyo kusisitizwe kupokelewa kwao katika ushirika wa Kanisa.
70. Nje ya kipindi cha Pasaka, maji
ya Ubatizo yaweza kubarikiwa katika ibada yenyewe ya Ubatizo kwa formula fupi
maalum iliyoidhinishwa.
Marekebisho ya adhimisho la
Kipaimara
71. Ibada ya Kipaimara
itengenezwe upya ili ionyeshe vizuri zaidi uhusiano wa ndani wa Sakramenti hii
na zingine za kumwingiza mtu katika ukristo. Kwa hiyo, kurudia ahadi za Ubatizo
kutangulie kupokea Sakramenti hii.
Ikiwa inafaa, Sakramenti ya
Kipaimara inaweza kutolewa wakati wa Misa. Kama ibada itaadhimishwa nje ya
Misa, itayarishwe formula ya kutumia kama utangulizi.
Marekebisho ya adhimisho la Kitubio
72. Ibada na formula za Kitubio
zitengenezwe upya ili zionyeshe waziwazi zaidi maumbile na matokeo ya
Sakramenti hii.
Sakramenti ya Mpako wa wagonjwa
73. Sakramenti ya “Mpako wa
Mwisho”, ambayo inaweza kuitwa vizuri zaidi “Mpako wa wagonjwa”, si Sakramenti
kwa wale tu walio katika hali ya kuaga dunia. Kwa hiyo, wakati ufaao kwa
kuipokea ni ule mwamini aanzapo kuwa katika hatari ya kufa kwa sababu ya
ugonjwa na uzee.
74. Licha ya ibada mbili
tofauti, yaani ya Mpako wa wagonjwa na ya Komunyopamba, itungwe pia utaratibu
wenye mfululizo, ambamo Mpako utatolewa kwa mgonjwa baada ya Kitubio na kabla
ya kuipokea Komunyopamba.
75. Idadi ya mipako irekebishwe,
kadiri inavyoonekana inafaa; pia sala za ibada ya Mpako wa wagonjwa
zirekebishwe ili zilingane na hali tofauti ya kila mgonjwa anayepewa
Sakramenti.
Marekebisho ya adhimisho la Daraja
76. Ibada na matini
yanayohusu Sakramenti ya Daraja yarekebishwe. Mawaidha (Allocutiones) ya
Askofu mwanzoni mwa kila ibada ya Daraja yaweza kutolewa katika lugha ya nchi.
Katika ibada ya kumweka wakfu
Askofu, Maaskofu wote waliopo waweza kumwekea mikono yao juu yake.
Marekebisho ya adhimisho la Ndoa
77. Ibada ya Sakramenti ya
Ndoa, iliyomo katika Rituale ya Kiroma, irekebishwe na itajirishwe zaidi ili
neema ya Sakramenti iashirishwe waziwazi zaidi, na pia majukumu ya wafunga ndoa
yakazwe sana.
Katika adhimisho la
Sakramenti ya Ndoa, “kama katika mila na desturi za taifa zipo mila na sherehe
nyingine za kufaa, Mtaguso unatamani kabisa hizo zihifadhiwe”[41].
Aidha, Mabaraza ya Maaskofu
ya kila mahali, kama ilivyoelezwa katika ibara 22 § 2 ya hati hii, yanaweza
kutayarisha kwa mujibu wa ibara 63, ibada maalum, nayo ilingane na mila za
taifa; lakini kwa sharti itunzwe sheria ya kwamba Padre anayesimamia Ndoa aombe
na kupokea ukubaliano wa wafunga ndoa.
78. Kawaida Ndoa iadhimishwe
wakati wa Misa, baada ya Injili na homilia, kabla ya “sala za waamini”. Sala ya
kumwombea bibiarusi irekebishwe ili iwaeleze vizuri wanaarusi wote wawili
wajibu wao wa kuwa waaminifu wao kwa wao; lugha ya nchi inaweza kutumika katika
sala hii.
Lakini, ikiwa Sakramenti ya Ndoa
inaadhimishwa bila Misa, mwanzoni mwa ibada usomwe waraka na Injili ya Misa ya
Ndoa; vilevile kila mara baraka ya wanandoa itolewe.
Marekebisho ya Visakramenti
79. Visakramenti
virekebishwe, kadiri ya kanuni ya msingi kwamba waamini wawezeshwe kushiriki
kwa ufahamu, matendo, na kwa urahisi. Tena vilinganishwe na mahitaji ya siku
hizi. Katika kurekebisha miongozo yao, kadiri ya ibara 63, kama ikifaa, yawezekana
kuongeza pia Visakramenti vipya.
Baraka za pekee ziwe chache
sana, na kwa ajili ya Maaskofu na Wakuu [wa mahali] tu.
Jitihada zifanyike ili Visakramenti
vingine vitolewe na walei wenye uwezo na sifa zinazotakiwa, walau katika nafasi
za pekee na kwa uamuzi wa Mkuu anayehusika.
Nadhiri za kitawa
80. Ibada ya kuweka wakfu mabikira
iliyomo katika Pontifikale ya Kiroma irekebishwe.
Itungwe pia ibada ya kuweka nadhiri,
au uprofesi (professionis religiosae), na ya kurejea nadhiri (renovationis
votorum), yenye kuonyesha kwa wazi zaidi umoja, usahili na heshima. Nayo
itumiwe na wale wanaoweka nadhiri za maisha au za muda wakati wa Misa,
isipokuwa kwa nafasi ya pekee.
Ni vema nadhiri ziwekwe wakati wa
Misa.
Marekebisho ya ibada ya Mazishi
81. Ibada ya Mazishi ionyeshe
kinaganaga zaidi tabia ya kipasaka ya kifo cha kikristo. Pia mintarafu rangi ya
kiliturujia hiyo, na ilingane zaidi na mazingira na mapokeo ya kila kanda.
82. Irekebishwe pia ibada ya Mazishi
ya watoto na itungwe Misa maalum kwa ajili ya hiyo.
Sura
ya Nne
LITURUJIA
YA VIPINDI
Liturujia ya Vipindi ni tendo la
Kristo na la Kanisa
83. Kuhani Mkuu wa Agano
Jipya na la milele, Yesu Kristo, kwa kutwaa maumbile ya kibinadamu, ameingiza
katika ugeni huu wa hapa duniani wimbo ule unaoimbwa daima katika makao ya
mbinguni. Yeye anaunganisha naye jumuiya ya wanadamu wote mpaka washiriki naye
katika kuuinua wimbo huo wa kimungu na wa sifa.
Kwa kweli, Yesu huendeleza
tendo hili la kikuhani kwa njia ya Kanisa lake, ambalo humsifu Bwana Mungu bila
kukoma na kumwomba kwa ajili ya ukombozi wa ulimwengu mzima, si kwa njia ya
kuadhimisha Ekaristi tu, bali pia kwa namna nyingine, na hasa kwa kusali “Kazi
ya Mungu” (Officio divino), yaani Liturujia ya Vipindi.
84. Liturujia ya Vipindi,
kadiri ya mapokeo ya zamani ya kikristo, imewekwa ili mfululizo wa mchana na
usiku utakatifuzwe kwa njia ya sifa ya Mungu. Wakati wenye kuadhimisha wimbo
ule wa sifa na wa ajabu ni mapadre, au wengine waliowekwa kwa ajili hiyo na
sheria ya Kanisa, au pia waamini wanaosali pamoja na Padre kwa jinsi
inavyokubalika, hapo kweli ni sauti ya Bibiarusi mwenyewe anayeongea na
Bwanaarusi. Kwa kweli ni sala ya Kristo ambaye, pamoja na Mwili wake, humwomba
Baba.
85. Wote wanaotimiza tendo hilo
wanatekeleza wajibu wa Kanisa, na pia wanashiriki heshima kubwa sana ya
Bibiarusi wa Kristo kwa sababu, wanapomsifu Mungu, hukaa mbele ya kiti cha enzi
cha Mungu kwa niaba ya Mama Kanisa.
Umuhimu wa Liturujia ya Vipindi
katika uchungaji
86. Mapadre wanaotekeleza
huduma takatifu ya kichungaji watasali masifu ya Vipindi kwa juhudi kubwa zaidi
kiasi ambacho kitawasukuma kushika onyo la Mtume Paulo: “Ombeni bila kukoma”
(1The 5:17). Kwa maana Bwana peke yake tu anaweza kuleta na kukuza matunda ya
kazi wanayofanya, yeye aliyesema: “Bila mimi hamwezi kufanya lolote” (Yn 15:5).
Kwa sababu hiyo Mitume, walipowawekea mikono mashemasi, walisema: “Na sisi
tutadumu katika kuomba na kulihudumia lile Neno” (Mdo 6:4).
87. Ili mapadre na waamini wengine
waweze kusali vizuri na kikamilifu zaidi Liturujia ya Vipindi katika nafasi
mbalimbali, Mtaguso Mkuu, ukiendeleza marekebisho yaliyoanzishwa na Kiti cha
Kitume, unapenda kuagiza yafuatayo kuhusu Liturujia ya Vipindi, kufuatana na
Riti ya Kiroma.
Marekebisho ya utaratibu wa
Liturujia ya Vipindi
88. Kwa vile lengo la Liturujia ya
Vipindi ni kutakatifuza siku nzima, utaratibu wa kimapokeo wa vipindi
urekebishwe ili Sala za Vipindi zifanywe kwa wakati wake, kadiri
inavyowezekana. Vilevile hali ya maisha ya siku hizi, na hasa ya wale
wanaojibidisha katika matendo ya kitume, iangaliwe.
Mwongozo kwa marekebisho ya
Liturujia ya Vipindi
89. Kwa hiyo, katika
kurekebisha Liturujia ya Vipindi, ufuatwe mwongozo huu:
a) Masifu ya Asubuhi (Laudes),
kama sala ya asubuhi, na Masifu ya Jioni (Vesperae), kama sala ya jioni,
kadiri ya mapokeo yenye heshima ya Kanisa lote ni bawaba maradufu ya Liturujia
ya Vipindi ya kila siku. Hivyo yatazamwe kama Vipindi muhimu zaidi na
yaadhimishwe kufuatana na umuhimu wake;
b) Utaratibu wa Sala ya
Usiku, au Kompleto (Completorium), urekebishwe ili ulingane inavyofaa na
mwisho wa siku;
c) Sala ya Kipindi kiitwacho Mikesha
(Matutinum), ingawa kinaendelea kuwa kipindi cha sala kwa ajili ya usiku
kisaliwapo pamoja katika kwaya (in choro), irekebishwe ili iweze
kutumika wakati wowote wa siku, tena iwe na zaburi chache na masomo marefu
zaidi;
d) Kipindi cha Kwanza (Prima)
kifutwe;
e) Katika kwaya Vipindi vidogo vya
Kabla ya Adhuhuri au Tersia (Tertia), Adhuhuri au Sesta (Sexta)
na Baada ya Adhuhuri au Nona (Nona) vihifadhiwe. Nje ya kwaya
inaruhusiwa kuchagua kimoja kati ya hivyo vitatu, kadiri ya majira ya siku.
Liturujia ya Vipindi ni chemchemi ya
uchaji
90. Licha ya hayo, Liturujia
ya Vipindi ni sala ya hadhara ya Kanisa na chemchemi ya uchaji na chakula cha
sala ya binafsi. Kwa hiyo, mapadre na waamini wengine wote wanaoshiriki
Liturujia ya Vipindi tunawasihi ili, katika kusali, akili na sauti zao
viungane; kwa kufikia lengo hilo wahusika wajipatie ufahamu wa kina zaidi wa
Liturujia na wa Biblia hasa kuhusu zaburi.
Katika kufanya marekebisho hayo,
hazina yenye heshima na ya zamani iliyomo katika Breviari ya Kiroma irekebishwe
ili waliokabidhiwa waweze kuitumia zaidi na kwa urahisi.
Mgawanyo wa Zaburi
91. Ili utaratibu wa Vipindi
uliopendekezwa katika ibara 89 uweze kutekelezwa kweli, zaburi zigawanywe sio
tena katika juma moja, bali katika muda mrefu zaidi.
Kazi hii ya kurekebisha mgawanyo wa
zaburi, iliyoanzishwa vizuri, imalizwe kwa haraka, bila kusahau Kilatini
kinachotumiwa na wakristo, na matumizi yake ya kiliturujia katika nyimbo. Vivyo
hivyo mapokeo yote ya Kanisa la Kiroma yasisahauliwe.
Utaratibu wa masomo
92. Kuhusu masomo, mwongozo
ufuatao uzingatiwe:
a) Usomaji wa Maandiko
Matakatifu upangwe ili hazina za Neno la Mungu zipatikane katika wingi wake kwa
urahisi zaidi;
b) Masomo yachukuliwayo kutoka
maandiko ya Mababa, Waalimu na Waandishi wa Kanisa, yachaguliwe vizuri zaidi;
c) Masimulizi ya mateso ya
watakatifu, yaani maisha yao, yarudishwe katika ukweli wa kihistoria.
Marekebisho ya tenzi
93. Pia tenzi zirudishwe katika
mtindo wao wa asili, kwa kiasi kifaacho; na yale yaliyo katika hali ya visasili
(mythologiam) au yasiyofaa kwa uchaji wa Mungu yaondolewe au
yabadilishwe. Aidha, zichukuliwe tena tenzi nyingine, kadiri ifaavyo, zilizomo
katika mikusanyo mbalimbali.
Wakati wa kusali kila Kipindi
94. Ili kutakatifuza kweli siku na
kusali Vipindi vyenyewe kwa matunda ya kiroho, Sala za Vipindi zifanywe
kulingana na majira yake, yaani sambamba na wakati halisi wa kila Kipindi.
Ulazima wa Liturujia ya Vipindi
95. Jumuiya zenye sharti la
kusali pamoja zinatakiwa kusali katika kwaya Liturujia ya Vipindi kila siku,
zaidi ya Misa ya shirikani; na hasa:
a) Jumuiya za Wakanoniki,
Mashirika ya Wamonaki wa kike na wa kiume na wale watawa wote (Regularium)
wanaotakiwa kusali pamoja katika kwaya, kadiri ya sheria na katiba zao,
wanapaswa kusali Vipindi vyote.
b) Kapitulo za Makanisa Makuu
na za Kolejata zinapaswa kusali sehemu zile za Ofisyo zinazoamriwa katika
sheria za kawaida au za pekee.
c) Wanashirika wote
waliotajwa juu, ambao wamepewa Daraja kuu (Ordinibus maioribus) au
wameweka nadhiri za maisha, isipokuwa ndugu watawa walei (conversis),
wanapaswa kusali peke yao Vipindi vile wasivyosali katika kwaya.
96. Makleri wasiopasika
kusali katika kwaya, kama wamepewa Daraja kuu, wanapaswa kusali sala zote za
Vipindi kila siku peke yao au kwa pamoja, kadiri ya ibara 89.
97. Mwongozo wa kushiriki
ibada nyingine kama mibadala ya kufaa ya Liturujia ya Vipindi uratibiwe.
Katika nafasi za pekee na kwa
sababu halali, Wakuu wa mahali wanaweza kuwaruhusu wale walio chini yao
kutofungwa na ulazima wa kusali Liturujia ya Vipindi, ama kufanya ibada
nyingine badala yake.
98. Wanashirika wa taasisi
yoyote ya kitawa ambao kwa mujibu wa Katiba husali sehemu kadhaa za Liturujia
ya Vipindi, huonyesha sala ya hadhara ya Kanisa.
Vilevile wanaonyesha sala ya hadhara
ya Kanisa kama, kwa mujibu wa Katiba, wakisali “Ofisyo fupi”, mradi zimetungwa
kulingana na mpango wa Liturujia ya Vipindi ya kawaida na kuidhinishwa
inavyotakiwa.
Kusali pamoja Liturujia ya Vipindi
99. Liturujia ya Vipindi ni sauti ya
Kanisa, yaani ya Mwili wote wa fumbo unaomsifu Mungu hadharani. Kwa hiyo,
Mtaguso unawasihi makleri wasiopasika kusali katika kwaya na hasa mapadre
wanaoishi au kukutana pamoja, wasali pamoja walau sehemu kadhaa za Liturujia ya
Vipindi.
Aidha, wale wote wanaosali Liturujia
ya Vipindi kwa pamoja au katika kwaya, watimize, kikamilifu iwezekanavyo,
wajibu waliokabidhiwa kwa uchaji wa rohoni na pia kwa vitendo vya nje.
Pia ni vema, kama inawezekana,
Liturujia ya Vipindi katika kwaya au kwa pamoja iimbwe.
Kushiriki kwa waamini katika
Liturujia ya Vipindi
100. Wachungaji wa roho wajitahidi
kwamba Vipindi vikuu vya sala, hasa Masifu ya Jioni (Vesperae),
viadhimishwe kanisani pamoja na waamini siku ya Dominika na Sikukuu kubwa
zaidi. Walei pia wanahimizwa wasali Liturujia ya Vipindi au pamoja na mapadre,
au wakiungana kati yao, au kila mmoja peke yake.
Lugha katika Liturujia ya Vipindi
101. § 1. Kadiri ya mapokeo
ya zamani ya riti ya kilatini, wakleri wanapaswa kuhifadhi lugha ya kilatini
katika Liturujia ya Vipindi. Lakini Mkuu wao ana uwezo wa kuruhusu matumizi ya
tafsiri katika lugha ya nchi, iliyoandaliwa kadiri ya ibara 36, kwa wale
wakleri mmoja mmoja (singulis pro casibus) ambao kwao matumizi ya lugha
ya kilatini ni kizuio kikubwa kwa kusali Liturujia ya Vipindi ipasavyo.
§ 2. Kwa wamonaki wa kike (monialibus)
na wanajumuiya wa mashirika ya kitawa, au wasio wakleri, au wa kike, Mkuu wao
anayehusika anaweza kuruhusu matumizi ya lugha ya nchi katika Liturujia ya
Vipindi, hata ikiadhimishwa katika kwaya, lakini tafsiri iidhinishwe.
§ 3. Kila mkleri anayepaswa kusali
Liturujia ya Vipindi, akisali katika lugha ya nchi pamoja na waamini, au pamoja
na wale waliotajwa katika § 2, anatimiza wajibu wake. Hata hivyo, tafsiri
inayotumika iwe imeidhinishwa.
Sura
ya Tano
MWAKA
WA LITURUJIA
Maana ya Mwaka wa Liturujia
102. Mama Kanisa takatifu huchukulia
wajibu wake kuadhimisha kwa kumbukumbu takatifu kazi ya ukombozi ya Bwanaarusi
wake aliye Mungu, katika siku zilizopangwa katika mwenendo wa mwaka mzima. Kila
juma Kanisa, katika siku aliyoiita “Dominika”, yaani “Siku ya Bwana”,
anaadhimisha kumbukumbu ya ufufuko wa Bwana. Kwa namna ya pekee anauadhimisha
ufufuko huo pamoja na mateso yake yenye heri mara moja kwa mwaka katika Sikukuu
ya Pasaka, iliyo kubwa kuliko Sherehe zote.
Katika mzunguko wa mwaka mzima,
[Mama Kanisa] analikunjua fumbo la Kristo, tangu umwilisho na kuzaliwa, hadi
kupaa mbinguni, mpaka siku ya Pentekoste na kungojea kwa tumaini lenye heri
kurudi kwake Bwana.
Anapokumbuka namna hii
mafumbo ya ukombozi, Kanisa huwafungulia waamini utajiri wa uweza na mastahili
ya Bwana wake. Kwa njia hii, uwepo wa mafumbo haya unakuwapo kwa nyakati zote,
ili kutoka humo waamini waweze kuchota na kujazwa neema ya wokovu.
103. Kwa kuadhimisha katika mzunguko
huo wa [kila] mwaka mafumbo ya Kristo, Kanisa humheshimu kwa upendo wa pekee
Maria mwenye heri, Mama wa Mungu, ambaye ameunganika na Mwana wake kwa namna
isiyoweza kutengwa, katika kazi ya wokovu. Tena, ndani ya Maria, Kanisa hustahi
na kutukuza tunda bora kuliko yote la ukombozi, na pia hutazama kwa furaha,
kama katika mfano usio na doa, yale anayoyatamani na kuyatumaini kwa ajili yake
lote.
Kumbukumbu za Mashahidi na za
Watakatifu
104. Kanisa limeingiza pia
katika mwaka wa Liturujia kumbukumbu za Mashahidi na za Watakatifu wengine
ambao, baada ya kufikia ukamilifu kutokana na neema ya Mungu iliyo ya namna
nyingi, na wakishapata ukombozi wa milete, wanaimba sifa kamili ya Mungu kule
mbinguni na kutuombea.
Kwa kuadhimisha siku za
kuzaliwa [mbinguni] kwa Watakatifu Kanisa latangaza fumbo la Pasaka lionekanalo
katika Watakatifu walioteswa pamoja na Kristo na kutukuzwa pamoja naye, na
lawaonyesha waamini mifano yao inayowavutia wote kwa Baba kwa njia ya Kristo.
Pia linawaombea fadhili za Mungu kwa njia ya mastahili yao.
105. Kanisa, katika vipindi
mbalimbali vya mwaka na kadiri ya utaratibu wa kimapokeo, linatimiza wajibu
wake wa kuwakomaza waamini kwa njia ya matendo ya kiroho na kimwili,
mafundisho, sala pamoja na matendo ya toba na ya huruma.
Kwa sababu hiyo Mtaguso Mkuu kwa
dhati unaamua yafuatayo.
Umuhimu wa Dominika
106. Kadiri ya mapokeo ya Mitume,
yanayopata asili yake katika siku ya ufufuko wa Kristo, Kanisa huadhimisha
fumbo la Pasaka kila siku ya nane, katika siku ile iitwayo kwa haki kabisa Siku
ya Bwana au Dominika. Katika siku hii waamini wanapaswa kujumuika pamoja ili,
wanaposikiliza Neno la Mungu na kushiriki Ekaristi, wafanye ukumbusho wa
mateso, ufufuko na utukufu wa Bwana Yesu. Na pia watoe shukrani kwa Mungu
“aliyewazaa upya katika tumaini lenye uhai kwa njia ya ufufuko wa Yesu Kristo
katika wafu” (1Pet 1:3). Kwa hiyo, siku ya Dominika ni Sikukuu ya kwanza ambayo
ni lazima ielezwe vizuri na kuingizwa, kwa kadiri inavyowezekana, katika maisha
ya kidini ya wakristo, ili iweze kuwa pia siku ya furaha na ya kuacha kazi.
Sherehe nyingine zisitiliwe mkazo sana, isipokuwa zile zenye umuhimu zaidi, kwa
sababu siku ya Dominika ni msingi na kiini cha mwaka mzima wa Liturujia.
Marekebisho ya Mwaka wa Liturujia
107. Mwaka wa Liturujia
urekebishwe ili zihifadhiwe au ziingizwe tena desturi na taratibu za vipindi
vitakatifu kadiri ya hali ya nyakati zetu. Pia maana yao ya asili ihifadhiwe
ili kulisha ipasavyo uchaji wa waamini katika kuadhimisha mafumbo ya ukombozi
wa Kristo, na hasa fumbo la Pasaka. Aidha, ikiwa ni lazima, marekebisho
yafanywe kulingana na hali ya kila mahali kadiri ya ibara 39 na 40.
108. Roho za waamini zielekezwe
kwanza kabisa kwenye sikukuu za Bwana, ambamo, katika mwaka, yanaadhimishwa
mafumbo ya wokovu. Kwa hiyo Vipindi vya Mwaka (Proprium de Tempore)
vipewe umuhimu wake kuliko sikukuu za Watakatifu, ili mfululizo mzima wa
mafumbo ya wokovu uadhimishwe ipasavyo.
Kwaresima
109. Maana mbili zinazofanya
kipekee Kipindi cha Kwaresima, ukumbusho wa Ubatizo au matayarisho yake, na
toba, zitiliwe mkazo wa pekee katika Liturujia na katekesi ya Liturujia. Nazo
zinasaidia kuwaandaa waamini kuadhimisha fumbo la Pasaka, wakisikiliza mara
nyingi zaidi Neno la Mungu na kujibidisha katika kusali. Kwa hiyo:
a) Mambo yote yadokezayo
Ubatizo yaliyomo katika Liturujia ya Kwaresima yapewe nafasi kubwa zaidi, na
pia, kama inafaa, yaingizwe tena mengine yatokanayo na mapokeo ya zamani;
b) Vivyo hivyo ifanywe kuhusu mambo
ya toba. Mintarafu katekesi, juhudi ifanywe ili iweze kuingizwa rohoni mwa
waamini, pamoja na matokeo ya kijamii ya dhambi, maumbile halisi ya toba yenye
kuchukia dhambi kwa sababu ni kumtukana Mungu; nafasi ya Kanisa katika tendo la
toba isisahauliwe kamwe, na pia sala kwa ajili ya wakosefu ihimizwe.
110. Toba ya wakati wa Kwaresima
isiwe ni tendo la ndani na la binafsi tu, bali pia lionekanalo kwa nje na
katika maisha ya jamii. Matendo ya toba na kujinyima, kadiri ya uwezekano wa
nyakati zetu na mahali mbalimbali, na pia kadiri ya hali ya waamini,
yasisitizwe na kuhimizwa na wale wenye mamlaka, kama ilivyoelezwa katika ibara
22.
Lakini tendo la kufunga chakula
wakati wa Pasaka litakuwa takatifu, nalo liadhimishwe popote siku ya Ijumaa ya
Mateso na Kifo cha Bwana na kuendelea, kama inawezekana, siku nzima ya Jumamosi
Kuu, ili kufikia furaha na shangwe ya Dominika ya Ufufuko kwa moyo wazi na
ulioinuliwa.
Sherehe za Watakatifu
111. Katika Kanisa, kadiri ya
mapokeo, Watakatifu huheshimiwa; vivyo hivyo masalia yao halisi na picha zao
huhifadhiwa kwa heshima. Maana sherehe za Watakatifu zinatangaza matendo ya
ajabu ya Kristo ndani ya watumishi wake, na pia zinawaonyesha waamini mifano
bora ya kuiga.
Ili sikukuu za Watakatifu zisipewe
umuhimu zaidi kuliko zile zinazokumbusha mafumbo ya wokovu, nyingi kati ya
sikukuu hizo [za Watakatifu] ziadhimishwe tu katika Kanisa faridi, au Taifa au
Shirika. Sikukuu zile tu zinazowakumbuka Watakatifu wenye umuhimu kwa wote
ziadhimishwe katika Kanisa zima.
Sura
ya Sita
MUZIKI
MTAKATIFU
Umuhimu wa muziki wa kiliturujia
112. Mapokeo ya kimuziki ya
Kanisa lote ni hazina yenye thamani isiyopimika, inayozidi aina nyingine ya
sanaa, hasa kwa sababu kuimba kutakatifu, kukiunganika na maneno, ni sehemu ya
lazima na ya ndani ya Liturujia ya sherehe.
Hakika kuimba kutakatifu kumesifiwa
katika Maandiko Matakatifu[42]na
pia na Mababa wa Kanisa na Mapapa wa Kanisa la Kiroma, ambao nyakati hizi
kwanzia na Mt. Pius X, wamesisitiza kwa dhati karama na huduma ya kuimba
kutakatifu katika ibada ya Liturujia.
Kwa hiyo, muziki mtakatifu utazidi
kuwa mtakatifu pale uunganikapo na tendo la Liturujia; maana utafanya sala kuwa
tamu zaidi na kuonyesha umoja wa mioyo, pia utaleta heshima zaidi katika
maadhimisho matakatifu. Tena Kanisa linakubali na kuingiza katika ibada kwa
Mungu mitindo yote ya sanaa ya kweli, lakini yenye sifa zinazotakiwa.
Kwa hiyo, Mtaguso Mkuu unahifadhi
kanuni na sheria zilizokubalika na za mapokeo ya Kanisa, na pia unalenga
shabaha ya muziki mtakatifu, ambayo ni utukufu wa Mungu na kutakatifuzwa kwa
waamini. Ili kutekeleza kusudi hilo, Mtaguso Mkuu unaamua yafuatayo.
Liturujia ya Sikukuu
113. Tendo la Liturujia
hupata kuwa na heshima zaidi wakati linapoadhimishwa katika sherehe kwa kuimba,
wakiwepo makasisi na kwa ushirikiano hai wa waamini.
Kuhusu matumizi ya lugha,
ibara 36 izingatiwe; juu ya Misa, kama ilivyoelezwa katika ibara 54; kwa
Sakramenti, ifuatwe ibara 63, na mintarafu Liturujia ya Vipindi, ifanywe kama
isemavyo ibara 101.
114. Hazina ya mapokeo ya muziki
mtakatifu ihifadhiwe na kukuzwa kwa uangalifu sana. Shule za Kwaya (Scholae
cantorum) zihimizwe, hasa katika Makanisa Makuu. Aidha, Maaskofu na
wachungaji wengine wa roho wafanye jitihada ili katika kila ibada iadhimishwayo
kwa kuimba, waamini wote waweze kushiriki kikamilifu, kadiri ya ibara 28 na 30.
Uandaaji wa wanamuziki
115. Jitihada kubwa ifanyike
ili kuhamasisha elimu na mazoezi ya muziki katika seminari, katika nyumba za
unovisi za mashirika ya kiume na ya kike, katika nyumba za wanafunzi, kama vile
vyuo na shule za kikatoliki; ili kupata elimu hii, walimu waandaliwe kwa bidii
kubwa, kisha watumwe kufundisha muziki mtakatifu.
Ikiwa inafaa, uundaji wa
Taasisi za Juu za muziki mtakatifu uhimizwe.
Wanamuziki, wanakwaya, na juu ya
wote watoto, wapewe elimu halisi ya kiliturujia.
Nyimbo za kigregoriani na nyinginezo
116. Kanisa anautambua uimbaji wa
mtindo wa kigregoriani kuwa ndio ulio rasmi wa Liturujia ya Kiroma: kwa hiyo,
katika matendo ya Liturujia ushike nafasi ya kwanza, isipokuwa kwa sababu
maalum.
Mitindo mingine ya muziki mtakatifu,
hasa ile itumiayo sauti nyingi (polyphonia), isiondolewe katika
maadhimisho ya ibada kwa Mungu, lakini ilingane na roho ya tendo la Liturujia,
kadiri ya ibara 30.
117. Toleo halisi (Editio
typica) la vitabu vya nyimbo za kigregoriani lichapwe; tena ni afadhali
litayarishwe toleo halisi zaidi kuliko vitabu vilivyochapwa baada ya
matengenezo ya Mt. Pius X.
Licha ya toleo hilo, bora
litayarishwe toleo jingine lenye tuni zilizo rahisi zaidi, la kutumia katika
makanisa madogo.
Nyimbo za kidini za mahali
118. Nyimbo za kidini za [wakristo]
wenyeji zihimizwe kwa bidii, ili katika ibada mbalimbali za watu na pia katika
matendo ya Liturujia sauti za waamini ziweze kusikika vizuri, kadiri ya
utaratibu na madai ya miongozo.
Muziki ya kiliturujia katika misioni
119. Katika nchi kadha wa
kadha, hasa zile za Misioni, yapo mataifa yenye mapokeo yao ya muziki ambayo
yana maana kubwa katika maisha yao ya kidini na ya kijamii. Muziki huu upewe
heshima na nafasi inayofaa katika kuyaelimisha mataifa hayo kidini, na pia
katika kutengeneza ibada kwa kulingana na tabia yao, kadiri ya ibara 39 na 40.
Kwa hiyo, katika kuwaelimisha
wamisionari juu ya muziki, jitihada ifanyike ili, kadiri inavyowezekana, waweze
kuendeleza muziki wa kimapokeo wa mataifa yanayohusika, katika mashule na
katika ibada takatifu.
Organi na ala nyingine za muziki
120. Katika Kanisa la Kiroma,
organi ya mianzi ipewe nafasi ya heshima, kama ala ya kimapokeo ya muziki
ambayo kwayo muziki huongeza fahari ya ajabu kwa ibada za Kanisa, na pia huinua
roho za waamini kwa Mungu na kwa mambo ya mbinguni.
Ala nyingine za muziki pia zinaweza
kutumika katika ibada kwa Mungu, kwa uamuzi na kibali cha Mabaraza ya Maaskofu
ya kila mahali, kadiri ya ibara 22 § 2, 37 na 40. Lakini sharti ziwe za kufaa
kwa matumizi matakatifu au zigeuzwe ili zifae kwa lengo hili. Tena, zilingane
na heshima ya hekalu na zisaidie kujenga [uchaji wa] waamini.
Wajibu wa watunga muziki
121. Watunga muziki,
wakisukumwa na roho ya kikristo, wajione kuwa wameitwa kuustawisha muziki
mtakatifu na kukuza hazina yake.
Pia watunge melodia
zinazolingana na sifa za muziki mtakatifu na ambao unaweza kuimbwa si tu na
kwaya kubwa, bali pia na kwaya ndogo. Tena ziwasaidie waamini wote kushiriki
kikamilifu.
Maneno yaliyomo katika nyimbo
yalingane na mafundisho ya Kanisa katoliki, zaidi yachukuliwe hasa katika Maandiko
Matakatifu na vitabu vya liturujia.
Sura
ya Saba
SANAA
TAKATIFU NA VIFAA VITAKATIFU
Hadhi ya sanaa takatifu
122. Mambo ya sanaa (artes
ingenuae) yanahesabika kwa haki kati ya kazi za maarifa ya kibinadamu zenye
heshima zaidi. Kati ya hizo, sanaa ya kidini na kilele chake ambacho ni sanaa
takatifu zinaheshimiwa kwa namna ya pekee. Hizo, kwa maumbile yao, huhusiana na
uzuri usiopimika wa Mungu, ambao lazima udhihirishwe kwa namna fulani katika
kazi za mwanadamu. Tena, huelekea kwa Mungu na kwa kukuza sifa na utukufu wake,
kwa sababu hazina lengo jingine isipokuwa kuzielekeza kwa nguvu na kikamilifu,
kwa njia ya matunda yao, akili za wanadamu kwa Mungu.
Kwa sababu hizo, Mama Kanisa
takatifu daima amependelea sanaa na kutafuta huduma yao yenye heshima, ili
mambo yahusuyo ibada takatifu yapewe kweli heshima na uzuri, kwani hayo ni
alama na ishara za yale ya mbinguni. Kwa hiyo, Kanisa pia amejitahidi kuwalea
wanasanaa. Tena Kanisa, tangu awali na kwa haki, amejiona kuwa mwamuzi juu ya
mambo ya sanaa, akichagua kati ya kazi za wanasanaa zile zilinganazo na imani,
uchaji na kanuni za mapokeo, ili zifae kwa matumizi ya kidini.
Kwa bidii ya pekee Kanisa
amejitahidi ili vifaa vitakatifu vitumike kadiri ya heshima na uzuri wa ibada;
na pia amekubali mabadiliko yale ya malighafi, ya maumbo na ya madoido
yaliyoingizwa na maendeleo ya mbinu za sanaa katika mwenendo wa karne.
Kwa hiyo, Mababa wamependa kuamua
yafuatayo.
Matumizi ya mitindo mbalimbali ya
sanaa
123. Kanisa hana mtindo wake maalum
wa sanaa, lakini amekubali mitindo ya sanaa ya kila karne, kadiri ya tabia na
mila za mataifa, na pia kufuatana na matakwa ya kila ibada. Hivyo, katika
mwenendo wa karne, Kanisa ameandaa hazina ya sanaa ambayo lazima kuhifadhi kwa
uangalifu mkubwa. Sanaa ya siku hizi na ya mataifa yote na ya nchi zote ipate
uhuru wa kujionyesha katika Kanisa, mradi tu iwe kwa ajili ya heshima na
matakwa ya majengo matakatifu na maadhimisho ya kiliturujia. Kwa njia hii,
[sanaa takatifu ya siku hizi] iwezeshwe kuunganisha sauti yake na kwaya ile ya
ajabu [ya masifu kwa ajili] ya utukufu ambayo wanasanaa maarufu katika karne
zilizopita waliimba kwa imani katoliki.
124. Katika kuhimiza na kuhamasisha
sanaa takatifu halisi, wenye mamlaka katika Kanisa watafute uzuri wenye heshima
kuliko fahari tupu. Vivyo hivyo ifanywe mintarafu mavazi na vifaa vitakatifu.
Maaskofu wasikubali kamwe
matendo ya sanaa yapinganayo na imani na maadili na uchaji wa kikristo katika
nyumba ya Mungu na mahali pengine patakatifu. Pia wakatae yale yanayovunja
heshima halisi ya kidini kwa sababu ni mapotovu kwa upande wa maumbo au kwa
sababu ya utovu wa uzuri wa kisanaa, au ya uhafifu wake au hila.
Katika kujenga majengo
matakatifu jitihada ifanyike ili yafae kwa ajili ya kuadhimisha Liturujia na
kwa kuwawezesha waamini kushiriki kikamilifu.
125. Desturi ya kuonyesha picha na
sanaa takatifu katika makanisa, kusudi waamini waweze kuziheshimu, iimarishwe.
Hata hivyo, idadi yake iwe ya kiasi kifaacho, na mahali zinapowekwa pafuate
utaratibu unaotakiwa, ili kutowakwaza baadhi ya waamini na kutohimiza uchaji
usio halali.
Sanamu takatifu
126. Katika kuhakiki kazi za
sanaa, Wakuu wa mahali wasikilize mapendekezo ya Kamati ya Sanaa takatifu ya
Jimbo; na pia, kama inatakiwa, wapokee mapendekezo kutoka kwa wale wenye ujuzi
maalum, na kwa zile kamati zilizotajwa katika ibara 44, 45 na 46.
Wenye mamlaka wakae macho ili vifaa
vitakatifu au vitu vya thamani, kwa vile ni urembo wa nyumba ya Mungu,
visichukuliwe au kuharibiwa.
Malezi ya wanasanaa
127. Maaskofu, wenyewe au kwa
njia ya mapadre wanaofaa ambao wanajua na kupenda sanaa, wawaangalie wanasanaa
kwa namna ya pekee, ili kuwaelimisha juu ya roho ya sanaa takatifu na ya
Liturujia takatifu.
Pia inatamaniwa kuanzisha shule au
idara za sanaa takatifu katika nchi zile ambazo inaonekana inafaa, ili kuwalea
wanasanaa.
Wanasanaa wote ambao,
wakiongozwa na maarifa yao, wanataka kutumikia utukufu wa Mungu katika Kanisa
takatifu, daima wakumbuke kwamba wanafanya kazi ambayo ni mtindo wa igizo
takatifu la Mungu Mwumbaji. Na pia matunda ya kazi yao yatakuwa kwa ajili ya
ibada katoliki, kukuza imani na uchaji na malezi ya kidini ya waamini.
Marekebisho ya sheria za sanaa takatifu
128. Sheria za Kanisa na
miongozo ya Kanisa inayohusu mambo ya nje yahusuyo ibada takatifu, pamoja na
vitabu vya Liturujia, vitengenezwe upya upesi iwezekanavyo, kadiri ya ibara 25.
Hasa yatazamwe tena mambo yafuatayo: ujenzi unaostahili na wa kufaa wa majengo
matakatifu; umbo na utengenezaji wa altare; heshima, mahali na usalama wa
tabernakulo ya Ekaristi; kufaa kwa mahali pa kubatizia na heshima yake; sehemu
ifaayo kwa kuweka sanamu, picha takatifu na mapambo yote. Kutokana na msingi
huo, sheria zile zisizolingana na marekebisho ya Liturujia zisahihishwe au
kufutwa; lakini zile zinazoinufaisha zitunzwe au kuingizwa tena vipya.
Kwa jambo hilo, na hasa kuhusu
malighafi na mitindo ya vifaa vitakatifu na mavazi, Mabaraza ya Maaskofu ya
kila mahali yanaruhusiwa kufanya marekebisho yanayotakiwa kadiri ya mahitaji na
mila za mahali panapohusika na kufuatana na ibara 22 ya hati hii.
Uandaaji wa makleri mintarafu sanaa
129. Makleri, wakati wa masomo ya
falsafa na teolojia, waelimishwe pia kuhusu historia na maendeleo ya sanaa
takatifu, kama vile kanuni halisi zinazoongoza utengenezaji wa vitu vya sanaa
na hivyo waweze kuheshimu na kulinda majengo na matendo matakatifu (venerabilia
monumenta) na pia kutoa ushauri kwa wanasanaa, ili watimize vema kazi yao.
Zana za kiaskofu
130. Inafaa ishara za kiaskofu
zitumiwe na watu wa Kanisa tu wenye Daraja ya kiaskofu au mamlaka ya pekee.
Nyongeza
TANGAZO
LA MTAGUSO MKUU VATIKANO II
KUHUSU
MATENGENEZO YA KALENDA
MATENGENEZO YA KALENDA
Mtaguso Mkuu Vatikano II hutilia
maanani sana matakwa ya wengi, yaani ya kutaka Sikukuu ya Pasaka iangukie daima
Dominika fulani na hivyo kudai matumizi ya kalenda isiyobadilika. Kwa sababu
hiyo, baada ya kuchunguza kwa makini yale yanayoweza kutokana na matumizi ya
kalenda mpya ya namna hii, Mtaguso Mkuu unatangaza yafuatayo:
1. Mtaguso Mkuu hauna kizuizi
chochote kwa kuichagua Dominika fulani ya Kalenda ya Kigregoriani kuwa Sikukuu
ya Pasaka. Ila kiwepo kibali cha wale wanaohusika, hasa ndugu zetu waliojitenga
na Kiti cha Kitume.
2. Vilevile Mtaguso Mkuu
hauwapingi wale ambao wangependa kuingiza aina tofauti ya kalenda ya kudumu
katika maisha ya kijamii.
Lakini, kati ya aina hizo mbalimbali
za kalenda za kudumu zinazopendekezwa ili ziingizwe katika maisha ya kijamii,
Kanisa linadai juma moja liendelee kuwa na jumla ya siku saba pamoja na
Dominika. Kwa hiyo, zisiongezwe siku nyingine zaidi ya zile saba za juma, ili
mfululizo wa majuma usibadilike; isipokuwa kama zipo sababu nzito mno. Nazo
hazina budi kukubaliwa na Kiti cha Kitume.
Mambo yote yaliyoamuliwa katika
konstitusio hii, na kila moja kati yao, yamewapendeza Mababa wa Mtaguso Mkuu.
Nasi, kadiri ya mamlaka ya kitume tuliyopewa na Kristo, na pamoja na Mababa
waheshimiwa, katika Roho Mtakatifu, tunayakubali, tunayaidhinisha na
tunayathibitisha. Na yale yote yaliyoamuliwa kwa pamoja katika Sinodi hii,
tunaamuru yawekwe kwa utukufu wa Mungu.
Roma, katika Kanisa la Mtakatifu
Petro, 4 Desemba 1963
Mimi
mwenyewe Paulo, Askofu wa Kanisa Katoliki
(zinafuata
sahihi za Mababa)
Comments
Post a Comment