Majadiliano ya kiekumene hayakwepeki: Askofu Ruzoka asisitiza
JIMBO
Kuu Katoliki Tabora linaendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene ili
kujenga na kudumisha majadiliano ya kiekumene miongoni mwa Wakristo.
Askofu Mkuu Paul Ruzoka wa Jimbo Kuu Katoliki
Tabora, katika mahojiano na gazeti hili hivi karibuni amesema kuwa, majadiliano ya kiekumene ndani ya Kanisa ni
kati ya mada zilizojadiliwa na kutolewa maamuzi na Sinodi ya kwanza ya Jimbo Kuu
Tabora iliyoadhimishwa hivi karibuni kwa kuongozwa na kauli mbiu “Yesu hu seba”
yaani “Yesu ni taa ya uhai wa imani
yetu.”
Kanisa linatambua kwamba, Kristo Yesu ndiye
muasisi wake na kwamba, aliunda: Kanisa moja, Takatifu, Katoliki na la Mitume.
Kumbe, majadiliano ya kiekumene miongoni mwa Makanisa ni jitihada za kutaka
kujenga na kudumisha umoja wa Kanisa kama Kristo mwenyewe alivyoliombea, liwe
na umoja. (Rej. Yn. 17: 21) Ikumbukwe kwamba, asili ya Kanisa ni moja,”ameeleza
Askofu Mkuu Ruzoka,
Aidha amesisitiza kuwa, Maaskofu Mahalia
kwa kushirikiana na Khalifa wa Mtakatifu Petro wanapaswa kukoleza ari na moyo
wa majadiliano ya kiekumene yanayojikita katika: ushuhuda wa imani yao kwa
Kristo na Kanisa lake hata kiasi cha kumwaga damu yao; ushuhuda wa sala na
maisha ya kiroho kwa kusali na kutafakari pamoja Neno la Mungu linalopaswa kuwa
ni dira na mwongozo wa maisha ya Wakristo pamoja na kushikimana kwa dhati
katika kuwahudumia maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.
Askofu Mkuu Ruzoka anaendelea kufafanua
kwamba, juhudi za majadiliano ya kiekumene zilianza tangu wakati wa maadhimisho
ya Mtaguso wa Pili wa Lyon mnamo mwaka 1276; Mtaguso wa Florence wa Mwaka 1437,
lakini maadhimisho yote haya hayakuweza kuzaa matunda ya umoja wa Kanisa.
Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatikani,
wakaamua kuivalia njuga changamoto ya majadiliano ya kiekumene; dhamana
iliyoendelezwa kwa namna ya pekee na Mtakatifu Yohane XXIII, Mwenyeheri Paulo
VI, Yohane Paulo II, Benedikto XVI na kwa sasa kasi ya majadiliano ya kiekumene
imeongezeka zaidi chini ya uongozi wa Baba Mtakatifu Fransisko.
“Kwa namna ya pekee kabisa, Jimbo Kuu Katoliki
Tabora lilihamasika kwa maneno ya Mtakatifu Yohane Paulo II wakati wa
maadhimisho ya Jubilei Kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo aliyelitaka Kanisa kuwa ni
chombo cha msamaha, haki, amani na upatanisho, ili kuponya dhambi na madonda ya
utengano miongoni mwa Wakristo, ili kweli maadhimisho ya Millenia ya tatu ya
Ukristo yaweze kuwa ni chachu ya msamaha, upatanisho na umoja wa Kanisa.
Hii ni changamoto pia iliyokuwa
imefanyiwa kazi na Mababa wa Sinodi ya kwanza ya Afrika na hatimaye, Papa
Yohane Paulo II akachapisha Wosia wa Kitume, Kanisa Barani Afrika, “Ecclesia in
Africa” akiitaka Familia ya Mungu Barani Afrika kujikita katika Uenezaji wa
Injili unaofumbatwa katika utamadunisho, majadiliano na mchakato wa maendeleo
endelevu ya binadamu: kiroho na kimwili, daima Kanisa likiwa ni sauti ya
wanyonge,” amesema.
Jimbo Kuu Katoliki Tabora linaendelea
kutekeleza maazimio ya Sinodi ya kwanza ya Jimbo masuala mbali mbali yaliyobainishwa
katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene.
Hii ikiwa ni pamoja na kushiriki katika
Juma la Sala kwa ajili ya Kuombea Umoja wa Wakristo, kuanzia tarehe 18 - 25
Januari, wakati wa maadhimisho ya Siku kuu ya Kuongoka kwa Mtakatifu Paulo,
Mwalimu na mtume wa mataifa. Lengo ni kuwajengea waamini uwezo ili kweli waweze
kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu sanjari na kuongeza ushirikiano
na mshikamano katika medani mbali mbali za maisha.
Pia amebainisha kuwa, Jimbo kuu la Tabora
limejiwekea utamaduni wa kusali pamoja na Wakristo wa Madhehebu mbalimbali
wakati wa Jumatatu ya Pasaka na Siku kuu ya Noeli, ili kuweza kuimarisha imani,
mwingiliano katika maisha ya ndoa na familia, ili familia ziweze kushiriki kikamailifu
katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa kwa kufuata taratibu, kanuni na sheria
zilizowekwa na Mama Kanisa.
Hii pia ni dhamana ya kuimarisha ushiriki
wa wazazi katika malezi na makuzi ya watoto wao kadiri kanuni msingi, maadili
na mwanga wa Injili.
Wnistimit-ho Tom Proulx click here
ReplyDeletekingtasfaestan