Sinodi ya Maaskofu kwa vijana kufanyika 2018
MAADHIMISHO
ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana yanatarajiwa kufanyika Oktoba 2018 na
kuongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na mang’amuzi ya Miito”. Maandalizi ya
sinodi hiyo yameanza kwa Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu kutoa Hati ya
Maandalizi ya Sinodi ya XV ya Maaskofu kwa ajili ya vijana. Hati hiyo inatoa
mwaliko wa kumfuata Yohane, mwanafunzi aliyependwa zaidi na Yesu.
Hati hiyo pia inaangalia hali ya
vijana duniani: utambulisho na ushiriki wao, mambo rejea binafsi na taasisi
pamoja na mchakato wa kuunda vijana wa kizazi kipya wanaoshikamana zaidi. Sura
ya pili ya hati hiyo inajikita katika imani, mang’amuzi na wito kwa kuzingatia
umuhimu wa imani na wito katika maisha ya vijana; zawadi ya kufanya mang’amuzi
ya miito ili kutambua, kutafsiri na kuchukua maamuzi ya maisha.
Sura ya tatu inapembua kwa kina
shughuli za kichungaji kuhusu miito kwa kuwataka viongozi wa Kanisa kufanya
hija na vijana katika maisha yao, ili hatimaye waweze kutoka, kuona na kuitikia
wito wa kumfuata Kristo Yesu. Walengwa wakuu ni vijana wote bila ya ubaguzi;
Jumuiya inayojihusisha na malezi ya miito pamoja na kuwa na watu ambao ni mfano
bora wa kuigwa.
Shughuli za kichungaji kwa ajili
ya miito zinatekelezwa katika maisha ya kila siku sanjari na ushiriki mkamilifu
katika masuala ya kijamii. Hati inachambua maeneo maalum ya shughuli za
kichungaji bila kusahau ulimwengu wa mitandao ya kijamii, ambamo vijana wengi
wanapenda kuogelea huko.
Mwishoni, Hati hii inamwangalia
Bikira Maria aliyehifadhi, akatafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika
maisha yake, ili aweze kuwasindikiza vijana katika safari ya maisha ya miito
yao. Kuna maswali dodoso yatakayosaidia kuandaa Hati ya Kutendea Kazi, maarufu
kama “Instrumentum Laboris”, kwa kuangalia hali ya kila bara. Namna ya
kukusanya takwimu, kuzitafsiri na kuzifanyia kazi.
Hati yenyewe
Katika utangulizi wake, Hati
ya Maandalizi ya Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, inatoa
mwaliko kwa vijana wote ili waweze kupata utimilifu wa furaha ya maisha, kwani
Kanisa limekabidhiwa dhamana ya kutangaza na kushuhudia Furaha ya Injili.
Huu ni mwaliko wa kuwasaidia
vijana ili kupata mang’amuzi kuhusu miito mbali mbali ndani ya Kanisa kama:
watu wa ndoa, watawa na mapadri, ili kwa njia ya mwanga wa imani, wawe tayari
kushuhudia utimilifu wa furaha katika miito yao.
Sura ya kwanza:
Hali ya Vijana Duniani! Sura hii inapembua hali ya vijana duniani ili kugusa
undani wa maisha ya vijana kimaadili na kiroho, tayari kufanya mang’amuzi ya
maisha na wito wao. Kuna hali ya kutojaliana, idadi ndogo ya watoto
wanaozaliwa; tamaduni na mapokeo ya imani ya Kanisa toka nchi moja hadi nchi
nyingine.
Bado kuna ubaguzi kati ya watoto
wa kike na kiume. Vijana wanaojadiliwa ni wale wenye umri kati ya miaka 16- 29
lakini pia umri huu unategemea na mahali walipo vijana.
Dunia inabadilika kwa kasi kubwa
jambo ambalo linahitaji kuwa na sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa
muda mrefu. Hii inatokana na ukweli kwamba, kuna idadi kubwa ya vijana ambao
hawana fursa za ajira; kuna athari za mabadiliko ya tabianchi; wimbi kubwa la
wakimbizi na wahamiaji lakini pia wapo vijana wachache wanaofaidika na
ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Pamoja na maendeleo yote haya
lakini kuna vijana wengi bado wanajikuta wakiwa wametumbukia katika upweke hasi
na hali ya kukata tamaa kutokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na
mahangaiko ya watu. Rasilimali ya dunia inatumika kwa ajili ya mahitaji ya watu
wachache na kwamba, kuna uharibifu mkubwa wa mazingira hali inayotishia usalama
na maisha ya kizazi kijacho!
Sura ya pili: Imani,
Mang’amuzi na Miito. Mama Kanisa katika mchakato wa maadhimisho ya
Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana anataka kukutana, kuwasindikiza na
kuwasaidia vijana bila ubaguzi ili kweli vijana waweze kupata utimilifu wa
maisha kwa kutambua kwamba maisha na imani ni zawadi ya Mungu.
Ili kuwahudumia vyema vijana,
anasema Baba Mtakatifu Fransisko kunahitajika wema, upole na majitoleo ya dhati
kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Yosefu, mtu mwenye haki, jasiri na mchapakazi;
aliyeonesha huruma na upendo. Kuna uhusiano wa pekee kati ya imani na
wito, kwani hapa vijana wanajisikia kupendwa na kuthaminiwa.
Imani inawasaidia vijana kujenga
na kudumisha umoja, udugu na mshikamano wa dhati, tayari kushuhudia tunu msingi
za maisha ya kiroho na kiutu, matokeo ya majadiliano ya kina katika dhamiri
nyofu. Wito na mwaliko kutoka kwa Kristo Yesu, umesheheni furaha na majitoleo
ya dhati ambayo yanapaswa kutakaswa, kuwekwa huru ili kutambua jambo jema na
kulitenda.
Vijana wanapaswa kufanya maamuzi
magumu katika maisha yao, kwa kusoma alama za nyakati na kutambua uwepo wa Roho
Mtakatifu katika historia; kwa kung’amua kilicho chema na kukifuata, ili kupata
utimilifu wa maisha. Mkazo ni kutambua, kutafsiri na kuchagua kile ambacho
Mwenyezi Mungu anataka katika maisha ya kijana.
Sura ya Tatu:
Mikakati ya shughuli za kichungaji: Sera na mikakati ya shughuli za kichungaji
kwa vijana inapaswa kujielekeza mahali waliko vijana katika maisha yao ya kila
siku, ili kuwasaidia kujenga historia ya maisha yao. Yesu apewe nafasi ya
kuweza kutembea na vijana hatua kwa hatua ili aweze kusimama na kuwaangalia kwa
jicho lenye huruma na upendo, ili kwa kufunga safari na vijana, Jumuiya nzima
ya waamini iweze kujengwa na kuimarishwa.
Vijana wapewe nafasi ya kuonesha
na kushirikisha kipaji chao cha ugunduzi; kwa kuwa na mwono na mwelekeo mpya na
mpana zaidi katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji.
Hapa, Mama Kanisa anakazia mambo
makuu matatu: kutoka, kuona na kuitwa. Utume kwa vijana ni mchakato unaopaswa
kuwashirikisha vijana wote pasi na ubaguzi kwa kutambua kwamba, Jumuiya ya
waamini nayo inawajibika barabara katika malezi, makuzi na majiundo ya vijana
wa kizazi kipya.
Jambo la msingi ni ushuhuda wenye
mvuto na mashiko kwa vijana kwa kuwashirikisha vijana katika maisha na utume wa
Kanisa. Kanisa linawataka wazazi, walezi na familia; viongozi wa Kanisa pamoja
na walimu kuwa kweli ni mfano bora wa kuigwa na vijana wa kizazi kipya.
Mwishoni, Hati
ya Maandalizi ya Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana kwa
Mwaka 2018 inatoa maswali dodoso ya jinsi ya kukusanya takwimu; kusoma na
kutafasiri takwimu za vijana wanaohudhuria maeneo ya Kanisa, wale ambao wako
nje au wale wanaojisikia kuwa ni wageni kabisa katika maeneo ya Kanisa.
Maswali ya utume kwa vijana
kuhusu miito; walezi na waalimu na mwishoni maswali msingi kwa kila bara pamoja
na kushirikisha wengine takwimu zilizopatikana yamekaziwa kwa wote.
Comments
Post a Comment