Maneno “uchawi” au “mchawi” kwa dhana za kiafrika hayastahili kuwamo kwenye Biblia
KATIKA kutolea maoni kibwagizo changu cha jana cha “WOTE KIMYAA!!”,
mwenzetu Deonatus F. N. Mutani ametaka kutuchanganya sote. Mimi nawatafuta
“wachawi” au “watu wenye uchawi” wanyeshe mvua siku hizi tupone. Nataka
wajitokeze tuone. Nataka wajitokeze hadharani watende kitu cha kutufaa sote.
Nimekataa uwapo wa uchawi na
wachawi kati yetu. Tulionao ni wababaishaji na watu tunaowatuhumu kwa
kuwasengenyasengenya tu. Wachawi kiukweli hawapo na bado ninawatafuta. Ninataka
wajitokeze na nimesema kama kuna anayewajua awataje, atuitie au atuoneshe
wenzake. Mwenzetu Deonatus Mutani ametoka huko niliko na kusema eti Biblia
inakiri kuwapo kwa uchawi na wachawi.
Ndipo amenishangaa mimi ni padre
wa aina gani kukataa uwepo wa uchawi ambao kwa kadiri yake unashuhudiwa na
Biblia yake.
Sawa. Lakini leo hii tukimuuliza mwenzetu huyu Biblia gani hiyo, bila shaka atasema ni Biblia ya Kiswahili au ya Kiingereza fulani. Kumbe, hapo ndipo atakapokosea na ndipo panaponipa mimi fursa ya kutoa somo la lugha asilia za Biblia, japo kwa ufupi tu.
Nisikilizeni vijana na wasomaji wangu.
Ni hivi, kwenye Biblia hakuna
hata mahali pamoja palipoandikwa kwa Kiswahili neno “mchawi” au “uchawi” kwa
mastahili. Biblia za Kiswahili zimetutumbukizia maneno hayo pasipo simile.
Maneno hayo yaliyotumbukia humo hayabebi maana na dhana halisi ya kilichosemwa
katika lugha asilia za Kiebrania au Kigiriki. Dhana ya Kiafrika juu ya “uchawi”
na “wachawi” haiingii kwenye Biblia hata kidogo.
Nina hoja. Nadhani mnaweza
kukubaliana nami kwamba katika makabila yetu dhana au fasili ya uchawi si
nyepesi. Ni dhana mtambuka. Dhana au fasili yetu ya “wachawi” ni ya watu wenye
nguvu za ajabu za kufanyia mambo ya ajabu kama tunavyosema wenyewe, labda
kuruka angani kwa nyungo, fisi, mbweha, pembe au mikeka;
kunyesha mvua hata kiangazi;
kupiga radi wapendavyo; kuingia majumbani mwa watu kwa kupitia milango na hata
madirisha yaliyofungwa, kuroga tokea mbali, kutazama na kudhuru watu kwa macho
au kauli, kuwabadili watu wakawa labda mainzi, nyoka au ngedere na kadhalika.
Orodha ni ndefu mno. Kwa lugha yenu vijana, “orodha ni ndefu kishenzi!”.
Ndipo kwetu sisi “wachawi” ni
watu wenye uwezo wa kuwatoa wafu makaburini na kuwala nyama maiti; wenye uwezo
wa kufanya mikutano usiku pasipo watu wengine kuwaona; watu wenye kuwatengeneza
na kuwatunza watu kama misukule; watu wenye uwezo wa kuroga wengine kutoka
mbali; watu wasioweza kuonekana wanapofanya shughuli zao; watu wenye kutembea
usiku uchi wa mnyama; watu wanaoweza wakawatazama watu kwa macho ya aina yake
wakadhurika vibaya; watu wanaoweza kuwasemea wenzao maneno ya laana au mikosi
wakadhurika na kadhalika.
Naomba maweza mengine muyaongezee wenyewe maana, bila mashaka, kwenu dhana hii ipo nanyi, kama humwamini wenyewe, walau mmesikia habari zake. Zaidi sana, imani hiyo mnaijua ilivyotuganda Waafrika wengi kiasi cha Baba Mtakatifu Benedikto XVI kutuonea huruma katika mausia yake Africae Munus namba 93 yaliyoelekezwa kwa Waafrika wote pale mwaka 2009 kufuatia Sinodi ya Pili ya Afrika.
Aghalabu, mnajua jinsi
tunavyodhuriana katika jamii zetu, kujichonganisha, kupoteza muda na pesa
nyingi, kwa shughuli za jamaa kushikana na kwenda “kunyoana” kwa waganga wa
kienyeji; watu kuwaalika “akina Lambalamba” na “kusafisha vijiji” vyao; watoto
kuwatuhumu na kuwaua wazazi wao; wanavijiji kubomoleana nyumba au kuchomeana
moto wakifukuzana kwa ukatili mkubwa;
Watu kuwaua vikongwe na wazee;
watu kuwafukuzia watuhumiwa wao kwenye vijiji vya wachawi; watu kuwapiga na
kuwachomea wengine nyumba moto au kuwaharibia mazao na mali zao wakidaiwa
kuzuia mvua; timu zetu za michezo kutumia pesa nyingi kulipia “mabenchi ya
ufundi” yaani waganga wa kienyeji; wachezaji wetu kupewa masharti magumu au
kulazwa makaburini kabla ya mechi; watu kuzindika nyumba zao kwa hirizi;
Watu kuwaua au kuwadhuru albino
wakitafuta viungo vyao wapate vyeo na utajiri; watu kutafuta mifupa na mafuvu
ya binadamu kwa ajili ya kuboreshea biashara au ajira zao; akina mama kuuawa
kwa sababu ya sehemu zao za siri; watu kunyofolewa macho, ndimi na masikio;
watu kutafuta, kuchukua na kuvaa hiziri na kadhalika.
Sina mashaka, haya yote mnayajua; imani na vitendo vilivyoipa Tanzania nafasi ya kwanza Afrika katika kuamini uchawi, kwa kadiri ya utafiti wa mwaka 2009 wa PEW Research Centre ya Washington D.C., Marekani. Lakini habari ngeni kwenu nyote ni hii kwamba Biblia haina dhana hiyo, hata chembe na hakuna panapostahili kutokea neno “uchawi” au “mchawi” ndani yake. Maneno hayo yanatokea isivyostahili.
Msishtuke. Ndipo hapo hapo ninapojaribu kulitangaza jambo hili pasipo kusadikika. Wengi wananishangaa sana. Lakini si kitu nimeunda jeshi la mtu mmoja! Hata ndugu yetu Deonatus Mutani ananishangaa sana. Kumbe, nguvu ya hoja yangu ni lugha asilia zilizotumika kuandikia Biblia. Nawahakikishieni nyote kwamba dhana yetu ya uchawi na wachawi haimo kwenye Biblia maana maneno yote asilia yaliyotumika humo hayana MAANA ZETU.
Msinibishe. Nendeni kwenye lugha asilia Kiebrania (Agano la Kale) na Kigiriki (Agano Jipya).
Biblia katika lugha zake asilia
hazina maneno yenye maana zetu. Ndiyo maana nakataa kwa nguvu na kwa kujiamini
kabisa. Tafsiri za Kiswahili na Kiingereza zinatupotosha. Kwa bahati njema
baadhi ya watafsiri wa nakala za Kiingereza wamejitahidi sana ama kuepuka au
kutumia kiusahihi maneno: “witchcraft”, “sorcery” na “magic”. Katika Kiswahili
tuna maksi ya karibu sefuri.
Tusiandikie mate, wino ungalipo. Hebu tuthubutu kujitengea muda siku fulani tujisomee na kutafakari kwa utulivu sehemu zifuatazo: Mwa 41:8.21, 1Sam 28:7, Kut 7:11.22, 8:7.18.19, 9:11, Law 19:26, Kum 18:10-11, Isa 3:3, 47:9.12, Dan 1:20, 2:2.10.27, Nah 3:4, Mdo 13:6.8, 19:19, Gal 5:20 na Ufu 22:15. Hizi ndizo sehemu maarufu kwa maneno “uchawi”, “mchawi” au “wachawi”.
Zatupasa kuzichambua kwa makini.
Maneno yametumika kwa kupwaya mno.
Nawahakikishieni tena kwamba tukizitalii sehemu hizi katika lugha zake asilia, hatutapata maana ya wachawi katika dhana ya Kiafrika isipokuwa mojawapo ya maana hizi:
Nawahakikishieni tena kwamba tukizitalii sehemu hizi katika lugha zake asilia, hatutapata maana ya wachawi katika dhana ya Kiafrika isipokuwa mojawapo ya maana hizi:
mabingwa wa kutumia visivyo
utaalamu mbalimbali, wachanganya madawa, wacheza mazingaombwe, watu wenye
kuwatinga wenzao kwa utaalamu, wataalamu wa nyota, watabiri, wapiga ramili,
waona maono, watu wanaotafuta ushauri wa wafu au mapepo, watafsiri ndoto na
kadhalika.
Maana hizi ndizo zilipaswa kuchaguliwa vyema na waliotutafsiria Biblia katika Kiswahili zamani zile. Kumbe, wote waliotajwa hivyo, kwenye Biblia, kwa Wayahudi, walikuwa wataalamu waliokuwa wanajulikana na watu na utaalamu wao uliwekwa kwenye vitabu vyenye kusomeka bayana (rej. Mdo 19:19).
Swali halali ni “Kama uchawi unataja zaidi utaalamu
fulani, inakuwaje Biblia inasema “wachawi wauawe” au hawataingia mbinguni, kwa
mfano Gal 5:19-20 na Ufu 22:15? Jibu ni
rahisi, wataalamu (“wachawi”), iwe kwa
maana ya waona maono, wachanganya dawa, wataalamu wa nyota, wacheza mazingaombe
na kadhalika, wakipitiliza maana nzuri ya utaalamu wao na kuanza kubabaisha
watu wengine wanaingia katika eneo la dhambi na hapo ndipo wanapostahilisha
adhabu kali.
Kwa mfano, mchanganya madawa
akichanganya dawa zake kiasi cha kuwalewesha watu kudhuru afya zao na kuwafanya
wabwate bwate na kukiri mambo yasiyojuzu
(kwa mfano kwa kupewa ketamini), atenda dhambi kubwa naye anajistahilisha
adhabu kubwa. Ndivyo inavyoweza kuwa katika mambo yote. Kuchinja kuku si
dhambi, lakini anayetumia ujuzi na wepesi wake wa kuchinja kuku kuchinja watoto
wa watu, afanya dhambi naye astahili kutupwa motoni. Udreva si dhambi, lakini
dreva anayeendesha gari na kuwaponda watu barabarani afanya kosa kubwa naye
anastahili asiingie mbinguni.
Anayepiga dawa ya usingizi ili
watu wafanyiwe operesheni (nusu kaputi), anafanya kazi iliyotukuka. Lakini mtu
huyo huyo akiwatia watu dawa kwa kuwalipa kisasi ili wafe watakapofanyiwa
operesheni afanya dhambi naye astahili kutupwa motoni na kadhalika. Ndipo kumbe
ilipostahili, katika tafsiri, kuchagua sana maneno ya kutumia badala ya
kutafsiri sehemu zote kwa neno kumbakumba “uchawi”.
Maana yake ilitakiwa kuwa makini
sana kwa sababu hata kama vitu vinafanana majina vinaweza kutofautiana. Ndiyo
kisa kuna “paa” na “paa” na kuna “kaa” na “kaa”. Kifupi, ilipasa kuainisha na
kupembua aya kabla ya kulitumbukiza neno uchawi kila mahali. Unakwazika kwa
haya ninayosema? Usikwazike. Nakujulisha.
Huu ndiyo utaalamu wa tafsiri
unaosomewa katika vyuo vya kutafsiri Biblia katika Kanisa Katoliki, kwa mfano
Biblicum, Roma. Neno la Mungu (Biblia) kwetu sisi Wakatoliki ni uwanja wa
utaalamu na si dhambi kuchunguza mambo kiasi cha kitaalamu. Kanisa Katoliki si
kanisa la wakariri Biblia tu, ni Kanisa la waelewa Biblia.
Ndipo, basi, tusidanganyike tukachukua dhana yetu ya uchawi ya Kiafrika tukaiingiza kwenye Biblia takatifu. Tutakuwa waongo na wakufi wa weledi. Narudia na kusisitiza kwamba katika Biblia hicho kinachotafsiriwa kama “uchawi” kilikuwa aina ya elimu au utaalamu. Ndiyo maana kulikuwa na vitabu vyake kama nilivyosema sasa hivi (rej. Mdo 19:19) na watu wenye elimu hiyo walikuwa wakijulikana na wengine.
Wataalamu wenyewe hawakumwonea
mtu yoyote haya na wala hawakujificha. Ndiyo maana waliwahi kuitwa na Farao
wakatokea barazani (Kut 7:11) na waliwahi kuitwa na mfalme Nebukadneza huko
Babiloni wakajumuika na wataalamu wengine (rej. Dan 2:2). Hali kadhalika tazama
jinsi Simeoni “mcheza mazingaombwe” alivyokuwa anajulikana na watu (rej. Mdo
13:6.8).
Asante sana uchawi haupo ni matapeli tu na wafanya mazingombwe, eti mtu apae angani kwa ungo?? Never on earth
ReplyDelete