Enyi watunzi, muziki mtakatifu ni sala!

Mtawajibika kwa kupoteza hadhi ya muziki mtakatifu
Na Pascal Mwanache
DHANA ya usasa na mabadiliko imekuja na changamoto ambazo zinadhihirika katika nyanja mbalimbali za maisha ya mwanadamu. Licha ya kuleta tija kwa jamii, maendeleo ya sayansi na teknolojia, ambayo yanachochea kwa kasi sana dhana za usasa na mabadiliko, kwayo athari kadhaa zinaendelea kujitokeza.
Muziki Mtakatifu wa Kanisa Katoliki unalenga kumsaidia muumini kusali vizuri, kumuingiza katika tafakari na sala, ili basi Mungu atukuzwe na mwanadamu atakatifuzwe. Hili ndilo lengo msingi la uwepo wa muziki mtakatifu katika maadhimisho ya Misa Takatifu.
Katika siku za hivi karibuni, kumeibuka wimbi la watunzi wengi ambao, aidha kwa kutojua (ignorance), au kwa makusudi kabisa, wanafanya mambo ambayo yanatia doa hadhi ya muziki mtakatifu. Wanafanya mambo (katika utunzi wao) ambayo hayatarajiwi yafanywe katika muziki mtakatifu. Hii siyo tu inastaajabisha, bali pia inawakwaza waamini na watu wenye mapenzi mema.
Swali linalojirudia katika vichwa vya wengi ni ‘Endapo kama watunzi waliotangulia, kama vile Padri Ntapambata, Felician Nyundo, John Mgandu, Padri Thomas Eriyo, Padri Kayetta, Mzee Kashumba, Mwarabu, Makoye, Kalolela, Mujwahuki nk, wangelikiuka utunzi wenye tija ndani ya kanisa, watunzi wachanga, waamini na kanisa kwa ujumla lingerithi nini?”
Ndiyo maana basi nikatangulia kusema kuwa, pengine watunzi hawa wachanga, wanafanya mambo yasiyotarajiwa kwa sababu wamekosa elimu ya teolojia, elimu sahihi ya utunzi na mang’amuzi ya kutosha katika kutunga nyimbo za Kanisa Katoliki. Kwa sababu hiyo, katika makala haya, nashawishika kutoa baadhi ya kero zinazowakabili na namna wanavyoweza kuziepuka, kama ifuatavyo:
Kubinafsisha utunzi
Kadiri ya kamusi ya Kiswahili sanifu (TUKI), ubinafsishaji ni hali ya kufanya mali ya umma kuwa ya binafsi. Hali hii inaweza kuwa na manufaa kwa umma au kuleta athari pia, kutegemea na lengo la ubinafsishaji huo. Kwa watunzi wetu, malalamiko yanayoelekezwa kwao ni kuleta mitindo ya utunzi, ufundishaji na uimbaji ambayo haiendani na hadhi ya muziki mtakatifu.
Kadhalika ubinafsishaji huo hauna lengo la kuwafanywa waamini wasali vizuri, bali hukusudia kujitengenea utambulisho wa mtunzi (identity), kukuza biashara na hatimaye kujiongezea kipato. Katika hali hii, watunzi wenye tabia hizi hujisahau na kujikuta wakienda kinyume na matarajio ya waamini. Ndiyo maana tunashuhudia kwaya zikiimba nyimbo ambazo hazina hadhi kuimbwa katika maadhimisho ya Liturujia.
Tunashuhudia nyimbo hizo zinazohamasisha kucheza kwa mitindo mbalimbali zikigeuza kwaya kuwa kikundi cha maonesho. Hapo utasikia watu wakiimba kwa sauti za ajabu kana kwamba wanataka kutapika. Na lengo la mtunzi linafanikiwa pale mitindo ya namna hiyo inapoigwa na kwaya kutoka maeneo mbalimbali nchini, hatimaye mitindo hiyo husambaa na kufifisha uchaji na hali ya sala.
“Utaratibu wa Liturujia ni wa kanisa zima siyo wa mtu binafsi. Je mnatunga nyimbo mkiwa katika hali gani, mnaongozwa na roho ya sala? Mazingira ya utunzi yakoje, ni wapi tunatungia nyimbo zetu?” aliwahi kuhoji Askofu Salutaris Libena wa Jimbo Katoliki Ifakara, na Mwenyekiti wa Idara ya Liturujia ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania TEC.
Kukosa elimu ya teolojia kwa watunzi
Watunzi wengi wachanga wanaoibuka kila kukicha wana uelewa mdogo wa teolojia. Wengi hawakuandaliwa kuwa watunzi katika taasisi za kanisa kama vile seminari, nyumba za malezi au vyuo vya dini. Hujifunza katika mazingira yasiyo rasmi. Siyo jambo baya kujifunza muziki katika mazingira yasiyo rasmi, ila kufanya yasiyostahili huleta makwazo.
Ndiyo maana basi mababa wa Mtaguso Mkuu II wa Vatikani wakatoa agizo kuwa elimu ya muziki ifundishwe katika seminari, shule na vyuo vya kikatoliki.
Jitihada kubwa ifanyike ili kuhamasisha elimu na mazoezi ya muziki katika seminari, katika nyumba za unovisi za mashirika ya kiume na ya kike, katika nyumba za wanafunzi, kama vile vyuo na shule za kikatoliki; ili kupata elimu hii, walimu waandaliwe kwa bidii kubwa, kisha watumwe kufundisha muziki mtakatifu.   Ikiwa inafaa, uundaji wa Taasisi za Juu za muziki mtakatifu uhimizwe” (SC 115) .
Aidha kwa watunzi ambao hawana elimu ya teolojia, wafanye bidii kuelewa kanuni za utunzi wa muziki mtakatifu, hasa unaotumika katika maadhimisho ya liturujia.
“Ukitaka kufanikiwa katika utunzi wako tumia Biblia Takatifu. Tusibadili asili ya muziki wetu kwani ni wa thamani kubwa. Kuna mwelekeo wa kuvutwa na matamanio ya watu na maneno mapya yanayoibuka kila siku mtaani. Tukumbuke kuwa hatupo kwa ajili ya kuwaridhisha watu, haya siyo maonesho, siyo burudani, muziki ni sala” anaeleza Padri Peter Msafiri, Mkufunzi wa Liturujia katika Seminari Kuu ya Segerea.
Utunzi wa nyimbo za mitaani
“Malengo ya Muziki Mtakatifu ni kuwasaidia waamini katika mawazo, maneno, matendo na maisha ya kila siku ili waweze kuzama katika mahusiano yao na Mungu. Ni utekelezaji wa kazi ya ukuhani wa Kristo, hivyo utunzi unalenga kuendeleza na kutekeleza kazi ya ukuhani wa Kristo” Anaeleza Askofu Libena.
Siku hizi siyo ajabu kusikia nyimbo za Kanisa Katoliki zikiimbwa katika melodia, maneno, mtindo unaoshabihiana sana na nyimbo za bongo fleva ama zile za kilokole. Wenyewe wanasema wanakwenda na wakati. Na hili linajitokeza zaidi katika nyimbo zilizorekodiwa.
Baada ya kazi ya kurekodi, inafuata kazi ya uhariri ambapo hufanyika pia ‘mixing’. Shughuli nzima ya kuharibu hadhi na urithi wa muziki mtakatifu hufanyika hapo. Ndiyo maana siku hizi ni vigumu kutofautisha nyimbo za Kanisa Katoliki na madhehebu mengine.
Inastaajabisha sana, hapo awali wenzetu walituonea wivu kwa jinsi muziki wetu ulivyokuwa na upekee na hadhi yenye kudumu, Lakini leo hii watunzi wetu wanawaonea wivu walokole na hivyo kuiga utunzi na uimbaji wao. Mifano ya watunzi na kwaya zilizorekodi nyimbo mithili ya nyimbo za walokole ipo. Tena katika utafiti wangu mdogo nimebaini kuwa watunzi hao wakishatunga basi huitwa na kwaya husika wakafanye ‘mixing’ huko studio.
Enyi watunzi wa namna hii, mtawajibika kwa kuua hadhi ya muziki mtakatifu na kufifisha ari ya uchaji na sala kwa waamini. Ni vema sasa mkasoma, mkaelewa na kufuata miongozo ya kiliturujia, na kuzingatia nyimbo zinazokubalika.
“Tathmini ya muziki imebaini pia baadhi ya watunzi chipukizi hutumia maneno ya mitaani wanapotunga nyimbo za kiliturujia wakidhani kufanya hivyo ni kuwavuta waamini katika uimbaji. Mfano ni nyimbo zenye maneno, Nimevunja mkataba na shetani, gari la shetani limepata pancha, zikatiririka, kidole juu, lipua puu puu…” anaeleza Padri Patern Mangi.
 “Liturujia yetu inapaswa iwavute watu wamwendee Kristo, vinginevyo wakristo watahama Kanisa letu na kwenda madhehebu mengine wanayodhani Kristo atagusa maisha yao” Askofu Libena (kiongozi, Mei 22-28, 2015. P 3)
Ibada lazima iwe na utulivu. Hivyo hata uimbaji pia uwe na utulivu ndani yake. Mababa wa Mtaguso wanahimiza juu ya unyamavu wakati wa Misa Takatifu. Wanasema hivi “Ili kuwawezesha waamini washiriki kimatendo, mashangilio ya waamini, viitikio, kuimba zaburi, antifona, nyimbo, vitendo, ishara na mkao wa mwili vitiliwe maanani. Unyamavu Mtakatifu utumike pia, wakati unapodaiwa” Ibara n.30).
Itaendelea

Maoni: 0657835343

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI