Mashemasi waige mfano wa mamajusi
Askofu Mkuu wa Jimbo
Kuu Katoliki Tabora Mhashamu Paul Ruzoka amewaasa mashemasi na waamini kumpenda
Kristo zaidi na kuwa tayari kupeleka Imani ya Kikristo kwa watu wote katika
maisha yao pendwa kwa Mungu.
Askofu Mkuu Ruzoka amesema
hayo wakati wa adhimisho la Misa Takatifu katika Kanisa la Kiaskofu Tabora
wakati wa sherehe ya tokeo la Bwana.
Akitoa mahubiri yake
kwa wana jimbo na waamini toka majimbo jirani ambayo baadhi ya mashemasi hao
wanatoka, Askofu Mkuu Ruzoka amesema kuwa Mamajusi walitoka sehemu mbalimbali
tofauti na bila kutaarifiana na kujikuta wanakutana Bethlehemu kumsujudia na
kumwabudu Mwokozi hivyo imani iliwakutanisha.
Aidha Askofu Mkuu Ruzoka
amesema imani peke yake ndiyo kitu kilichowafanya Mamajusi hao wavumilie tabu
na changamoto walizokutana nazo safarini bila kukata tamaa, bila imani safari
yao isingekuwa na mafanikio.
Mashemasi Ignas
Akilimali, Francis Kiguli na Fabian Mkama wamefananishwa na Mamajusi ambao
baada ya kufika Bethlehemu na kutoa zawadi zao yaani dhahabu, uvumba na manemane
walirudi kwa njia nyingine ambapo mashemasi hao walianza safari yao ya malezi
kwa njia ya kawaida toka makwao, lakini baada ya kuwa mashemasi wanaanza maisha
ya Useja yaani wanaanza safari kwa njia nyingine tofauti na ile waliyokuja nayo
awali.
Aidha amesema jamii
kwa kawaida inaelewa na kuzoea kuona kijana akifikia umri fulani hana budi
kutafuta mwenzi wake na kufunga ndoa kanisani ambapo nderemo na vigelegele
hutawala, ila kwa hawa vijana haitakuwa hivyo.
"Mashemasi
mnapaswa kumpenda sana Kristo na kujitoa kwake kimwili na kiroho ili awatumie
kwa ajili ya kuwapeleka watu kwa Kristo, aliye njia ya ukweli na uzima,"
Askofu Mkuu Ruzoka amesema.
“Kama tunavyosoma,
Mamajusi hawa baada ya kumuona mtoto na kutoa zawadi zao walirudi makwao na
kitu fulani walichokuwa wamepata na kuwa tayari kukipeleka kwa wale waliokutana
nao, hivyo basi mashemasi pelekeni habari njema kwa watu wote yaani uwepo wa
Kristo katika ulimwengu wa leo.”
Amewatia moyo mashemasi
hao na kuwaomba kuwa na moyo mkuu wa kuvumilia changamoto ambazo wanaweza kukutana
nazo katika kutekeleza majukumu yao.
“Mamajusi walisikia
na kupokea mpango wa Mungu katika ndoto na hawa vijana wanapaswa kuzingatia
malezi waliyoyapata wakati wote walipokuwa wanafundwa katika nyumba za
malezi.(seminari zao).”
Jimbo Kuu Katoliki Tabora
linatarajia kupata mashemasi wengine mapema mwezi Machi mwaka huu ambapo wito
umetolewa wa kuendelea kuwaombea mashemasi hao ili wafanye yote kwa ajili
ya sifa na utukufu wa Mwenyezi Mungu.
Comments
Post a Comment