Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo 2017: Muda wa Upatanisho!
Wakristo sehemu mbali mbali za dunia kuanzia tarehe 18 Januari hadi tarehe 25 Januari, Siku kuu ya kuongoka kwa Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa watakuwa wanaombea umoja wa Wakristo. Kauli mbiu ya mwaka 2017 ni “Upatanisho: Upendo wa Kristo unatuwajibisha”. Haya ni maneno yaliyotolewa kutoka katika Waraka wa Pili wa Mtume Paulo kwa Wakorintho yanayowabidisha Wakristo kuendeleza majadiliano ya Uekumene wa sala na maisha ya kiroho; tayari kujipatanisha ili kumshuhudia Kristo Yesu kwa njia ya huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. (Rej. 2 Wakr. 5:14- 20).
Juma la kuombea Umoja wa Wakristo linaandaliwa na Baraza la Kipapa la kuhamasisha Umoja wa Wakristo kwa kushirikiana na Baraza la Makanisa Ulimwenguni. Maadhimisho ya Mwaka 2017 yameandaliwa na wajumbe wa Makanisa kutoka nchini Ujerumani wanaoendelea kuadhimisha Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani, yaliyoanza kutimia vumbi tarehe 31 Oktoba 2016 kwa uwepo na ushiriki wa Baba Mtakatifu Francisko huko Lund, nchini Sweden.
Makanisa ya Kikristo nchini Ujerumani yameamua kumsherehekea Kristo katika siku kuu maarufu inayojulikana kwa lugha ya Kijerumani “Christusfest” Sherehe ya kiekumene inayowaunganisha Wakristo wote ili kumshuhudia Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Kumbu kumbu ya Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani ni tukio endelevu kwani Wakristo wanakumbushwa kwamba, wamekombolewa kwa njia ya neema na imani kwa Kristo Yesu. Kumbe, Wakristo wanapaswa kufurahia zawadi ya ukombozi waliopatiwa na Mwenyezi Mungu kwa njia ya Fumbo la Msalaba yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu; Fumbo ambalo linavuka mipaka ya kinzani na migawanyiko miongoni mwa Wakristo, kiasi cha kuwakusanya pamoja, tayari kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa zawadi ya Ukombozi. Maadhimisho haya yanawapatia Wakristo ujasiri wa kuweza kuungama hadharani dhambi ya vita, kinzani na utengano miongoni mwa Wakristo uliofuatia baada ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani, yapata miaka 500 iliyopita.
Wakristo kwa pamoja wanataka kusema, “yaliyopita si ndwele, tugange yaliyopo na yale yajayo” kwa kuombana msamaha, kwani upendo wa Kristo unawabidisha, kiasi kwamba, nyoyo za Wakristo zilizogawanyika na kutengana ziweze tena kwa njia ya neema ya Kristo Yesu, kuungana, tayari kuwa mashuhuda na vyombo vya upatanisho. Familia ya Mungu nchini Ujerumani inakumbuka kwamba, kunako mwaka 1989 walishuhudia Ukuta wa Berlin uliowatenganisha na kuwagawa Wajerumani ukianguka na huo ukawa ni mwanzo wa Ujerumani mpya iliyoungana na kushikamana.
Kikundi cha Sala ya Amani, maarufu kama “Peace Prayer Movement” kikaanzishwa na kuanza kutembea nyumba kwa nyumba kikisali na kuwasha mwanga wa mshumaa wa matumaini, mshikamano na dhamana katika ujenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku kuu ya kuongoka kwa Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa, jioni, tarehe 25 Januari 2017 anatarajiwa kuongoza Masifu ya jioni kwa ajili ya kufunga Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Comments
Post a Comment