Eti Wasomi wa Siku hizi hamna kitu: Ni wasomi au mfumo wa elimu umechoka?
JAMII
yetu imewachoka wasomi. Inawasema vibaya! Wasomi hawaheshimiki tena kama
zamani. Eti wasomi wa siku hizi ni hamna kitu. Yaani ni Tabula rasa. Ajabu
sana. Mtu ametumia karibu nusu ya maisha yake akisoma leo anaambulia kuitwa
hamna kitu. Unajua Mungu anawaona?
Kijana mmoja anawatukana walimu
kwamba tunazalisha wasomi vihiyo.
Acha atukane tu maana mdomo ni mali yake. Anayemtukana mwalimu ni dhahiri
hajitambui, maana angejitambua angefahamu kwa nini ualimu ni wito.
Sharti la kuwa mwalimu lazima
ujikane mwenyewe na kuubeba msalaba wa wajinga kwa malipo ya kufedheheshwa na
kudhalauriwa. Ndiyo! Mwanafunzi akifeli
ni uzembe wa mwalimu, akifaulu ni juhudi zake mwenyewe! Na huu ndiyo wito
wenyewe. Asiyekuwa nao hawezi!
Imekuwa fasheni hata
aliyeshindwa shule kumsema ovyo msomi. Ni kutukana tu. Msanii mmoja wa BongoFleva
aliyeishia darasa la nne anasema haoni umuhimu wa elimu kwa sababu kupitia
muziki ana kipato kikubwa kuwashinda waliosoma na bado amewaajiri waliosoma.
Unaibeza elimu, lakini
unawatumia wasomi katika kazi zako. Ni sawa na Chichidodo ndege anayesema
kinyesi ni uchafu lakini anakula minyoo kutoka kwenye kinyesi hicho. Huyu
Msanii ni mpumbavu. Mbona kuna walioacha shule na kukimbilia muziki lakini bado
wanahenya?
Hapa ndiyo utajua kila asemaye
Bwana Asifiwe atakwenda Mbinguni. Mfalme Suleiman hakukosea aliposema, Hata
ukimtwanga mpumbavu kwa mchi kinuni pamoja na ngano, upumbavu wake hautamtoka.
Hata madiwani nao wanasema
wasomi hawana kitu. Maskini ya Mungu. Madiwani wengine hata kusoma na kuandika tu
ni shida, nao wanabeza. Huku kukaririshwa cha kusema, kunadhalilisha watu kwa
kweli. Tembelea Halmashauri uone wakurugenzi wanachofanyiwa na madiwani.
Ni vitisho na amri za kuudhi tu.
Kitendo cha Diwani kumwambia mkurugenzi ni mbabaishaji hivyo afukuzwe kazi ni
muujiza kama ilivyo miujiza mingine. Mbiti anakwambia shida ni kwamba watu
weusi tunatumia hisia na vionjo zaidi ya akili katika kufikiri ndo maana
maajabu hayaishi. Unadhani kwa nini TANESCO imeshindwa kuangaza maisha ya
watanzania wote?
Tatizo, wataalamu wanaelekezwa
nini cha kufanya na wanasiasa. Yaani ni sawa na fundi cherehani akafanye kazi
za upasuaji kwa sababu ana uzoefu mkubwa wa kutumia mkasi. Enyi wajinga, hata
lini mtapenda ujinga?Anauliza Mfalme Suleiman.
Lakini pia wasomi wenye nafasi
zao serikalini na katika sekta binafsi nao wanasema ovyo kuhusu wasomi wa siku
hizi utadhani wao walisomea Mbinguni. Utaskia, vyuo vikuu vya siku hizi vinazalisha
mburula.
Ukiwauliza kwa nini wanasema hivyo,
watakwambia wasomi wa siku hizi hawajui kiingereza. Yaani wao kigezo cha usomi
ni uwezo wa kumudu lugha ya kikoloni. Huu kama si utumwa wa fikra ni nini?
Sasa kuna lugha nyingine za ovyo
kabisa. Eti unaweza kusoma sana lakini maisha yakakupiga. Waliofanikiwa katika
maisha wanajisifia kwamba mafanikio yao hayakutokana na elimu bali juhudi
binafsi. Wanakwenda mbali zaidi na kuiaminisha jamii kwamba kusoma sana ni
kujitafutia umaskini. Wengine wanatoa takwimu za ovyo ovyo kwamba hakuna tajiri
aliyesoma sana utadhani shuleni tunafundisha utajiri.
Kuyaruhusu mawazo ya namna hii
kuendelea kuishi katika jamii ni kuiua jamii. Kwa sababu jamii hiyo itapuuza
elimu na hapo majanga yatatokea. Vyuoni hatufundishi utajiri bali tunafundisha
ustaarabu. Hatuwezi wote kuwa matajiri
lakini wote tunaweza kuwa wastaarabu. Tumekuwa jamii ya kubeza elimu na wasomi
wetu kupitia tungo za kuchekesha, tungo ambazo husambazwa kupitia whatsap kama
sehemu ya burudani.
Eti kuna maprofesa 40 walipanda
Air Tanzania ili wasafari. Kabla ndege haijaanza kuondoka, lilipita tangazo
kama ifuatavyo: Ndugu wasafiri wote, ndege unayotarajia kusafiri nayo
imetengenezwa na wanafunzi wa Kitanzania. Baada ya tangazo maprofesa wote
waliteremka isipokuwa mmoja alibaki kwenye kiti chake.
Walipomuuliza ni kwa nini
hakuondoka akajibu kwa haraka na furaha kuwa: Kama ndege hii imetengenezwa na
watanzania, hata kuwaka haitawaka!” Huku kama siyo kuwafedhehesha wasomi wetu
ni nini? Tungo kama hizi pengine ndiyo husababisha viongozi wetu nao kuwabeza
wasomi. Kiongozi mmoja kauita utafiti uliofanywa na wasomi kwamba ni lamli. Asiye
na akili siku zote humbeza mwenzake alisema Mfalme Suleiman.
Angalia utungo huu nao, “Kijana
mmoja akaulizwa hivi ukiambiwa upewe milioni kumi za Kitanzania uchome vyeti
vyako utakuwa tayari? Kijana akajibu nitakuwa tayari siyo vyeti tu nitachoma
mpaka nyumba zote za waalimu na mabweni na kila kitu”. Hivi tungo kama hii inatufundisha nini zaidi
ya kuidhalilisha elimu yetu? Kwamba elfu kumi ina thamani kuliko elimu ya
Tanzania!
Kitendo cha kuibeza elimu yetu
kimewafanya watanzania wengi kukosa imani na shule zetu kabisa. Badala yake,
shule zetu zimebaki ni kimbilio la walala hoi, huku walala hai wakiishia shule
za kimataifa na Ughaibuni. Kuna jamaa aliwapeleka watoto wake Uganda wakarudi
wanaongea kiganda. Walirudi ni wajinga zaidi ya walivyokwenda. Alifikiri Uganda
nako ni Ughaibuni. Jamani mbona tunakuwa
kama ndege aendaye haraka mtegoni?
Masengenyo haya huwafanya
wasomi wajiskie vibaya na kuwa wanyonge. Nadhani kama wasomi hawapaswi kujibu
mapigo kwa kila anayewatukana, badala yake kama jamii tuupitie tena mfumo wetu
wa elimu upya. Ni ukweli usiopingika kwamba mfumo wetu wa elimu hauwezi kuandaa
watu watakaoendani na kasi ya dunia.
Tunatakiwa kuufumua na kuusuka
ili uweze kuzalisha wasomi watakaokuwa wakombozi wa jamii, wasomi watakaotoa
majibu ya matatizo ya jamii yetu badala ya kuendelea kuwa na wasomi
wanaotegemea kuajiriwa na wakati ajira zenyewe hatuna. Juma lijalo nitajadili
elimu tuitakayo! Asanteni!
Wasomi Wajinga
ReplyDelete