Ujumbe wa Papa Fransisko kwa Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji 2017
‘WAHAMIAJI
wadogo ni wahanga wasio na sauti’ ndiyo kauli mbiu inayoongoza maadhimisho ya
Siku ya 103 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani itakayoadhimishwa na Kanisa hapo
Januari 15, 2017. Baba Mtakatifu Fransisko katika ujumbe wake kwa siku hii,
anaangalia kwa jicho la masikitiko mateso na mahangaiko ya watoto wadogo
wanaolazimika kukimbia nchi zao na kujikuta wakiwa wanaishi ugenini.
Watoto hawa ambao “hawaonekani” na wala hawana
sauti wamejikuta wakiishi katika mazingira magumu na hatarishi
yanayowatumbukiza kwa urahisi katika ukahaba na biashara ya ngono; ni kundi
linalofanyishwa kazi za suluba pamoja na kupelekwa mstari wa mbele kama askari.
Watoto hawa wamekuwa wakibebeshwa mzigo wa
biashara haramu ya dawa za kulevya na hatimaye kutumbukizwa katika magenge ya
kihalifu. Ni watoto wanaolazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na vita,
manyanyaso, dhuluma na matokeo yake wanajikuta wakiwa peke yao bila msaada wa
wazazi na walezi wao. Maandiko Matakatifu yanaonya kwa ukali wale wote
wanaosababisha makwazo kwa watoto wadogo.
Baba Mtakatifu amesema kuwa katika maadhimisho ya
Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa Mwaka 2017, anapenda kuweka mkazo
juu ya matendo na mahangaiko ya watoto wakimbizi na wahamiaji, hasa wale ambao
wako pweke. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna idadi kubwa ya watoto wanaoishi nje
ya mazingira ya familia na nchi zao na hivyo kujikuta wakiwa kama wakimbizi na
wahamiaji, changamoto kubwa katika ulimwengu mamboleo.
Wakimbizi na wahamiaji na watu wanaotafuta fursa
za ajira, maisha bora zaidi lakini kuna watu wanaolazimika kuyakimbia makazi na
nchi zao kwa matumaini ya kupata amani na usalama wa maisha.
Baba Mtakatifu anasema, waathirika wakubwa zaidi
ni kundi la watoto wadogo wanaokumbana na majanga ya maisha, umaskini pamoja na
matukio ambayo yanajikita katika ulimwengu wa utandawazi hasi, kiasi cha
kuwatumbukiza katika biashara haramu ya binadamu.
Hili ni kundi linalohitaji mazingira ya kifamilia,
ili kulindwa na kuendelezwa na wazazi pamoja na walezi wake. Watoto wana haki
ya kupata elimu bora kutoka ndani ya familia na shule, ili waweze kukua na
kukomaa, tayari kuwajibika barabara katika ustawi na maendeleo ya nchi zao kwa
siku za usoni.
Baba Mtakatifu anasema, ili kukabiliana na
changamoto hizi zote kuna haja ya kutambua kwamba, wakimbizi na wahamiaji ni
sehemu ya historia ya ukombozi hata Waisraeli wanakumbushwa katika Agano la
Kale kwamba, kuna wakati hata wao walikuwa ni watumwa katika nchi ya kigeni,
changamoto ya kusoma alama za nyakati, ili kujenga na kudumisha umoja na
mshikamano na watu wanaolazimika kuzikimbia au kuzihama nchi zao.
Watu watambue na kuguswa na mahangaiko ya
wakimbizi, ili kuwaonesha ukarimu, tayari kutambua mpango wa Mungu hata katika
mazingira kama haya kwani Jumuiya ya Kikristo inawaambata watu wote kutoka
katika lugha, jamaa na taifa. Kila mtu ana thamani kubwa mbele ya Mwenyezi
Mungu na kwamba, utu na heshima ya binadamu kamwe hauwezi kulinganishwa na
vitu. Ubora wa taasisi yoyote ile unapimwa kutokana na jinsi inavyotoa
kipaumbele chake kwa utu na heshima ya binadamu, lakini zaidi jinsi
inavyowahudumia wanyonge ndani ya jamii na katika mazingira kama haya watoto
wakimbizi na wahamiaji.
Baba Mtakatifu anaitaka Jumuiya ya Kimataifa
kuhakikisha kwamba inajikita katika sera ambazo zitasaidia kuwalinda,
kuwaingiza watoto katika maisha ya kijamii sanjari na kuivalia njuga changamoto
ya wakimbizi na wahamiaji duniani, ili watoto hawa wasitumbukie mikononi mwa
watu waliofilisika kiroho, kimaadili na kiutu.
Comments
Post a Comment