Yaliyojiri katika mahojiano ya Papa Francisko na Bwana Pablo Ordaz!

Kanisa linapaswa kuwa karibu sana na watu kwa ajili ya watu ili kuwapeleka kwa Mungu mbinguni kwa njia ya Kristo Yesu. Mapinduzi na mageuzi ya kweli ndani ya Kanisa daima yanafanywa na watakatifu kwa njia ya toba na wongofu wa ndani. Viongozi wa Kanisa wajenge utamaduni wa kukubali kukosoa na kukosoana: katika ukweli, uwazi, upendo na udugu. Ni mapema mno kuanza kumkosoa Rais Donald Trump wa Marekani. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuibua mbinu mkakati utakaowasaidia, wahudumia na kuwaingiza wakimbizi na wahamiaji katika maisha ya jamii zinazowahifadhi, kwa kujenga na kudumisha madaraja ya watu kukutana na kusaidiana!
Kimsingi haya ndiyo mambo makuu ambayo Baba Mtakatifu Francisko amejitahidi kuyafafanua kwa kina na mapana katika mahojiano maalum aliyofanya na Bwana Pablo Ordaz wa gazeti la El Paìs linalochapishwa kwa lugha ya Kihispania. Mahojiano haya yamechapishwa kwa urefu kabisa katika toleo la tarehe 20 Januari 2017. Baba Mtakatifu anasema, tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kunako mwaka 2013 ameendelea na maisha yake kama kawaida kwani si rahisi mtu mwenye umri wa miaka 76 kubadilika, vinginevyo ni kujidanganya kabisa.
Baba Mtakatifu anasema ameendelea kubaki kuwa ni Padre wa barabarani, anayetamani kukaa kati ya watu kwa ajili ya watu, ili kuwapeleka mbinguni kwa njia ya Kristo na Kanisa lake. Kanisa linapaswa kuwa karibu na watu kwa ajili ya watu na wala si vinginevyo. Lengo ni kujenga umoja, udugu na mshikamano miongoni mwa waamini ili kutoa ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Huu ni mshikamano unaofumbatwa katika matendo ya huruma kiroho na kimwili, kama anavyokaza Kristo Yesu katika Injili ya Mathayo, sura 25 yaani matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Kwa njia hii, waamini wanaweza kugusa Fumbo la Mwili wa Kristo kwa njia ya huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii!
Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kukaza kwa kusema, licha ya udhaifu wa kibinadamu unaooneshwa katika Sekretarieti kuu ya Vatican, “Curia Romana” lakini pia kuna watu watakatifu ambao wamejisadaka kwa ajili ya huduma kwa Kristo na Kanisa lake. Ikumbukwe kwamba, wadau wakuu wa mchakato wa mageuzi ya kweli ndani ya Kanisa ni watakatifu; wadhambi waliotubu na kumwongokea Mungu wakawa tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili kumwilisha Injili katika uhalisia wa maisha ya watu!. Watakatifu hawa ni watu wa familia; wazee na vijana wanaoendelea kujisadaka kwa sala na huduma kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Utakatifu wa umati huu wa waamini ni mkubwa kwa ajili ya kulitakatifuza Kanisa la Kristo, licha ya mapungufu ya kibinadamu yanayojitokeza!
Baba Mtakatifu akijibu swali kuhusu mchakato wa mageuzi anaoendelea kuufanya ndani ya Kanisa kiasi cha kukumbana na upinzani kutoka kwa baadhi ya viongozi wa Kanisa wasiotaka mabadiliko kama ilivyojidhihirisha katika Wosia wake wa kitume “Furaha ya upendo ndani ya familia” “Amoris laetitia” anasema, hakuna mageuzi, bali anatekeleza mchakato wa kuiendeleza Injili ya Kristo katika uhalisia wa maisha ya watu kwa kuwasindikiza waamini katika hija ya maisha yao, ili kweli waweze kukutana na huruma na upendo wa Mungu unaofunuliwa kwa njia ya Kristo Yesu.
Baba Mtakatifu anatambua kwamba, katika maisha na utume wake, kuna umati mkubwa wa familia ya Mungu unaomsindikiza. Kwa wale wasiokubaliana naye katika baadhi ya mambo, anawaalika kujitokeza ili kuweza kujadiliana katika ukweli na uwazi; katika upendo na udugu badala ya kuanza “kupika majungu mitaani kwani majungu si mtaji, kama ungalikuwa ni mtaji, basi wangetajirika wengi”. Kila mtu anayo haki ya kutoa maoni yake katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo!
Kuhusu Taalimungu ya Ukombozi ambayo kwa miaka kadhaa ililitikisa Kanisa la Amerika ya Kusini, kiasi cha kupigwa marufuku na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kardinali Joseph Ratzinger wakati huo akiwa ni Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa alitoa nyaraka mbili zilizokuwa na maelezo ya kina! Waraka wa kwanza ulifafanua kwa kina na mapana “Taalimungu ya Ukombozi” kwa kupembua Siasa ya Ukomunisti ili kubainisha mambo mazuri yaliyokuwa yanafumbatwa katika siasa hiyo! Kimsingi, “Taalimungu ya Ukombozi” imekuwa na mambo yake mazuri pia na mambo ambayo yalikuwa yanakinzana na tunu msingi za Kiinjili.
Baba Mtakatifu Francisko akizungumzia kuhusu mchakato wa ujenzi wa uchumi endelevu na shirikishi; unaozingatia mahitaji msingi, utu na heshima ya binadamu anasikitika kusema, leo hii dunia iko kwenye “Vita kuu ya Tatu ya Dunia” iliyomeguka vipande vipande na hivyo kuendelea kuleta madhara sehemu mbali mbali za dunia. Leo hii, Jumuiya ya Kimataifa inazungumzia hatari ya matumizi ya silaha za kinyuklia kana kwamba, ni jambo la mzaha! Jambo ambalo linamtisha sana Baba Mtakatifu ni pengo kubwa linaloendelea kujitokeza kati ya maskini, “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi” na matajiri “wanao kula na kusaza vinono”! Kuna kundi dogo sana la watu duniani linalomiliki na kuhodhi walau asilimia 80% ya utajiri wote wa dunia. Hii inaonesha kwamba, kiini cha uchumi ni utajiri na faida kubwa la wala si binadamu, mahitaji yake msingi, utu na heshima yake. Jumuiya ya Kimataifa inaendelea kujenga uchumi unaosababisha majanga makubwa kwa binadamu; uchumi unaojenga utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu!
Baba Mtakatifu Francisko akijibu swali kuhusu maoni yake kwa Rais Donald Trump wa Marekani anasema, si tabia yake kumhukumu mtu pasi ya kuona matendo na maamuzi yake! Ni mapema sana kuanza kumshutumu Rais Trump na sera zake. Jambo la msingi ni kuvuta subira ili kuona kile atakachoamua na kutenda katika uhalisia wa mambo na wala si katika dhana ya kufiri na kuacha mambo yakiwa yanaelea kwenye ombwe kwani huu si Ukristo hata kidogo! Katika mazingira ya hali tete, ugumu wa maisha na majanga mbali mbali yanayomwandama mwanadamu, daima watu wanatafuta mkombozi atakaye wavusha katika majanga haya kwa kuwapatia utambulisho wao wa kitaifa.
Hivi ndivyo ilivyotokea nchini Ujerumani, wakampigia kura ya kidemokrasia Adolfu Hitler, badala ya kuwapatia utambulisho waliokuwa wanalilia, akawatumbukiza katika majanga makubwa ya kihistoria. Katika hali ya kukata na kujikatia tamaa, mara nyingi wanadamu wanakosa muda wa kufanya mang’amuzi ya kina na matokeo yake ni kutafuta kiongozi ambaye wanadhani kwamba, atawapatia utambulisho wa kitaifa, atawalinda kwa kujenga kuta na waya za umeme dhidi ya watu wengine ambao wanataka kuwapoka mali na utambulisho wao wa kitaifa. Hii ndiyo hatari kubwa katika maisha. Kumbe, hapa kuna haja ya kuendeleza daima mchakato wa majadiliano ya kina katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi!
Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, Bahari ya Mediterrania imegeuka kaburi la wazi linaloendelea kumeza katika tumbo lake, wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta usalama, hifadhi na maisha bora zaidi. Baba Mtakatifu anatumia fursa hii kuishukuru na kuipongeza Serikali ya Italia ambayo licha ya changamoto za matetemeko ya ardhi na kuanguka kwa theluji kubwa inayoendelea kusababisha majanga makubwa kwa watu na mali zao, bado inaendelea kutoa msaada na hifadhi kwa wakimbizi na wahamiaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Kila nchi inayo haki ya kulinda mipaka yake, lakini hakuna nchi ambayo ina haki ya kuwazuia raia wake kujadiliana na jirani zao. Kanisa hata katika ukimya wake, linaendelea kutekeleza dhamana na wajibu wa kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia.
Baba Mtakatifu anakaza kusema, diplomasia ya Vatican ni kujenga na kudumisha madaraja ya watu kukutana ili kukuza na kudumisha utu, heshima, ustawi na maendeleo ya wengi. Ni diplomasia inayojikita katika mchakato wa kukuza haki, amani na ushirikiano wa kimataifa kwa ajili ya mafao ya wengi. Kuna umati mkubwa wa wanawake, wasichana na watoto wanaotumbukizwa katika utumwa mamboleo, nyanyaso na dhuluma mbali mbali! Wanawake wanapaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Kanisa.
Baba Mtakatifu Francisko akijibu swali kuhusu afya ya mtangulizi wake, Papa mstaafu Benedikto XVI anasema, anaendelea vyema, ila tu anasumbuliwa na miguu kiasi kwamba, lazima atumie fimbo ili kutembea, lakini bado ana kumbu kumbu ya ajabu utadhani ni “Tembo”. Anaweza kukufafanulia mambo katika undani wake, ukabaki umeshika tama! Anahitimisha mahojiano haya maalum na Bwana Pablo Ordaz wa Gazeti la El Paìs kwa kusema, tangu tarehe 16 Julai 1990, takribani miaka 25 iliyopita hapendi sana kuangalia Televisheni na kwamba, hajutii kwa uamuzi huu kwani hakuna jambo linalomkosa katika maisha. Hata katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro anasema, bado Mwenyezi Mungu amemkirimia kipaji cha kutabasamu kwa raha zake mwenyewe! Hii ndiyo siri ya Furaha ya Injili!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI