YUBILEI YA MIAKA MIA MOJA YA UPADRI TANZANIA
Waamini Wawaombee Makuhani
Waamini wachache wamepata kuuliza:
Katika kuadhimisha Mwaka wa Yubilei ya Upadri, kuna nafasi ya Mapadri kufanya
mazoezi mbalimbali ya kiroho. Je, waamini wanatakiwa wafanye kitu gani hasa? Tunapozungumza kuhusu
Mapadri tunamaanisha wale wote waliopata Sakramenti ya Daraja takatifu:
Ushemasi, Upadri na Uaskofu ambayo ni
Daraja ya Upadri katika ukamilifu wake. Tuone uzito wa madaraka
waliyopewa wakati wa Liturujia ya Daraja Takatifu, halafu tutaona nini
kinachotakiwa.
Daraja
Takatifu ya Ushemasi
Kanisa Katoliki lina utaratibu
madhubuti wa kuwaweka wakfu makuhani wa
kuadhimisha Liturujia takatifu na
kuwatumikia waamini katika yale yamhusuyo Mwenyezi Mungu (Rej. Ebr 5:1). Kanisa linatoa malezi
kwa muda wa kutosha ili kuwaandaa kitaaluma na kuwajenga kimaadili vijana wale
wanaotaka kuwa makuhani. Kisha hutoa Daraja takatifu katika Liturujia
maalum.
Daraja kubwa ya kwanza ni Ushemasi.
Katika Liturujia ya Ushemasi Wakristo hukumbushwa wajibu wa Shemasi kwamba: “humsaidia
Askofu na Mapadri katika huduma ya Neno la Mungu, Altare na ya upendo”(Liturujia ya Ushemasi). Shemasi anapaswa kuhubiri Injili, kuandaa
vipaji kwa ajili ya sadaka ya Ekaristi na kuwagawia waamini Mwili na Damu ya
Bwana.Kama anaagizwa na Askofu, anakuwa na wajibu wa kuwaonya na kuwafunza
katika mafundisho ya Kristo waamini na wasio waamini, kuongoza sala,
kuadhimisha Sakramenti ya Ubatizo, Ndoa na kuwapelekea waliopo kufani
Komunyopamba, kuongoza Liturujia ya mazishi.
Katika Liturujia ya kutoa Daraja
takatifu, kabla ya kuwekewa mikono kijana anaulizwa maswali kadhaa na hujibu: Nataka.
Swali la mwisho katika mfululizo wa maswali hayo linasema: “Je, wataka kulinganisha bila
kukoma maisha yako na mfano wa Kristo, ambaye Mwili na Damu yake utavigusa
altareni?” Kujibu swali hili
Mteule hutanguliza kuomba msaada wa Mungu hivi: “Kwa msaada wa Mungu, nataka.”
Kwa kuulizwa vile Liturujia inaweka wazi
kwamba mtu halazimishwi bali mbele ya waamini anaamua mwenyewe kuitika wito wa
Mungu na kupata Daraja takatifu ya Ushemasi.
Baada ya kumpa Daraja ya Ushemasi, Askofu humkabidhi Shemasi
mpya Kitabu
cha Injili na kumwambia hivi: “Pokea Injili ya Kristo, ambayo umewekwa
kuwa mhubiri wake; angalia, usadiki hayo utakayosoma, ukafundishe hayo
utakayosadiki na ukashike hayo utakayofundisha.”
Basi, ili waweze kuishi kadiri ya
wito wao Mashemasi wanahitaji msaada wa
Mungu. Kwa namna ya pekee mwaka huu wa
Yubilei ya Upadri hapa Tanzania, waamini wanatakiwa kuwaombea Mashemasi na
Makuhani wao.
Daraja Takatifu
ya Upadri
Kama inavyokuwa katika Liturujia ya
kupata Ushemasi, Liturujia ya Daraja Takatifu ya Upadri hufuata utaratibu
uleule. Shemasi akishaitwa na kuitika,
Askofu anayetoa Daraja Takatifu anamjulisha rasmi kwa waamini na kuwaeleza
hadhi ya Upadri na wajibu wake. Sehemu ya mafundisho hayo ya utambulisho
inasema: “Na ndugu huyu baada ya kufikiriwa sana anawekwa sasa katika Daraja ya
Upadri ili naye apate kuwa mhudumu wa Kristo Mwalimu, Kuhani na Mchungaji.
...Naye atafananishwa na Kristo aliye Kuhani mkuu na wa milele, na ataunganishwa
na ukuhani wa Maaskofu; yaani atawekwa wakfu kuwa kuhani halisi wa Agano Jipya
ili aihubiri Injili, alichunge taifa la Mungu na kuziadhimisha Ibada takatifu,
hasa sadaka ya Bwana.”
Kisha utambulisho kwa waamini, Askofu
humwelekea Shemasi na kumwambia wajibu wake atakaotekeleza baada ya kuwekewa
mikono na kuwa Padri. Sehemu ya mafundisho hayo
inasomeka hivi: “Hivyo uwagawie wote lile Neno la Mungu ambalo nawe
ulilipokea kwa furaha. Unapotafakari sheria ya Bwana angalia usadiki kile
unachokisoma, na kufundisha kile unachokisadiki, na kufuasa kile
unachokifundisha. ...ili kusudi kwa neno na kwa mfano upate kuijenga nyumba yaani
Kanisa la Mungu.” Hayo yanahusu wajibu wa Padri wa kufundisha na
kuhubri Neno la Mungu. Anatakiwa kuhubiri siyo tu kwa maneno bali pia kwa mfano
wa maisha yake.
Kuhusu wajibu wa kutakasa kwa
kuadhimisha Sadaka ya Bwana anaangalishwa hivi: “Kwa hiyo elewa vizuri
unachokifanya, na iga unachokitenda; na
kwa kuwa unaadhimisha fumbo la kifo na ufufuko wa Bwana, jitahidi kutiisha viungo
vyako kwa kukomesha vilema vyote na kuenenda katika upya wa uzima”.
Mafundisho hayo ni mazito; Padri inampasa kuadhimisha Ekaristi kwa ibada na
uchaji, kwani anaadhimisha tendo takatifu sana. Anatakiwa kujitahidi kuishi
katika maadili mema. Katika mfululizo wa maswali ya kumhoji, hujibu daima: Nataka. Swali la mwisho, lakini linasema hivi:
“Je, wataka kujiunga zaidi siku hadi
siku na Kristo Kuhani Mkuu ambaye alijitoa mwenyewe kwa Baba kuwa sadaka safi
kwa ajili yetu na pamoja naye kujiweka wakfu kwa Mungu kwa ajili ya wokovu wa
watu?”
Hapo Padri-mteule anahitaji sana
msaada wa Mungu na hujibu: “Kwa msaada wa Mungu, nataka”. Swali
hili linahusu jitihada ya Padri mpya kujiunga na Kristo na kujiweka wakfu kwa
Mungu siku kwa siku. Jitihada ya kuwa
mwadilifu na kufanana na Yesu Kristo ni jambo la kila siku. Katika mwaka huu
maalum Wakristo wanatakiwa kuwaombea Mapadri ili Mwenyezi Mungu awawezeshe
kuishi kadiri ya wito wao. Mara nyingi baadhi ya waamini hupenda kuwasengenya
na kuongea kuhusu mapungufu ya Makuhani;
lakini kwa wito maalum wa Yubilei ya Miaka 100 ya Upadri waamini wafanye bidii kumshukuru Mwenyezi
Mungu kwa zawadi ya miito ya Upadri na kuwaombea Makuhani wao.
Daraja
Takatifu ya Uaskofu
Daraja Takatifu ya Uaskofu ni kilele
cha Sakramenti ya Daraja Takatifu, kwani
ni Urika wa Mitume. Mafundisho anayopewa Askofu-mteule ni mazito zaidi ya yale
ya Upadri. Anakumbushwa kwamba kuwa Askofu ni kuwa mtumishi, wala siyo adhama.
Askofu anatakiwa kutumikia na siyo kutawala. Katika mahojiano kuhusu
kupokea
utumishi huo anaulizwa maswali tisa. Swali la tisa linasimama hivi: “Je,
wataka kumwomba bila kukoma Mungu Mwenyezi kwa ajili ya taifa lake takatifu na
kutekeleza utume wa ukuhani mkuu pasipo lawama?” Askofu-mteule hujibu: “Naam,
kwa msaada wa Mungu, nataka.”
Katika Liturujia ya kumweka wakfu
Askofu-mteule, mashemasi wawili hushikilia Kitabu cha Injili kinachowekwa juu
ya kichwa chake, ishara ya madaraka ya
kuwa Kuhani mkuu na wajibu wa kwanza wa kuhubiri na kutetea imani. Mteule
yampasa kujibu kwa dhati ya moyo wake “Nataka” au “Kwa msaada wa Mungu, nataka”,
mbele ya Mwenyezi Mungu; kutekeleza hayo yote
anahitaji sana msaada wa Mwenyezi
Mungu. Kwa hiyo kabla ya kupewa Daraja takatifu Liturujia imeweka nafasi muhimu
kwa waamini wote kumwombea kwa Maombi
makuu ya Litania wakati huo
Mteule anakuwa amelala kifudifudi ili kujinyenyekea kwa Mwenyezi Mungu na
kumuomba kwa dhati neema zake.
Hatima
Tumeona kwa kifupi Liturujia ya
Daraja takatifu. Kwa kuzingatia madaraka mazito wanayotwishwa katika kupata
Daraja takatifu, katika mwaka huu wa Yubilei ya miaka 100 ya Upadri hapana budi
Wakristo kuwaombea Makuhani kwa bidii ili hayo waliyoahidi wakati wa kupewa
Daraja Takatifu waweze kuyaishi. Umuhimu
huo wa kuomba siyo tu kwa nafasi hii ya Yubilei, bali kila siku Wakristo
wanatakiwa kuwaombea Makuhani wao. Nao Makuhani wanatakiwa pia kuwaombea
waamini wao kama wanavyoahidi katika
Liturujia ya Daraja takatifu.
Comments
Post a Comment