Serikali Yatoa Tahadhari Kuhusu Mafua Ya Ndege
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imewatahadharisha Watanzania juu ya kuwapo kwa virusi vya ugonjwa wa mafua ya ndege.
Ugonjwa huo umegundulika kuwapo katika nchi jirani ya Uganda ambako taarifa zinaeleza kuwa maeneo yaliyoathirika ni yale yanayozunguka Ziwa Victoria.
Tahadhari hiyo imetolewa jana na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kupitia taarifa yake iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Kurugenzi ya Mawasiliano Serikalini- Afya.
“Ugonjwa huu umegundulika baada ya kuwapo kwa vifo vingi vya ndege pori katika maeneo ya Lutembe Beach, Masaka, Kachanga, Bukibanga na Bukakata nchini Uganda.
“Vilevile, vifo hivi vimetokea kwa baadhi ya ndege wafugwao (kuku na bata) na inahisiwa kuwa ndege hao wamepata virusi vya ugonjwa huo kutoka kwa ndege pori wanaohama kutoka nchi za Ulaya,” alisema.
Waziri Ummy alisema vifo hivyo vya ndege pori vilianza kuonekana tangu Januari 2, mwaka huu na vimeonekana kuendelea hadi sasa.
“Kwa hapa nchini hakuna vifo vya ndege vilivyoripotiwa hadi sasa,” alisisitiza.
Alisema ingawa hadi sasa hakuna binadamu aliyeonekana kuwa na dalili za ugonjwa huo nchini Uganda, tahadhari inatolewa kwa kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kusambaa kwa binadamu ikiwa hatua madhubuti za kujikinga hazitazingatiwa.
Waziri Ummy alisema ugonjwa huo unasababishwa na virusi aina ya Influenza na huenezwa na ndege pori wanaohama hama.
Alisema ndege hao hubeba virusi vya ugonjwa huu bila ya kuonesha dalili za ugonjwa.
“Hivyo huweza kuambukiza ndege wanaofugwa majumbani mfano kuku na bata wakati wanapokutana nao. Aidha ndege hao huweza kuambukiza ugonjwa kupitia njia ya kinyesi ambacho hudondoshwa ardhini au kwenye mabwawa na madimbwi ya maji,” alisema.
Aliongeza: “Kwa kuwa binadamu huwezaa kuambukizwa ugonjwa huu kwa kugusana na ndege au kinyesi cha ndege aliyeathirika na ugonjwa huu. Ni muhimu kutokugusa mizoga ya ndege pori au kinyesi chake.”
Alisema kuwa binadamu anaweza pia kupata maambukizi wakati wa kuchinja kuku, kunyonyoa manyoya, na wakati wa kutayarisha kabla ya kumpika.
Waziri Ummy aliwataka wananchi watoe taarifa iwapo wataona dalili zozote za ugonjwa na vifo katika jamii ya ndege wa kufugwa na ndege pori.
“Kuna uwezekano wa virusi hivi kuambukizwa kutoka kwa binadamu mwenye uambukizo kwenda kwa binadamu mwingine, na hii ikitokea inaweza kusababisha mlipuko mkubwa unaoweza kusambaa pande zote za dunia,” alisema.
Comments
Post a Comment