Papa: Martin Luther alitaka kulipyaisha na wala si kuligawa Kanisa!

Ujumbe wa Kiekumene kutoka Finland kwa muda wa miaka thelathini umekuwa ukifanya hija ya kiekumene mjini Roma wakati wa maadhimisho ya Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo, changamoto kwa Wakristo kutubu na kumwongokea Kristo, Mkombozi wa wote. Uekumene wa kweli unafumbatwa katika toba na wongofu wa ndani kwa Kristo Bwana na Mkombozi, tayari kuwaendelea jirani kwa moyo wa huruma na mapendo, tayari kuanzisha mchakato wa upatanisho.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo kwa Mwaka 2017 ni ”Upatanisho: upendo wa Kristo unatuwajibisha”. Katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene, kunako tarehe 31 Oktoba 2016, Wakristo kutoka sehemu mbali mbali za dunia walikusanyika kwa ajili ya kusali mjini Lund, nchini Sweden kama sehemu ya uzinduzi wa Maadhimisho ya Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani; maadhimisho ambayo yana umuhimu wake pekee katika maisha ya kiutu, kitaalimungu na kiroho.
Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi, tarehe 19 Januari 2017 wakati alipokutana na kuzungumza na Ujumbe wa Kiekumene kutoka Finland unaofanya hija ya kiekumene mjini Roma. Baada ya miaka 50 ya mchakato wa majadiliano ya kiekumene kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Duniani, waamini wa Makanisa haya hatimaye, wameweza kuweka hadharani mambo msingi yanayowaunganisha; kwa kutambuana kwamba, wote ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa; watu wanaopaswa kutubu na kumwongokea Mungu kutokana na dhambi ya utengano ambayo kweli imelitesa Kanisa la Kristo!
Katika mwanga huu, wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani mjini Lund, nchini Sweden, Wakristo wamekumbushwa kwamba, Martin Luther hakuwa na mpango wa kuanzisha wala kuligawa Kanisa, changamoto na mwaliko wa kusonga mbele kwa ari na mwamko mpya ndani ya Kristo Yesu, ili kuendeleza kwa pamoja safari ya kiekumene pamoja na kudumisha majadiliano ya kitaalimungu ambayo ni muhimu sana katika mchakato wa upatanisho unaopaswa kuwa ni endelevu katika utekelezaji wake!
Huu ni mwaliko wa kumwachia Roho Mtakatifu atende kazi ili siku moja Makanisa haya yaweze kufikia muafaka katika Mafundisho tanzu na Maadili ya Kanisa, ili kukaribiana na hatimaye kuunda umoja unaonekana zaidi. Baba Mtakatifu anaiombea Tume ya Pamoja ya Majadiliano ya Kiekumene kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiinjili la Kiluteri nchini Finland inayoendelea kufanya kazi ya kutafsiri kuhusu Sakramenti za Kanisa, Ekaristi Takatifu na Utume wa Kikanisa ili iweze kuzaa matunda yanayokusudiwa.
Baba Mtakatifu anakaza kusema, Mwaka 2017 ni kilele cha Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani ni wakati muafaka wa kuimarisha Imani, kugundua umuhimu wa Injili na kudhamiria kuishuhudia kwa ari na mwamko mpya. Ni wakati wakati wa kujenga na kudumisha majadiliano ya Uekumene wa huduma kwa ajili ya maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; Uekumene wa damu na wale wote wanaoteseka kwa vita, dhuluma na nyanyaso kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, ili kwa kutekeleza yote haya katika upendo na mshikamano, siku moja Kanisa liweze kuwa na umoja mkamilifu.
Baraza la Kiekumene nchini Finland, mwaka 2017 linaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwake, changamoto kwa waamini kusimama kidete kuungama na kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, kama alivyoshuhudia Mtakatifu Henrik, kwa kujikita katika ushuhuda wa huduma, udugu na ushirikiano. Hija hii isaidie pia kuimarisha mchakato wa ushirikiano kati ya Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Finland na Makanisa mengine yote, ili kwa pamoja Wakristo waweze kushuhudia imani, matumaini na mapendo na kwa maombezi ya Mtakatifu Henrik, mchakato huu uweze kuzaa matunda mengi. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amempongeza Askofu Turku wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Finland aliyekuwa ameambatana na wajukuu wake, kwani Kanisa linahitaji kuwa na unyenyekevu wa watoto wadogo, unaowafundisha waamini kudumisha safari ya kumwendea Kristo Yesu katika maisha yao!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI