Asilimia 70 ya walimu wanaidai serikali
IMEELEZWA
kuwa asilimia 70 ya walimu wanaidai serikali ambapo kuanzia mwaka wa fedha
2013/2014 mpaka Desemba 2016, walimu walikuwa wanadai shilingi trilioni 1.185
sawa na trilioni 1.19.
Hayo yameelezwa na Kaimu Katibu
Mkuu wa Chama Cha Walimu Tanzania CWT, Ezekiah Oluoch katika mkutano wake na
waandishi wa habari hivi karibuni, na kubainisha kuwa madai hayo ya walimu
yanaathiri shule kwa kuwa walimu wanapaswa kufanya kazi na akili zilizotulia,
hivyo wanapokuwa na madeni mengi ari ya utendaji wao inashuka.
“Mchanganuo huu wa madeni
umechangiwa kwa kiasi kikubwa na walimu waliostaafu ambao wako 6,044 ambao
hawajalipwa shilingi bilioni 556 ambazo zinapaswa kulipwa na PSPF. Lakini PSPF imeshindwa
kuwalipa kwa sababu serikali haijapeleka fedha za walimu hawa katika mfuko wa
PSPF” ameeleza Ezekiah.
Aidha amesema kuwa walimu
waliopandishwa madaraja mwaka 2016 ni 85,945 na wanadai shilingi bilioni 301,
na kwamba deni linakua kila mwezi kwa kiwango cha bilioni 25 ambapo endapo
halitalipwa hadi kufikia Juni 2017, deni litakuwa limeongezeka kwa shilingi
bilioni 150.
Pia Ezekiah ameiomba serikali
kuongeza walimu kwani kuna upungufu mkubwa wa walimu katika shule mbalimbali
nchini ili hali kuna walimu waliohitimu mafunzo yao na hawajaajiriwa bado.
“Tuna upungufu mkubwa sana wa
walimu shuleni. Hii inatokana na walimu elfu 40 wako mtaani wanasubiri ajira,
serikali haijawaajiri kwa kigezo cha kuhakiki vyeti” ameeleza.
Comments
Post a Comment