MIITO INADUMISHWA KWA KUSALI, KUSIKILIZA NA KUSINDIKIZA-PAPA FRANSISKO


Mama Kanisa ameanza maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, imani na mang’amuzi ya miito itakayoadhimishwa kunako mwaka 2018. Ili kweli Kanisa liweze kupata miito mitakatifu, kuna haja ya kusali, kuwasikiliza vijana kwa makini pamoja na kutembea nao katika matumaini, shida na mahangaiko yao ya ndani, ili hatimaye waweze kupata mambo makubwa katika maisha yao, yaani kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake!
Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 5 Januari 2017 alipokutana na kuzungumza na washiriki 800 wa kongamano la miito lililoandaliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia kwa kuongozwa na kaulimbiu “Simama! Ondoka! Usiogope. Miito na Utakatifu: Mimi ni utume”. Baba Mtakatifu anawataka viongozi wa Kanisa waliopewa dhamana ya kulea miito kuhakikisha kwamba, wanatoa kipaumbele cha kwanza kwa sala, kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikiliza vijana kwa makini pamoja na kuanzisha utume wa shughuli za kichungaji kwa kutembea na vijana katika uhalisia wa maisha yao.
Vijana wanapaswa kuwa na ujasiri wa kusimama tena kama ilivyotokea kwa Mtakatifu Petro alivyokuwa amefungwa gerezani alipoambiwa na Malaika, akasimama akaondoka na kuwakuta Wakristo wakisali kwa ajili yake na walipomwona, hawakuyaamini macho yao! Hata leo hii kuna vijana wengi wanaosikia mwaliko huu wa kusimama na kutembea, lakini bado wanajifungia katika ubinafsi wao, changamoto ni kuthubutu kumfungulia Kristo malango ya maisha yao!
Baba Mtakatifu anayapongeza na kuyashukuru Majimbo na Mashirika ambayo yamebahatika kuwa ni idadi kubwa ya miito mitakatifu, wakati huu ambako pia kuna ukame wa miito kwa baadhi ya majimbo na mashirika ya kitawa na kazi za kitume! Haya ni majimbo ambayo yametoa kipaumbele cha kwanza kwa ajili ya sala ili kuombea miito! Ni wajibu unaotekelezwa na wazee, wagonjwa na wanandoa wapya, kwa kutambua kwamba, familia ni shule ya kwanza ya miito mitakatifu!
Dhamana ya kwanza kwa Askofu ni kuhakikisha kwamba, anasali kwa ajili ya kuombea miito mitakatifu ndani ya Kanisa, huku akisaidiwa na familia ya Mungu inayomzunguka! Pili, ni kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo inayofumbatwa katika maisha yenye mvuto na mashiko!Mapadre wanapaswa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwamegea waamini Mafumbo Matakatifu ya Kanisa. Majitoleo haya yanajionesha hata katika huduma ya michezo kwa watoto Parokiani, jambo ambalo linaweza kusaidia kupandikiza mbegu ya miito ya maisha ya Kipadre na Kitawa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya!
Baba Mtakatifu Francisko anawataka wadau waliodhamishwa malezi ya miito mitakatifu ndani ya Kanisa kukuza na kudumisha utamaduni na utume wa kusikiliza kwa makini pamoja na kutembea na vijana katika shida na mahangaiko yao; katika furaha na matumaini yao ya maisha. Mapadre na watawa wajenge ari na moyo wa kuwasikiliza vijana, kiasi hata cha kupoteza muda pamoja nao, ili kuwasindikiza na kuwaongoza katika maisha na majitoleo kwa Kristo na Kanisa lake. Vijana washirikishwe kikamilifu katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya miito.
Vijana washirikishwe kazi za kimissionari na matendo ya huruma kwa wagonjwa, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii!  Vijana wanapaswa kuwa kweli ni mashuhuda na “majembe” ya huruma ya Mungu katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili! Vijana wasipopendwa na kuthaminiwa, hawa watachoka na kuwa wachovu hata kabla ya muda wa kwenda pensheni!
Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha hotuba yake ya ana kwa ana na wajumbe wa kongamano la miito mitakatifu kutoka Majimbo mbali mbali nchini Italia kwa kuwakumbusha kwamba, ushuhuda wenye mvuto na mashiko kutoka kwa Mapadre na Watawa ni chachu muhimu sana ya miito ndani ya Kanisa. Vijana wanataka kuona Wakleri na Watawa wanaojisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa; watu wasiojitafuta wenyewe katika ubinafsi wao, kwani matendo yanazungumza zaidi kuliko maneno matupu anasema Baba Mtakatifu Francisko!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI