‘Sheria ya habari isikiuke tunu za Kanisa’ Ask. Msonganzila




WITO umetolewa kwa Waandishi wa habari wa Kanisa Katoliki kuhakikisha wanaendelea kutangaza Habari Njema kwa kutumia vyombo vya habari, kwa kufuata sheria na taratibu za nchi  huku  wakizilinda tunu za Kanisa zisitikiswe na  sheria mpya ya huduma ya habari ya mwaka 2016.

Hayo yamesemwa  na Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki Musoma katika kikao  cha dharura cha Wakurugenzi  wa Mawasiliano majimboni na Wakurugenzi wa Vyombo vya habari vya Kanisa Katoliki nchini kilichofanyika Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), kurasini, jijini Dar es salaam .

Awali amewapongeza  wanahabari wa Kanisa Katoliki  kwa majukumu makubwa na magumu ya uinjilishaji waliyo nayo.

 “Mnaifanya kazi hii katika nyanja mbalimbali za jamii, ninyi ni wainjilishaji nambari moja  katika Kanisa na kama ukitaka kuielezea  biblia ama  habari njema  na kuwafikia watu kwa urahisi  ni kupitia viganja vyenu, kalamu zenu na karatasi zenu…

Tunaona watu wana kiu kubwa ya kupata taarifa mbalimbali zinazowazunguka kupata habari njema na mbovu lakini ninyi  tukiamini kama waandishi   wakristo wakatoliki  na katika taasisi za kikanisa tunaamini sehemu kubwa ya mawasiliano yenu mtafikisha habari njema inayomhusu mwanadamu na itajengwa, kupambwa na kufinyangwa na tunu za kikristo kikristo maahali popote,”amesema Askofu huku akiongeza;

“Tunapokuwa tumefika  hapa kujadili pia juu ya sheria hii lengo letu ni kuona kwamba tunu za kikristo za kikanisa hazitikiswi na sheria, kumbe tunashukuru kwa mwaliko huu lakini ninaamini kwamba akili yote iliyopo hapa  wajumbe, mliojikusanya hapa mnaweza kutoa kitu kitakachotusaidia  sana …

Inaweza kuwa na ujenzi mkubwa kiimani kimawasiliano na mahusiano kati yetu sisi wenyewe na serikali inayotuongoza, kati yetu na waamini na kati yetu na  wanachi, huduma yenu siyo ndogo, siyo ya kudharauliwa na inapaswa kupewa  uzito wa kipekee… nilipokuwa naongoza idara hii niliona umuhimu na ugumu wake  na hasa katika ulimwengu wa mawasiliano.”

Awali akifungua kikao hicho Mratibu wa Vijana Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Padri Liberatus Kadio ameeleza kuwa sheria yoyote ni lazima imuhakikishie mwanadamu usalama wake, ilinde haki yake na kumrahisishia maisha yake.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa TEC, Padri Kadio amesema kuwa sheria ni lazima ipeleke furaha kwa watu, ili waishi kama Mungu anavyotaka. Pia amevitaka vyombo vya habari vya kanisa kuchochea uelewa kwa waamini juu ya Jubilei ya miaka 150 ya uinjilishaji Tanzania Bara na miaka 100 ya upadri.


sheria mpya ya huduma ya habari izingatie maadili

Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Mtakatifu Agustino Tanzania Tawi la Dar es salaam (Msimbazi Centre), Padri Dkt. Charles Kitima amesema kuwa sheria mpya ya huduma ya vyombo vya habari ya mwaka 2016 iliyosainiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli iwajenge waandishi katika kutenda utume wa uinjilishaji kwa kuzingatia  maadili mema na kuzingatia sheria na kanuni za nchi.

Padri. Dkt. Kitima amewaasa  Wakurugenzi na wanahabari wa Kanisa  Katoliki nchini kusoma    Hati za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatikani ya Inter  Mirifika  ya mwaka 1965 na ili  walifahamu kwa undani Kanisa Katoliki ili iweze kuwasaidia katika uinjilishaji  sanjari na   wanahabari  walei kupata elimu Teolojia.

“Pamoja na maelezo mengi kuhusu  sheria  hii, sisi vyombo vya habari vya Kanisa  viendelee kutuweka kuwa makini katika utendaji wetu wa kazi za uinjilishaji ili tusije kujikuta tumeingia katika matatizo…kweli tunahitaji uhuru wa kujieleza na binadamu  wanahitaji  uhuru wa kufanya mawasiliano hata sheria  za kimataifa tangu kuumbwa kwa ulimwengu zinatambua uhuru wa kupata  na kutoa habari,”amesema.

Ameonya licha ya kuwepo na tahadhari katika kukiuka sheria  lakini Kanisa liepuke uwoga wa kusema  ukweli  kwa jamii ama kuhubiri injili, kukemea ikiwemo na  kutoa angalizo kwa manufaa  ya  watu wake.

“Mjitahidi kubobea katika taaaluma yenu…pitieni na kutoa ushauri wa kitaaluma kwa wanaosema kwa niaba ya Kanisa na wenye mamlaka hayo ni Mababa Maaskofu, Mapadri, Makatekista na  Viongozi wa  walei. Pitieni ujumbe wanaohitaji kuutoa  na kwa Mababa Maaskofu kupitia barua  za kichungaji kabla ya kuzitoa ili kuepuka  kukiuka sheria…kabla Askofu hajatoa mahubiri tukiacha mahubiri ya kichungaji ni vizuri kujuwa na kumuuliza Askofu mapema katika tamko lolote ili kuepuka kuingia katika mgogoro na  serikali,”amefafanua.


Vyombo vya habari vya Kanisa vyasisitizwa kuwa na umoja

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Mawasiliano, Baraza la Maaskofu Tanzania(TEC), Bernard James amewasihi wakurugenzi  wa mawasiliano  na  wakurugenzi wa vyombo vya  habari za Kanisa  kuwa  na sauti moja hasa kunapotokea matukio ya kitaifa, kushirikiana  katika utoaji wa habari na utafutaji wa habari.

Bernad   ameshauri  kushiriki kwa pamoja  Siku ya upashanaji habari  inayotarajia  kufanyika mwaka huu huku akiwasihi kufanya habari zenye utafiti,vyanzo vya uhakika na uchunguzi wa kina zenye ukweli  na uwazi    ambazo zitawaweka huru na kusisitiza kupitia kabla  matamko  na jumbe zinazotolewa na Maaskofu  kitaaluma  ikiwemo na kutoa ushauri ili kuepuka mivutano na serikali.

Ameviagiza vyombo mbalimbali vya habari vya Kanisa Katoliki  nchini kuripoti matukio mbalimbali yanayoendelea kufanyika ikiwemo na miradi inayofanywa na majimbo katika jamii  kwa kusaidiana na serikali.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI