Historia ya Epifania
Makanisa
ya Kikristo ya nchi ya Magharibi na Sherehe ya Epifania:
HATA
kabla ya mwaka wa 354, Makanisa ya nchi za Magharibi yalikwishaiweka sherehe ya
Kuzaliwa kwa Kristo kama sikukuu ya Krismasi na kuipangia siku ya kuisherehekea
kwake kuwa ni tarehe ya 25 ya mwezi wa Desemba.
Tarehe ya 6 ya mwezi wa Januari
ilikuwa imetengwa kwa kusherehekea sikukuu ya Epifania ya Kristo hasa ule ujio
wa Mamajusi lakini pia kwa kusherehekea ubatizo na harusi ya Kana. Ilipofika
mwaka wa 1955 ilianzishswa sikukuu ya pekee ya kusherehekea ubatizo wa Bwana.
Uanzishwaji wa hiyo sikukuu ya
pekee ya kusherehekea ubatizo wa Bwana kwa makanisa ya nchi za Magharibi
ulidhoofisha zaidi ule uhusiano uliokuwepo hapo awali kati ya sherehe ya
Epifania na ile ya Kuzaliwa kwake Kristo.
Desturi
za Kiliturujia zinazozingatiwa na Makanisa ya nchi za Magharibi.
Wakristo walio wengi wa nchi za
Magharibi wanakuwa na siku 12 za sherehe zikianzia tarehe ya 25 ya mwezi wa
Desemba na kumalizika tarehe ya 5 ya mwezi wa Januari. Hata hivyo, kwa wakristo
wakatoliki, siku hizo za kipindi cha Krismasi kinaanza tangu jioni ya mkesha wa
Noeli hadi Jumapili baada ya Epifania au baada ya tarehe ya 6 ya mwezi wa
Januari.
Makanisa mengi, hasa yale ya
Amerika Latino yana desturi ya kuendeleza kipindi hiki hadi siku arobaini
kikiishia tarehe ya 2 ya mwezi wa Fubruari.
Kwa baadhi ya maeneo, hasa yale
yaliyo katika nchi za Ulaya ya Kati, mapadri waliovaa mavazi meupe wanabariki
maji ya Epifania, ubani na vipande vya chaki. Chaki hizo zilizobarikiwa
zinatumika kwa kuandikia mifupisho ya majina ya wale Mamajusi watatu yaani
Kaspari, Melkiori na Baltazari milangoni mwa majengo ya makanisa na nyumba za
waamini.
Wakati wa kuandika, padri
anatamka maneno ‘Christus mansionem benedicat’ yenye maana kwa lugha ya
Kiswahili ‘Kristo aibariki nyumba hii.’
Makanisa
ya Kiothodoksi ya Kimashariki na Sherehe ya Epifania:
Jina la sikukuu hii kama
inavyosherehekewa na hayo makanisa ya Kiothodoksi ni ‘Teofani’ lenye maana
inayokaribiana na ‘Mungu anayeng’ara au ‘Ufunuo Mtakatifu. ’Katika makanisa
hayo, siku hii ya Teofani ni moja ya zile siku kubwa za mwaka wa liturujia, ikiwa
ni sikukuu ya tatu kwa ukubwa ikitanguliwa na sikukuu ya Pasaka pamoja na ile
ya Pentekoste.
Sherehe ya sikukuu hii
inafanyika tarehe ya 6 ya mwezi wa Januari. Dokezo la kwanza kabisa kuhusu
sikukuu hii lilitolewa na Mtakatifu Klementi wa Aleksandria kama linavyoonekana
katika ‘Stromateis, I XXI, 45.’Dokezo hili linawiana na sherehe ya Kuzaliwa kwa
Kristo na pia na Ubatizo wake wa tarehe ya 6 ya mwezi Januari.
Iwapo mambo ni hivyo, basi sherehe hii inawiana pia na yale mazoea ya
Kanisa la Kitume la nchi ya Armenia linalosherehekea Kuzaliwa kwa Kristo tarehe
ya 6 ya mwezi wa Januari likiitaja sikukuu hiyo kuwa ni ya Kuzaliwa na pia ya
Teofani ya Bwana Wetu Yesu Kristo.
Siku hizi, katika makanisa ya
Kiothodoksi ya Mashariki kinachosisitizwa zaidi ni ule Mng’aro na Ufunuo wa
Yesu Kristo akiwa kama Masiha na pia akiwa kama Nafsi ya Pili ya Utatu
Mtakatifu kama ilivyodhihirishwa saa ile alipobatizwa na Yohani mtoni Yordani.
Siku hii inasherehekewa kwa sababu,kulingana na
mapokeo, ubatizo wa Yesu mtoni Yordani ulikuwa moja ya nafasi mbili tu
ambapo Nafsi zote Tatu za Utatu Mtakatifu zilijionyesha kwa binadamu kwa
pamoja.
Mungu Baba alisikika
akizungumza katika mawingu, Mungu Mwana ndiye aliyekuwa anabatizwa mtoni
Yordani na Mungu Roho Mtakatifu akiwa katika umbo la Hua akishuka kutoka
mbinguni.Nafasi nyingine ambapo Nafsi zote Tatu zilijionyesha, ilikuwa ile ya
Yesu Kugeuka Sura Mlimani Tabor. Hivyo basi, siku hii takatifu inachukuliwa
kuwa ni sikukuu ya Utatu.
Kanisa la Kiothodoksi linauona
ubatizo wa Yesu kama ni ngazi ya kwanza ya kuelekea mlimani Kalvari
alikosulubiwa. Ili kuthibitisha wazo hili nyimbo zinazoimbwa siku ya kumbukumbu
ya Kuzaliwa kwa Yesu zinafanana na zile zinazoimbwa siku ya Ijumaa Kuu.
Desturi
za Kiliturujia kuhusu Epifania zinazozingatiwa na makanisa ya Kimashariki:
Mwanzo
wa Sherehe: Sherehe za Kiliturujia za mwanzo wa Teofani zinaanza
tarehe ya 1 ya mwezi wa Januari na zinahitimishwa kwa sala mwishoni mwa sherehe
hizo hapo tarehe ya 5 ya mwezi wa Februari.
Paramonia:
Paramonia ni siku ya mkesha wa sherehe ambayo ni siku ya lazima ya kufunga kwa
kila mwamini asiyekuwa na matatizo ya kiafya.Waamini hawa hufunga kula chakula
siku nzima hadi nyota ya kwanza inapoonekana saa za jioni. Hapo ndipo chakula
pamoja na mvinyo na mafuta kinapoweza kuliwa. Katika siku hiyo husherehekewa
Saa Takatifu ikiwa na kumbukumbu ya Ijumaa Kuu.
Zile Saa Takatifu hufuatiwa na
Liturujia Takatifu ya Mtakatifu Basili inayoziunganisha sala za jioni na
Liturujia Takatifu. Wakati ule wa sala za jioni masomo 15 ya Agano la Kale
husomwa. Masomo haya yanayoonyesha ishara za Ubatizo wa Kristo husomwa pamoja
na sala za antifona maalumu.
Iwapo Sikukuu ya Teofani
inaangukia siku ya Jumapili au Jumatu, zile Saa Takatifu husaliwa siku ya
Ijumaa inayotangulia. Sala za liturujia za Mtakatifu Yohani Krisostomi hutumika
kwa kusali na mafungo hulegezwa kwa kiasi fulani.
Kubariki
maji: Makanisa ya Kiothodoksi yanabariki maji siku hiyo ya
Teofani. Kwa kawaida tendo hili la kubariki maji hufanywa mara mbili; mara ya
kwanza hufanywa jioni ya mkesha wa sikukuu yenyewe kwenye kisima cha maji
kilicho ndani ya kanisa na hufanywa tena kwa mara ya pili siku ya sikukuu
yenyewe kwenye chanzo cha asili cha maji kilicho karibu na Kanisa.
Chanzo hicho kinaweza kuwa mto,
ziwa, bwawa la kuogelea, bandari, ufukoni, gati n.k. Mwishoni mwa ibada padri
anatoa baraka kwa yale maji. Kwa utaratibu wa nchi ya Ugiriki, baraka hiyo
inatolewa kwa tendo la padri la kuutupa msalaba majini.
Kama uogeleaji unawezekana
katika aina ya maji yanayobarikiwa, waamini wanaogelea kujaribu kuupata tena
ule msalaba.Mwamini anayefanikiwa kuupata msalaba huo anaurudisha kwa padri
anayempa mwamini huyu baraka ya pekee kwa ujasiri aliouonyesha wa kuogelea na
kuupata tena ule msalaba.
Maji yanayobarikiwa siku hiyo
yanachotwa na waamini na kuyapeleka majumbani kwao. Waamini hawatajibariki tu
kwa kujimwagia maji yale bali pia watayanywa.
Kanisa la Kiothodoksi
linafundisha kuwa maji hayo ya baraka ni tofauti na maji mengine kwa sababu
utaratibu wake wa asili huwa umebadilika kutokana na ile baraka na kwa hivyo
huwa hayawezi kuharibika kwa mujibu wa ushahidi wa mwujiza wa Mtakatifu Yohani
Krisostomi. Siku hiyo ya sherehe ya Teofani, kwa kufuata desturi za jadi, huwa
ni siku ya kuwabatiza waamini walioandaliwa kwa kubatizwa siku hiyo.
Kubariki
nyumba: Siku hiyo ya Teofani padre huzibariki nyumba za waamini
kwa kuingia katika kila nyumba na kuzungukia sehemu za bustani akizibariki kwa
maji yale mapya yaliyobarikiwa.
Baada
ya Sikukuu: Sikukuu ya Teofani hufuatiwa na kipindi cha siku 8 cha
kutokuwa na ulazima wa kufunga. Jumamosi na Jumapili baada ya Teofani huwa ni
siku zinazoambatana na masomo ya pekee ya ibada yenye uhusiano na kile kitendo
cha ibilisi cha kumjaribu Kristo. Kwa hiyo huwa kuna mwendelezo kati ya sikukuu
ya Teofani na mwanzo wa kipindi cha Kwaresima.
Comments
Post a Comment