Wazazi waaswa kusaidia Utoto Mtakatifu kuinjilisha
Akitoa homilia katika Misa Takatifu
kigango cha Mbutu Parokia ya Kimbiji Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam Paroko
Msaidizi wa Parokia hiyo Padri Justus Lugayimkam amewakumbusha na kuwataka
wazazi na walezi wote kutambua kuwa, jukumu la kulea Watoto wa Utoto Mtakatifu, lipo
mikononi mwao na mtoto anapokua katika malezi ya dini humfanya awe mwenye
heshima na mchamungu.
Amesema wapo walezi ambao jukumu la Utoto
Mtakatifu wamewaachia walimu jambo linaloleta ugumu kwa walimu pindi inapotokea watoto wanahitaji kushiriki katika
matamasha mbalimbali .
“Watoto
wanahitaji mchango wa kifedha ili waweze kushiriki matamasha na watoto wenzao
kutoka katika maparokia mbalimbali. Amesema michango hiyo ya fedha ni kwaajili
ya nauli na chakula hivyo kila mtoto anapaswa kuchangiwa na mzazi wake ama
mlezi si mwalimu,” amesisitiza.
Amewataka
wazazi kutambua kuwa Yesu Kristo anawapenda watoto waende kwake kama
alivyosema “waacheni watoto waje kwangu
kwa maana ufalme wa mbingu ni wao,” kwa hiyo ni vema wazazi wakawa bega kwa
bega na walimu wa utoto mtakatifu ili kuwawezesha
watoto kuwa wamisionari wa kuinjilisha katika maeneo mbalimbali ndani ya nchi.
Hata hivyo
kilio cha Watoto wa Utoto Mtakatifu kwa
wazazi wao kutowachangia pale wanapohitajika kwenda kuhiji, kuinjilisha ama
kukutana na watoto wenzao kijimbo na kitaifa kimekuwa ni cha muda mrefu na kipo
katika majimbo karibu yote Tanzania.
Hivyo
wazazi wanasisitizwa kuweka kipaumbele cha kuwawezesha watoto wao kukutana
katika kutafakari neno la Mungu, kufanya matendo ya huruma kwa wengine na
kuinjilishana kwani hayo ndiyo malezi chanya kwa watoto hususani katika nyakati
hizi.
Kipaumbele
cha wazazi kiwe katika kuinjilisha watoto wao wawe askari shujaa wa imani yao
huku wakiandaa kizazi chenye imani thabiti, chenye maadili na utu wema katika
jamii.
Comments
Post a Comment