Jubilei ya Miaka 100 ya upadri kufungwa Dodoma
JIMBO Kuu
Katoliki Dodoma limeteuliwa kuwa mwenyeji wa kilele cha Jubilei ya miaka 100 ya
Upadri Tanzania tangu padri wa kwanza mwafrika kupewa daraja takatifu ya
upadri mnamo mwaka 1917.
Hayo yameelezwa na Askofu Edward Mapunda wa Jimbo Katoliki Singida
hivi karibuni alipokuwa akiadhimisha ibada ya misa takatifu ya kutoa Daraja
Takatifu la Ushemasi wa mafrateri wawili wa Shirika la Wamisionari wa Damu
azizi ya Yesu Kanda ya Tanzania , iliyofanyika katika parokia ya amu Azizi ya
Yesu Itigi Singida.
Mafrateri waliopewa daraja Tajatifu la Ushemasi ni pamoja na
Frateri Dominic Mavulla na Frateri Alesandro Manzi,
Askofu Mapunda amesema kuwa ni heshima kubwa iliyotolewa katika
Metropoliani ya Dodoma ambayo inaundwa na majimbo matatu ambayo ni Jimbo kuu
katoliki Dodoma, Jimbo katoliki Singida na Jimbo Katoliki Kondoa , hivyo wana
kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa zawadi hiyo ya kuwa mwenyeji kilele cha
Jubilei ya mIaka 100 ya upadrI.
Amesema kuwa mbali na majimbo mengi kutindikiwa na mapadri lakini
wana sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa hali iliyopo kwa sasa kwani hadi
sasa ni majimbo machache yenye uhaba mkubwa wa watendakazi katika shamba la Bwana.
Hata hivyo amesema kuwa mbali na Jubiulei hiyo ya miaka 100 ya
upadri pia mwaka 2018 Kanisa la Tanzania bara litaadhimisha Jubilei ya miaka
150 tangu ukristo ulipoingia Tanzania na jubilei hiyo itafanyika Bagamoyo.
Askofu Mapunda amesema kuwa kilele cha maadhimisho hayo itakuwa ni
Agosti 15 mwaka huu 2017 katika Jimbo Kuu Katoliki Dodoma katika sikukuu ya
Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni ambapo mapadri wa kwanza waafrika
walipadirishwa Agosti 15 mwaka 1917.
Akizungumza katika ibada hiyo Askofu Mapunda alisema kuwa Jubilei
ni zawadi kutoka kwa mwenyezi mungu hivyo waamini wanapaswa kumshukuru Mwenyezi
Mungu kwa zawadi ya wamisionari waliokuja Tanzania kwa ajili ya kuhamasisha
vijana kujiunga na utume na hatimaye kuwapata mapadri.
Amesema kuwa, Kanisa bado linauhitaji mkubwa wa mapadri hivyo
amewataka waamini kuendelea kuliombea Kanisa katika hitaji hilo ili
uinjilishaji uendelee katika vizazi vya sasa na vijavyo .
Amesema kuwa mfano wa mamajusi ni mfano bora na wa kuigwa kwani
wanatufundisha kumtafuta Mungu kwani wao walikuwa wanafanya hija ya kiroho
katika nyakati tofauti tofauti kumtafuta Yesu Kristo kila mmoja kwa wakati wake
na kumwabudu.
"Mamajusi walizunguka huko na huko walivuka mabonde, milima
na mito katika kuifuta nyota ambayo ilikuwa inawapeleka kumwona Mtoto Yesu
alipokuwa amelazwa baada ya kuzaliwa kwake" aliongeza Askofu Mapunda
Hata hivyo Askofu Mapunda amewataka waamini kujenga tabia ya
kufanya hija za kiroho na watambue kuwa katika shughuli zote za kila siku wanaongozwa
na nyota mbalimbali kwa mfano uuguzi, upadri na hata utangazaji wa neno la Mungu.
Amesema kuwa watu wengi wana njaa ya kiroho na watu wengi
wanauliza ni wapi watapata mponyaji hivyo amewataka pia mapadri kuwa ni
mkombozi wa wanaohitaji uponyaji huo.
Aliwataka kuzisome alama za nyakati na kuzifahamu na
kuwataka kuenenda kujifunza mahangaiko ya watu kama mwanzilishi wa shirika hilo
Mtakatifu Gaspar Del Buffalo alivyokuwa na hamu hiyo.
Awali akimpokea shirikani Frateri Domonic Mavula Mkuu wa Shirika
Proviensi ya Tanzania Padri Chesco Peter Msaga alimtaka kuwa mwanga na nuru ya
kuwaongoza wengine kuvuka kutoka kwenye giza.
Alisema kuwa Dira ya Kanisa kwa sasa ni kuhubiri neno la Mungu na
kazi hiyo inapaswa kuenziwa kwani imeanza kufanyika miaka 100 iliyopita na
ilikuwa ikifanywa na wamisionari waliokuja barani Afrika na Tanzania kwa ujumla
kuendeleza kazi ya uenezaji wa neno la Mungu.
Padri Msaga alisema; “Wamisionari walikuja Tanzania kutuondoa
katika utumwa wa vifungo vya giza la dhambi na kutuwezesha kumwabudu Mungu wa
kweli.
Wamisionari walikuja kwa lengo la kutoa huduma ndani ya Kanisa na
kuwasaidia wenye shida za kiroho,” Aliongeza Padri Msaga.
Akitolea mfano wakati wa mkutano uliofanyika huko amerika amesema
kuwa mkutano huo baada ya kuulizwa nini mpango kazi wa Kanisa la Tanzania kwa
kipindi cha miaka kumi alisema kuwa wao walisemakuwa mpango kazi wa Kanisa la
Tanzania kwa miaka kumi ni kutangaza habari njema ya wokovu na kutangaza
mwaka wa bwana uliokubalika, kuwatangazia wafungwa habari njema ya
kufunguliwa kwao na kuwahubiria maskini habari njema ya wokovu,
Hilo ndilo jukumu la padri na kila muumini katika nyakati hizi.
Comments
Post a Comment