UTUME
WA KATEKESI KATIKA KANISA
SEHEMU
YA KWANZA
ASILI NA MAANA YA NENO KATEKESI
Neno Katekesi kadiri ya mazoea ya wengi
lina maana ya maarifa ya kufundisha katekisimu, pia ni maarifa ya namna ya kufundisha
dini. Dini maana yake ni uhusiano baina ya Mungu na mwanadamu.
Katekesi kama namna ya kufundisha dini, ina maana ya kumwelekeza mtu
atambue uwepo wa Mungu, Uwezo na Nafasi yake katika maisha ya mwanadamu.
Kwa asili neno Katekesi
linalotokana na neno la lugha ya kiyunani Katechein au katechizen likiwa na
maana ya kufundisha kwa mdomo.
Katika Agani Jipya
tunaona mkazo wa namna hiyo ya kufundisha
kwa mdomo katika nukuu mbalimbali kwa mfano:-
‘... enendeni
mkawafanye kuwa wanafunzi wangu... na kuwafundisha
kuyashika yote niliyowaamuru ninyi’ (Mt 28:19-20). ‘...mtu huyo alifundishwa njia za Bwana, na
kwa kuwa roho yake ilikuwa ikiwaka alianza kunena na kufundisha kwa usahihi
habari za Yesu...’ (Mdo 18:25); ‘...nipate kunena maneno...nipate kuwafundisha wengine’ (1Kor
14:19); ‘....mwanfunzi amshirikishe mkufunzi wake katika mema
yote’ (Gal 6:6); ‘...mmekwisha kulisikia
neno neno la kweli, habari njema ya wokovu wenu...’ (Efe 1:13). Pamoja
na kufundisha kwa mdomo, bado katika Injili neno katekesi linajionesha hasa
katika maana ya kazi ya kuhubiri ambayo hufanyika zaidi kwa njia ya mdomo kama tunavyosoma
katika habari za Yesu, alikuwa akihubiri na kufundisha kwa mdomo mfano ‘hata baada ya Yohana kutiwa gerezani Yesu
akaenda Galilaya akihubiri habari njema ya Mungu (Mk. 1:14,). ‘Naye
alikuwa akizunguka katika Galilaya yote akifundisha na kuhubiri habari njema
katika masinagogi yao’ (Mt. 4:23).
Ni katika Injili ilivyosimuliwa na Luka
tunasikia Yesu akisisitiza kuwa utume wake awali ya yote ni kuhubiri ni lazima
autimize na kuukamilisha kadiri ya mpango wa Mungu Baba ninamnukuu ‘Roho wa
Bwana yu juu yangu kwa maana amenitia mafuta ili niwahubiri maskini Habari
Njema’ (Lk 4:18). Tena alikazia kuwa ‘imenipasa
kuhubiri habari njema ya ufalme wa Mungu katika miji mingine pia’ (Lk.4:43), mwisho Luka anatuonesha jinsi
Yesu alivyotekeleza utume huo kwa kuwaendea watu waliohitaji kusikia Habari
Njema ‘…ikawa baada ya hayo alikuwa akizungukazunguka katika miji na vijiji
akihubiri na kutangaza habari njema...’ (Lk. 8:1).
Pia Injili
inaonesha kuwa Yesu alikutana na watu aliowafundisha katika mahali pao pa sala
‘ikawa siku moja alipokuwa akifundisha watu hekaluni na
kuhubiri watu habari njema (Lk.20:1).
Kutokana na mifano hiyo, tunahitimisha kuwa
waandishi wa Injili wanasema wazi kuwa Katekesi ni kufundisha, kuhubiri, kutangaza,
kushirikisha na kufahamisha.
Katika Kitabu cha Matendo ya Mitume
tunasikia habari za Mitume waliokuwa wakifundisha kwa mdomo. Mfano, katika
tukio la Pentekoste ya kwanza Petro kwa ujasiri alisimama na kutangaza wazi
Fumbo la Ufufuko wa Bwana tunasoma ‘…Petro akasimama… akapaza sauti yake
akawaambia…’ (Mdo 2:14- 36).
Pamoja na mitume kuna wengine waliojitokeza
pia kushirikiana nao katika kuitangaza Habari hiyo Njema ya wokovu mmoja wapo
ni yule Apolo myahudi wa Iskanderia aliyeishi kule Efeso kama tunavyosoma ‘…huyo alikuwa amefundishwa njia ya Bwana; na
kwa kuwa roho yake ilikuwa ikiwaka alianza kunena na kufundisha kwa usahihi
habari za Yesu, naye alijua ubatizo wa Yohani tu (Mdo 18:25).
Pia
Paulo mwenye anathibitisha kuwa alishiriki utume wa mkatekista katika Kanisa la
mwanzo kama anavyosema ‘sikujiepusha katika kuwatangazia neno lolote liwezalo
kuwafaa, bali niliwafundisha waziwazi nyumba kwa nyumba (Mdo 20:20). Na katika katika nyaraka zake, Mtume Paulo anasema wazi, ‘basi sisi tunamhubiri Kristo aliye
sulubiwa’ (1Kor.1:23). Na anaongeza
kusema kuwa aliitenda kazi hiyo kwa ushirikiano na wengine ‘...maana Mwana wa Mungu Kristo Yesu
aliyehubiriwa katikati yenu na sisi yaani mimi na Silwano na Timotheo...
katika Yeye ni ndiyo. (2Kor.1:19).
Pamoja na mtazamo huo wa kibiblia, bado
kuna wataaalamu mbalimbali wamejaribu na wanendelea kujitahidi kulielezea neno Katekesi
kadiri ya mitazamo yao. Katika ujumla wao wengi waliiona katekesi kuwa ni tendo,
kazi au shughuli zote zinazofanywa na Kanisa ili kufanikisha ufahamu wa
binadamu katika kujua ufunuo wa kimungu. Wanaowakilisha mtazamo huu wa katekesi
wanasema yafuatayo.
Katekesi
ni kila tendo linalofanywa ndani ya Kanisa ambalo linamshirikisha
binadamu Neno la Mungu kikamilifu katika mazingira ya maisha yake (Van
Caster). Shughuli inafanywa
na Kanisa ili kumwingiza binadamu aone kazi ya Mungu ya ukombozi. Katekesi ni
shughuli inayomshuhudia Kristo ikitangaza Neno lake na Utume wake wa wokovu wa
mwanadamu. Katekesi ni tangazo la ujumbe
wa maisha ya Kristo, na ni elimu ihusuyo imani hai, tena ni mwanzo wa kuingia
katika maisha ya Kanisa. Katekesi ni kazi ya kufunua mwito wa Mungu kwa
binadamu aweze kutambua mwito wa upeo na mwitikio kwa njia ya imani iliyo Imara (Audinet
1974).
Maisha
ya kushirikishana kiimani na waamini wapya katika Kanisa (Jean Danelou); Mafundisho
juu ya Imani ya kikristo (J.A. Jungman). Katekesi katika
mwelekeo wa kimystagojia inamaana ya kuelekeza kwa kina mafundisho ya dini
baada ya ubatizo (A. Liege). Katekesi
pia humaanisha maelezo na tafsiri juu ya Tangazo la awali la Habari njema (Kerygma)
anayopewa mtu ili kuendeleza ujuzi wake hata elimu ya dini (J. Colombo).
Nia
ya katekesi ni kuamsha na kuchochea imani mioyoni mwa watu pia ni kusisimua
binadamu ili aishi maisha yaliyonyooka kiimani (Nijmegen School).
Kwa nyakati zetu tafsiri sahihi na ya kina
ya neno katekesi ni ile iliyotolewa na Mamlaka ya Ufundishaji ya Kanisa
(Magistero) katika Katekisimu ya Kanisa Katoliki. Katekisimu hii inaeleza kuwa katekesi ni jumla ya jitihada zote za makusudi
na njia zote za Kanisa Katoliki za kuwatafuta, kuwaunda, kuwaingiza na
kuwakomaza waamini wake (wapya na wale waliotayari waamini tangu zamani) katika kuwasaidia kuamini kweli
kuwa Kristo ni Mwana wa Mungu na kwa imani hiyo wapate uzima wa milele kwa njia
ya Yesu Kristo.
Hii ina maana kuwa Katekesi ni jitihada na
njia zote za kimpangilio za kuwatafuta, kuwafundisha na kuwaelimisha watu
katika Imani ya kikristo na za kuujenga mwili wa fumbo wa Kristo yaani Kanisa
ambalo ndilo Sakramenti ya wokovu katika maisha ya hapa duniani.
Na hii inatufanya sisi kuelewa kuwa
Katekesi ni shule na elimu katika imani kwa watu wote na wa nyanja zote kuanzia
watoto na vijana wote na pia kwa watu wazima ndani na nje ya familia.
Kwa kuwa katekesi ni elimu basi ni lazima
itolewe kwa mpangilio na utaratibu wa hatua kwa hatua mpaka mwisho ili
kuwaingiza wamini katika ukamilifu wa maisha ya kikristo, kwa kufuata kwa
makini na uaminifu muhtasari wote wa mafundisho ya Imani ya Kanisa ulio kwenye
kitabu/kijitabu tukiitacho Katekesimu -hasa ile maarufu kama (KKK 4-6).
Comments
Post a Comment