‘Utajiri usiwasahaulishe Mungu,’ waamini watahadharishwa
MOROGORO, Askofu Telesphor Mkude wa Jimbo Katoliki
Morogoro amesema kuwa mali na utajiri si kigezo au sababu ya kumsahau mwenyezi
mungu kama ilivyo desturi ya baadhi ya watu wanaomsahau wanapopata mafanikio.
Amesema hayo
wakati wa kutoa Daraja Takatifu la Ushemasi kwa Mashemasi watatu wa shirika la
Mtakatifu Vicenti wa Msalaba iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Patris
jimboni Morogoro.
Askofu Mkude
amesema kuwa ni watu wachache ambao wanamuweka mbele Mwenyezi Mungu wanapopata
mafanikio katika nyanja mbalimbali, isipokuwa wengi wao wanamsahau Mungu kabisa
na kutawaliwa na utajiri unaowazunguka.
“Watu wachache
ambao wamekuwa wakimuweka Mungu mbele wanapopata mafanikio katika nyanja
mbalimbali maishani mwao huku wengi wao wakimsahau kabisa na kutawaliwa na
utajiri unaowazunguka pia husahau walipokuwa wakitafuta walipiga goti ili
wapate, kwa vile wamepata hawana budi waendelee kumshukuru Mungu ili aendelee
kuwabariki na kulinda kile walichobarikiwa,” amesema Askofu Mkude.
Aidha amesema
kuwa watawa ni mfano bora wa kuigwa katika maisha kutokana na kazi na majitoleo
yao katika huduma za jamii bila ya kudai ujira na maslahi bali wanafanya kazi
zao kwa utii na unyenyekevu kwakuwa ni wito huku wakiendelea kumshukuru Mungu
katika utawa wao.
“Watawa ni mfano
wa kuigwa kwakuwa wamejitoa sadaka kwa Mungu ili wahudumie watu kiroho na
kufanya shughuli nyingine za kijamii kwa kujitoa pasipokudai ujira wowote,
naamini haya yote wanafanikisha kwa kumtanguliza Mungu kwa walichokifanikisha,
wanachofanya na wanatakachofanya hawachoki kumshukuru na kumuomba katika kila
hatua yao, nami nawatia moyo katika hilo na wasikate tamaa katika kuitenda kazi
ya Bwana kwakuwa mavuno ni mengi ila watenda kazi ni wachache,” amesema Askofu
Mkude.
Hata hivyo
kiongozi huyo wa kiroho amesema kuwa si vibaya kuwa na mali na utajiri katika
dunia, bali mali na utajiri zitumike kwa unyenyekevu ili iwe njia pekee ya
kuwasaidia wahitaji mbalimbali ambao Mwenyezi Mungu anawatizama kwa jicho la
huruma.
Mbali na hayo
Askofu Mkude ametoa pongezi kwa mashirika mbalimbali ya kitawa jimboni humo,
kutokana na mchango wao katika huduma za kiroho kwa waamini, ambazo zinaendelea
kuwa kivutio katika jimbo katoliki Morogoro
Shirika la
Mtakatifu Vicenti wa Msalaba mpaka sasa lina miaka zaidi ya 300 tangu
kuanzishwa kwake, likiwa na mwendelezo wa huduma za kiroho katika sehemu
mbalimbali za dunia zinazotolewa na mapadri na masista katika kulitegemeza Kanisa
la Mungu.
Comments
Post a Comment