‘Ukame siyo mpango wa Mungu, tumejitakia’ Ask. Amani
ASKOFU
wa Jimbo Katoliki Moshi Mhashamu Isaac Amani amesema kuwa athari za mabadiliko
ya tabia nchi, kama ukame na mlipuko wa magonjwa, ni matokeo ya uzembe wa mwanadamu
katika kuhifadhi mazingira.
Ameeleza hayo hivi karibuni
alipokuwa anafungua Mkutano wa Kitaifa wa Wakurugenzi wa Idara na Vitengo
vilivyopo chini ya Kurugenzi ya Uchungaji, uliofanyika katika Baraza la
Maaskofu Katoliki Tanzania na kuhudhuriwa na wakurugenzi kutoka majimbo
mbalimbali katoliki nchini.
“Kutunza mazingira na usafi ni
amri ya Mungu. Tumepewa jukumu la kuhifadhi uhai kwa kuyatunza mazingira,
tukizembea jukumu hilo tunaonja athari za mabadiliko ya tabianchi. Athari hizi
tunatengeneza sisi, siyo mpango wa Mungu” ameeleza Askofu Amani.
Wakati huo huo Askofu Amani
amesema kuwa, katika kusherehekea Jubilei ya miaka 150 ya uinjilishaji na miaka
100 ya Upadri Tanzania, ni lazima kuweka mkazo wa kuinjilisha katika familia za
kikristo.
Amesema kuwa nafasi ya familia
na jumuiya katika uchungaji ni kubwa na kwamba nafsi ya mtu hujengeka na
kuponywa katika familia.
“Kanisa linaadhimisha zawadi ya
umri wa miaka 150 ya imani Katoliki Tanzania. Neno la Mungu lijenge tamaduni
mpya katika familia, kwani familia yenye nguvu na mshikamano hustawisha taifa”
ameeleza.
Pia ametoa wito kwa waamini
nchini kutumia maadhimisho ya miaka 150 ya uinjilishaji na miaka 100 ya upadri
Tanzania kwa kufanya hija katika maeneo ya kihistoria. Amesema kuwa kufanya
hija kunawaunganisha waamini pamoja na matukio ya zamani yanayowaimarisha
kiimani.
Comments
Post a Comment