Mwanadamu na serikali
KWA kawaida vijana hawakumbuki
ya kwamba kuna Serikali mpaka labda siku wanapodaiwa kodi. Hapo hufumbuka macho wakiwaza “Serikali
inataka nini nami? ina haki gani initoze kodi? Kwa kweli Serikali itasema mara kwa
mara neno katika maisha yako. Afadhali ufahamu kidogo maana ya Serikali na
uhusiano ulio nayo.
Tuone Utawala wa Wazee zamani
Kama
ungalizaliwa wakati wa babu zako, maisha yako yangalipangika tofauti na sasa.
Zamani watu wote walikaa kama jamaa moja wakilima na kujilisha kwa mavuno ya
Shambani. Mzee wa jamaa aliwasimamia watu wake, tena aliamua magomvi. Mashauri
makubwa zaidi yalipelekwa kwake, ndiye mkubwa wa Ukoo.
Huyu
na wazee wenzake walikuwa Serikali kwa watu wao. Ingawa ukoo ulikuwa sehemu ya kabila,
wakubwa wa koo zote hawakushirikiana katika
utawala wa kabila zima, maana kila mmoja alikuwa sawa na wenzake,
akishika mamlaka kwa watu wake tu isipokuwa katika shida kubwa kama vita.
Hapo
walisaidiana kwa muda. Mpango huo ulikuwa wa kawaida kwa makabila mengi ya
Wabantu. Pengine Kabila moja moja
lilitawaliwa na Mfalme, hasa kwa makabila yaliyopenda vita. Lakini hata kwao
mashauri ya kila siku yalikatwa na mkubwa wa Jamaa.
Makabila
yalikuwa mengi sana. Kila kabila lilitafuta faida yake tu. Mara nyingi
halikupatana na Kabila la jirani. Watu
walikaa kwa shingo upande. Walishindwa kwenda mbali kwa hofu ya kukamatwa na
adui zao au kuuawa au hata kufanywa watumwa.
Biashara
au shughuli za maendeleo hazikuwa na nafasi, wala nchi haikupata nafasi ya kuinuka
na kupata maendeleo. Hali kama hiyo kwa sasa hivi haina nafasi. Tumshukuru
Mungu kwamba katika maendeleo ya siku hizi imefaa makabila yaunganike katika
taifa, kama ilivyotendeka hapa Tanzania na kusimamiwa na Serikali kuu jinsi
ilivyo.
Maana ya Serikali
Tunashukuru
kwamba Serikali haipunguzi haki za kila mtu, wala kuyachukua madarakaya
familia,ya jamaa ,ya kabila ,wala haimchagulii mtu kazi ya kufanya au dini n.k
wala haiwazui wazazi kuwapa watoto wao malezi wanavyotaka wenyewe.
Serikali
imewekwa kwa ajili ya raia, siyo raia kwa ajili ya Serikali. Kwa hiyo Serikali
yafaa ifanye bidii yoyote iwatunze raia zake na kuwapa nafasi ya kuendelea
vizuri badala ya kubakia nyuma.
Serikali iwasaidie katika nini?
Wajibu
wa Serikali iwe ni kuwasaidia raia wake katika mambo mazuri yote wasiyoweza
kuyapata kwa nguvu zao peke yao. Ni wajibu wake kutunga Sheria zitunzazo amani
na utaratibu wa nchi ili raia wakae kwa raha, kuweka mapolisi waihifadhi amani
hiyo na kuwaadhibu wakosefu wanaozivunja Sheria. Tena kuweka Jeshi la askari
walinde mipaka ya nchi yetu na kuwazuia adui wasiishambulie.
Kujenga
hospitali na kuweka Sheria za afya kama kuzuia Malaria, kifua Kikuu na Magonjwa
mengineyo, kufungua biashara, barabara, njia za gari la moshi, na kufungua
mapatano ya biashara na nchi za kigeni,
kusimamia vizuri miundo mbinu yote na njia zote za mawasiliano.
Serikali ina haki ya kutoza
ushuru
Kwa
kazi zote chache nilizozitaja hapo juu, Serikali inahitaji fedha, nayo
hupatikana hasa kwa ushuru na kodi za kila namna. Ni haki ya Serikali kutoza
fedha hii, kwa sababu inatumiwa kwa ajili ya raia. Hata Kanisa litakubaliana na
Serikali kama inazijali Sheria za maumbile na za Mungu.
Serikali imepata mamlaka kwa
Mungu
Jamaa
haitoshi ijipatie mafaa yote jinsi ipasavyo, wala haiwezi kulinda amani na
kuinua nchi jinsi itakiwavyo. Kwa mambo hayo inahitajika taifa na Serikali kuu
kama nyongeza yake. Mungu mwenyewe ametaka taratibu hiyo alipothibitisha Sheria
ya maumbile kwa amri zake kumi. Alizitangaza kwa fahari nyingi, ili watu
wakiona enzi yake wazidi kuzishika, soma katika kitabu cha pili cha Musa, sura
ya 19 na 20 katika Agano la Kale.
Kwa
hiyo ndugu msomaji wa makala haya, uwezo wa Serikali wategemea Mungu, na
wakubwa wa Serikali wamepata kwake haki yao ya kutawala. Maneno hayo
yamethibitishwa katika maandiko
matakatifu. Pilato alipomwambia Yesu, “ Hujui ya kuwa nina mamlaka ya kukusulubisha
na mamlaka ya kukufungua? Alijibu, “Hungekuwa na mamlaka yo yote juu
yangu kama hungepewa kutoka juu,” Soma Yohane 19: 10-11.
Utii
kwa Serikali ni muhimu kwa sababu kuna msingi wake. Mtume Paulo ameandika hivi:
“Kila
mtu aitii mamlaka ya wenye kutawala, kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa
Mungu. Basi, anayekataa kuitii mamlaka anashindana na agizo la Mungu, lakini
wenye kushindana nalo wajipatia hukumu” Warumi 13:1-2.
Kwa
kuwa wakubwa wa Serikali wamepata mamlaka yao kwa Mungu, hawawezi kutawala
jinsi wapendavyo, bali imewapasa kuzijali amri za Mungu na kutawala kwa kadiri
yake. Haifanyi tofauti kama wamerithi cheo au wamechaguliwa na raia wenyewe.
Mwisho watahukumiwa na Mungu.
Mara
kwa mara kuna watawala wabaya wasiomtii Mungu. Hao wataadhibiwa na Mungu.
Lakini raia wana lazima wawatii ispokuwa huamuru neno lililokatazwa na Mungu,
kwa maana wanashika mamlaka kwa haki ijapo wanaishutumu.
Watawala,
ambao Mtume Paulo amewaambia wakristo wake wawatii, walikuwa wapagani wenye
mazoea mabaya. Yesu amesema. “ Yo yote watakayowaambia yashikeni na
kuyatenda, lakini matendo yao msiyafuate” Mt 23:3. Wakristo wa zamani
waliwatii hata watawala wadhulumu katika mambo yote ya Serikali, ila walikataa
kukana dini au kutenda yaliyokatazwa na Mungu.
Kwa
hiyo ni wajibu wetu kuitii Serikali kwa ajili ya Mungu, siyo kwa hofu ya
kukamatwa. Ukifikiri, sitalipa kodi nikipata nafasi ya kutolipa, wala sitazishika
amri nyingine za
Serikali
nikiona njia za kuziepuka, huna maono ya kikristo. Kumbuka kuwa hupatwi na kosa
tu unapokamatwa bali kuivunja Sheria kwenyewe ni kosa. Mtume Paulo ameandika
hivi. “ Hamna
budi
kuinyenyekea Serikali siyo kwa ajili ya adhabu tu, lakini pia kwa ajili ya
dhamiri…….. Basi, wapeni wote yawapasayo, kodi astahiliye kodi, Ushuru,
astahiliye ushuru, hofu astahiliye hofu, heshima astahiliye heshima “ Warumi
13:5-7.
Kodi
na Sheria zote za Serikali zimewekwa kwa ajili ya mafaa ya watu wote. Ndugu
yangu unapozivunja hizo unakosa amri ya
4 ya Mungu inayotudai kuwaheshimu baba na mama, ili upate miaka mingi na heri
duniani. Tena na amri kuu ya mapendo, maana unawanyima wenzako haki yao.
Mwandishi
ni Padri wa
Kanisa
Kuu JIMBO
Katoliki
– KIGOMA.
Comments
Post a Comment