Sababu za maelfu kuukimbilia ushirikina
SWALI: Padri, kuna viongozi wengi nchini,
wakiwamo wa dini, wanaojilinda kwa ulozi. Wewe unasemaje juu ya jambo hili? Hii
si aibu kwetu? Swali hili limeulizwa na vijana katika akaunti yangu ya Facebook.
Jibu: Ninayo
habari na maneno ya namna hiyo ya kwamba viongozi mbalimbali, wakiwamo wa
kidini, wanaojilinda kwa ulozi. Ninyi vijana mnaniuliza juu ya maoni yangu,
lakini kwa kweli mimi sijui niseme nini kuhusu tuhuma hizo. Inabidi ufanyike
utafiti ili watu wanaojilinda kwa ulozi wahesabiwe.
Husikika kwamba
watu hutafuta uongozi kwa kuwaendea waganga wa kienyeji wanaowapa dawa za
kunywa au kujipaka pamoja na hirizi za kuvaa. Husemwa wengine huagizwa wawaue
albino au wawatoe kafara watu wa karibu nao. Kishapo husemwa viongozi wengine
wakishapata madaraka na vyeo walivyowania hujilinda kwa hirizi na kinga
mbalimbali.
Sasa, kwa kuwa
haujafanyika utafiti wowote, tuhuma hizo zinabaki kuwa tuhuma tu. Lakini
kutokana na utafiti wa mwaka 2009 wa PEW Research Center ya Washington, DC,
ulioonesha kwamba Tanzania ni nchi ya kwanza barani Afrika kwa kuamini uchawi
(kwa vile uligundua kwamba 93% ya Watanzania wanaamini katika ushirikina).
Kusema kwamba
viongozi mbalimbali, wakiwamo wa kidini wanajilinda kwa ulozi kunaweza kufanana
na ukweli. Hakika mtu anayeamini katika mambo ya kishirikina, lazima atashindwa
kujiamini kuishi pasipo kuyategemea mambo anayoyaamini.
Lakini hiyo ni
bahati mbaya sana. Wakristo tulipaswa kumwamini Mungu na kumwacha yeye atulinde.
Wala haiingii akili, mtu anayemwamini Mungu mwenyezi aamini kupata ulinzi
kutoka kwenye kipande cha mti au mzizi ulioshonewa hirizi. Mti mzima hauwezi
kumlinda mtu, sembuse gome au kipande chake cha mzizi uliokufa!
Wala haiingii
akili, mtu anayemwamini Mungu mwenyezi aamini kupata ulinzi kutoka kwenye jino
la nguruwe au kutoka kwenye kipande cha mkia wa kenge aliyekufa. Nguruwe mzima
au kenge mzima hawawezi kumlinda mtu, sembuse meno yao au mikia yao
iliyokaushwa! Tena ni kinyume kabisa cha matazamio ya Mungu. Mungu alituamuru
tukavitawale viumbe vyote, kumbe badala yake tunatawaliwa navyo! Ndivyo
tunavyosoma kwenye Biblia.
Sikiliza
imeandikwa, “Kisha Mungu akasema,
‘Tumfanye mtu kwa kwa mfano wetu, kwa sura yetu; atawale samaki wa baharini,
ndege wa angani, wanyama wa kufugwa , dunia yote na viumbe vyote vitambaavyo.’
Basi, Mungu akamuumba mtu kwa mfano wake;
naam, kwa mfano wake Mungu alimuumba, alimuumba mwanamume na mwanamke. Mungu
akawabariki na kuwaambia, ‘Zaeni muongezeke, mkaijaze nchi na kuimiliki,
muwatawale samaki wa baharini, ndege wa angani, na kila kiumbe hai kitembeacho
duniani’” (Mwa 1:26-28).
Sasa inakuwaje
binadamu kushuka hata kuhangaishwa na ndege kama bundi, sisimizi, panya, mende
na kadhalika na si kukomea hapo bali kwenda mbali zaidi na kuamini kwamba
viumbe hivyo, mifupa yao au ngozi zao zinaweza kuwapa ulinzi kumpita
Mungu?
Hapo ndipo
inapoingia aibu kwa shughuli zima za kutafuta bahati na ulinzi wa kishirikina
au ulozi Hilo la kujilinda kwa vitu vya ziada vya kishirikina wenyewe wanaita
siku hizi “ulinzi shirikishi”. “Ulinzi shirikishi” si sawa na ni kazi bure kwa
maana Mungu ndiye mlinzi halisi na chochote tunachofanya kilitakiwa kiwe chini
ya usimamizi na baraka zake.
Si kwamba tusema
wanadamu tukae na kusubiri kulishwa kama kuku zizini, la hasha. Kuna upande
wetu na kuna upande wa Mungu katika utendaji wetu. Kwa upande wetu tulitakiwa
kujiamini na majaliwa aliyotupatia yatusaidie maishani, yaani vipaji vya akili
na utashi na karama au talanta zetu mbalimbali (1Kor 12-14).
Ndivyo
inavyopasa kutendeka, sisi tutumie akili na utashi na neema tunazopata kutoka
kwa Mungu na yeye abariki nia na kazi zetu. Nasisitiza kusema ndivyo ilivyopasa
kufanyika kwani tumeandikiwa ifuatavyo: “Mwenyezi
Mungu asipoijenga nyumba, waijengao wanajisumbua bure. Mwenyezi Mungu
asipoulinda mji, waulindao wanakesha bure. Mnajisumbua bure kuamka mapema
asubuhi na kuchelewa kwenda kumpumzika jioni, mjipatie chakula kwa jasho lenu.
Mungu huwazuruku walio wake hata walalapo” (Zab 127:1-2).
Kumbe, kweli
tunajiaibisha mbele ya Mungu na mbele ya wenzetu, kwa kuamini kwetu mambo ya
ushirikina na ulozi. Mungu anatushangaa na bila shaka atatuadhibu kwa kupindua
alichotupangia kiwe. Anapika dawa yetu, ikiiva atatunywesha. Tutakiona cha
mtema kuni kilichomtoa khanga manyoya huko mwishoni mwa maisha haya. Basi, ole
wetu. Tuache kuyategemea mambo hayo na kwa kweli aliyakataza.
Tusisahau
tulivyopigiwa marufuku kujihusisha na mambo ya kishirikina katika Kum 18:9-13.
Tumeandikiwa, “Mtakapofika katika ile nchi niwapayo
Mwenyezi Mungu, Mungu wenu msifuate zile tabia za kuchukiza za mataifa ya huko.
Asiwepo mtu yeyote miongoni mwenu atakayemchoma mtoto au mwanawe wa kiume au wa
kike kuwa tambiko, wala mtu apigaye ramli, wala mwaguzi, wala mpiga bao, wala
“mcheza mazingaombwe” ya kudhuru, wala mlozi, wala mwenye kutaka kauli kwa
mizimu na pepo au kutoka kwa wafu, maana yeyote atendaye mambo haya.
Mambo haya ni chukizo kwa Mwenyezi Mungu na
kwa ajili ya mambo haya ya kuchukiza Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawafukuza
watu wa namna hiyo mbele yenu. Muwe wakamilifu mbele ya Mwenyezi Mungu, Mungu
wenu”.
Watu wa mataifa
mengine wanatuonea huruma Waafrika wote kwa sababu hatutaki kubandukana na
mambo ya imani ya kishirikina. Wenzetu wengi walishabandukana nayo na wala hawajala
hasara yoyote. kwa upande wetu hatutaki kubandukana nayo na wala hatupati faida
yoyote. Kwa nini tusivae ushujaa wakuachana na kitu ambacho hakituletei faida
wala hasara tuliachana nacho?
Baba Mtakatifu
Benedikto XVI akituonea huruma alituusia kwa maneno haya: “Uchawi, ambao msingi wake
ni dini za jadi, kwa hivi karibuni hutiwa tena nguvu. Woga wa zamani unaibuka
tena na unatengeneza pingu poozeshi za kutojiamni. Wasiwasi kuhusu afya,
ustawi, watoto, hali ya hewa, na kujikinga na pepo wabaya mara nyingine
husababisha watu kukimbilia kwenye mazoezi fulani ya dini za jadi za Kiafrika
ambayo hayapatani na mafundisho ya Kikristo.
Tatizo
la ‘kujisajili kuwili’ – kwenye Ukristo na kwenye dini za jadi za Kiafrika –
linabaki ni changamoto. Kwa njia ya katekesi na utamadunisho wa kina, Kanisa
huko Afrika linahitaji kuwasaidia watu kugundua ukamilifu wa tunu za Injili. Ni
muhimu kuweka wazi maana ya kina ya mazoezi haya ya ushirikina kwa kuainisha
mambo mengi ya kiteolojia, kijamii na kiuchungaji yanayohusu janga hili” (Africae Munus na. 93).
Lakini ajabu ni
kwamba Waafrika wengi hatuyajui mausia haya na wala hatujali. Eti huko mbele ya
safari Waafrika tutakapotupwa motoni kwa kuamini na kuendesha maisha kwa imani
za kishirikina tutashangaa!
Imetangazwa kabisa
tutaadhibiwa na hatutaonja ufalme wa Mungu tukibaki katika uongo wa kishirikina
bado hatutilii maanani jambo hilo (rej.
Gal 5:19-21). Sisi bwana! Kwa herini kwa sasa!
Comments
Post a Comment