Kimbiji wasali kwenye banda la miti
WANAJUMUIYA ya Mtakatifu Yohane Mbatizaji
Kijaka Parokia ya Kimbiji jijini Dar es salaam wametakiwa kutokata tamaa
kutokana na mazingira magumu ya kuabudu.
Rai hiyo imetolewa na Padri Thomas Laurent
baada ya kuwatembelea wana jumuiya hao siku ya Dominika na kushuhudia mahali
wanapoabudia ambapo ni banda la miti
lililopo katikati ya pori lililo wazi na kuezekwa kwa minyaa.
Wakizungumza na gazeti la Kiongozi
wanajumuiya hao wamesema ni kwa mda mrefu sasa wanasali katika kibanda hicho na
hali hiyo inatokana na umbali mrefu uliopo kati yao na Parokia. Wamesema
inawachukua takribani saa saba kutembea mpaka Parokiani jambo lililowapa ugumu
na wakaamua kujenga banda hilo ambapo Padri hufika eneo hilo kwa gari kwa ajili
ya Misa ya Ibada Takatifu.
Naye mwenyekiti wa jumuiya hiyo Bi .Paulina
Jeremia ameliambia gazeti la Kiongozi kuwa, wazo la kujenga banda hilo la
kuabudia limeokoa waamini wa Jumuiya hiyo waliokuwa kwenye hatari ya kubadili
imani yao kutokana na umbali na ugumu wa kushiriki katika ibada. Jumuiya hiyo
yenye waamini zaidi ya 25 bado haijatambulika kuwa Kigango japokuwa ina kila
kitu cha kutambuliwa kama Kigango.
Aidha Padri Thomas amezitaka Parokia na watu binafsi ndani ya Kanisa
kuwasaidia wanajumuiya hao ili wapate mazingira mazuri ya kuabudia na pia
amewataka waamini hao kujikwamua kwa hali na mali ili wapate kujenga angalau Kanisa
dogo la matofali kwa kushirikiana na wadau (waamini) kutoka parokia nyingine.
Comments
Post a Comment