Kard. Pengo: Bikira Maria ni matumaini ya amani ulimwenguni
ASKOFU
Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo
amesema kuwa Bikira Maria ni chimbuko la Baraka na matumaini ya amani, siyo tu
kwa taifa la Tanzania, bali kwa ulimwengu mzima.
Ameeleza hayo hivi karibuni
katika uzinduzi wa Groto ya Bikira Maria, uliofanyika katika Ofisi za Makao
Makuu ya Radio Maria Tanzania, Mikocheni, jijini Dar es salaam, na kuwataka
waamini kutoka sehemu mbalimbali kutumia Groto hiyo ili kujichotea za Mungu
kupitia maombezi ya Mama Maria.
“Natumaini na ni ombi langu
kwenu kuwa Grotto hili halitakaa bure. Wale wote tuliopo hapa na wale waliopo
popote, mtakapopata nafasi ya kutembelea Makao Makuu ya Radio Maria Tanzania,
msikose kupita hapa kumsalimia huyu Mama. Huyu Mama ni chimbuko la neema,
chimbuko la Baraka na ni matumaini ya amani, siyo tu kwa ajili ya Taifa letu bali kwa ulimwengu mzima.
Tumtembelee na tumuombe amani kwa ajili ya ulimwengu wote” ameasa Kardinali
Pengo.
Aidha Kardinali Pengo
amewashukuru waamini kutoka sehemu mbalimbali ambao wamefanikisha kukamilika
kwa Groto hiyo kupitia michango yao ya hali na mali. Ameongeza kuwa hata uwepo
wake katika kushuhudia uzinduzi huo umetokana na Baraka za Mungu kupitia kwa
Mama Maria.
“Siku ya leo ni ya kumbukumbu
kubwa kwa Radio Maria Tanzania na ulimwengu mzima. Tunawashukuru wale wote,
waliochangia kwa namna moja ama nyingine kutengeneza Grotto ya Mama Bikira
Maria. Mimi namshukuru Mungu na Mama
Maria kwa namna ya pekee ambaye ameniwezesha kuwa hapa pamoja nanyi, kwa sababu
kulikuwa na vizuizi na matatizo mengi ambayo yangeweza kunifanya nishindwe
kuhudhuria” ameeleza.
Kwa upande wake Rais wa Radio
Maria Tanzania, amewashukuru wote waliojitoa na kufanikisha kukamilika kwa
Groto hiyo, huku akitoa mwaliko kwa waamini kuitumia Groto hiyo kuomba Baraka
za Mungu kw maombezi ya Mama Maria.
“Tunapenda kuwashukuru wote
waliojitoa kwa hali na mali katika kufanikiha ujenzi huu. Tunawakaribisha
wafike hapa Mikocheni kwa ajili ya kujichotea neema na Baraka za Mungu kupitia
Mama yetu Bikira Maria” amesema.
Naye Mkurugenzi wa Radio Maria
Tanzania Padri John Maendeleo amesema kuwa ujenzi wa Groto hiyo umewezeshwa na
michango ya waamini kutoka maeneo mbalimbali, huku akitoa rai kwa watu wote
kuitumia Groto hiyo kwa ajili ya kuomba Neema na maombezi ya Mama Maria.
Comments
Post a Comment