KUJITEGEMEA HAKUEPUKIKI-KITIMA
Na Bernard James, Dsm
Watanzania wametakiwa kuishi kivitendo falsafa ya elimu ya
kujitegemea kama ilivyojengwa na Baba wa
taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ili kuliletea taifa maendeleo ya kudumu
kwa vizazi vyote.
Akiongea na gazeti hili jijini Dar es salaam makamu mkuu mstaafu
wa chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino Tanzania
dokta Charles Kitima amesema falsafa(mtindo wa kufikiri) ya elimu hiyo
itasaidia kizazi cha sasa na kijacho kujitawala kisiasa, kiuchumi na
kiutamaduni na hivyo kudumisha uhuru wa Taifa huru la Tanzania ambapo raia wake
huishi kama ndugu.
Amesema Mwalimu Nyerere alihakikisha elimu ya kujitegemea
inaleta maendeleo kwa kila aipataye, kujijengea maaarifa na utaalamu, kutatua
matatizo kitaalamu, na ilimfikia kila mtanzania katika eneo lake pasipo na ubaguzi wowote.
“Tunahitaji falsafa ya elimu ya aina hii kwakweli, ili
wasomi na raia wote kwa ujumla wawe na
uwezo wa kufikiri na kupambanua masuala mbalimbali kwa uelewa mpana”. Dokta Kitima
amesisitiza.
Amesema japokuwa katika miaka ya 1970 mfumo wa elimu ya
kujitegemea ulikuwa na lengo la kumfikia kila mtu na kumwezesha kupambana na
maadui watatu ambao ni ujinga, umaskini na maradhi lakini ulipata changamoto
kadhaa zikiwemo upatikanaji wa walimu bora na mazingira ya ufundishaji, bado
elimu hiyo iliweka misingi bora ya kujenga taifa la watu wanaoamini kuwa
maendeleo ya kweli yanahitaji watu huru, ardhi, siasa safi na uongozi bora.
“Kipindi kile elimu iliwaandaa watu ili wajitawale, wasaidie
kuleta maendeleo na ilitolewa kwa kila aliyestahili jambo lililowafanya
wanufaika wa elimu kuhangaika huku na kule kuliletea taifa mafanikio makubwa
wakikumbuka kuwa taifa liliingia gharama kubwa kuwasomesha ndani na nje ya
nchi”.
Dokta Kitima amesisitiza pia kuwa elimu ya kujitegemea
ilihakikisha inamwandaa mwanafunzi ajifunze vizuri ili aweze kumudu maisha na
kujipatia mafunzo ya juu tofauti na hali ilivyo sasa ambapo kwa kiwango kikubwa
kinachoangaliwa ni ufaulu wa mitihani wa mwanafunzi.
“ Kwenye utawala wa Mwalimu Nyerere wazazi ambao ni wadau
wakubwa katika elimu walipewa nafasi na walishirikishwa kupitia uwakilishi
unaojali matarajio ya wazazi na watoto katika kuandaa sera na mifumo ya elimu
ya watoto wao tofauti na sasa ambapo serikali inasimamia kila kitu na wazazi
wakishirikishwa kidogo ama kutoshirikishwa kabisa na ndio maana kila waziri
huja na mambo yake. Hii ni kutokana na serikali kutokuzingatia falsafa ya Taifa
juu ya kujitawala kwetu” Amesisitiza.
Amepinga vikali tabia ya wasomi wengi wa sasa kukataa kwenda
kufanya kazi na kukaa vijijini kuwasaidia watanzania wengi waishio huko
akisisitiza juu ya malengo ya kuwatumia wasomi, akikumbusha jinsi Baba wa Taifa
mnamo mwaka 1961 wakati wa uanzishaji wa chuo kikuu cha kwanza nchini aliposema
‘ elimu ya vyuo vikuu ilenge kuwatumikia watu, na kwa vile watu wengi wapo
vijijini, basi wasomi wajipatie weledi wa kubobea ili kuinua hali ya maendeleo
vijijini’.
“Kwa sasa Serikali
inataka maendeleo vijijini, tazama inapeleka pesa nyingi huko ili ziwasaidie
wananchi kuinua hali ya maisha katika
kilimo, maji, miundombinu, elimu na afya lakini pesa hizo badala zikasimamiwe
na wasomi wetu tuliotumia gharama kubwa kuwasomesha, zinasimamiwa na viongozi
katika ngazi za chini kabisa huko vijijini wasio na utaalamu wa kutosha kama wa
hawa wasomi wetu, endapo hali hii haitadhibitiwa maendeleo ya vijijini yatakuwa
ni ndoto”.
Akizungumzia utendaji wa serikali ya sasa maoni yake ni kuwa serikali ya Rais
John Joseph Magufuli imeonyesha ishara
nzuri za kuirejesha elimu ya kujitegemea mfano harakati za kutatua matatizo
katika sekta ya elimu nchini hasa katika
kuweka mazingira rafiki ya watoto kufikia shule ya sekondari na kujifunza,
mikopo vyuo vikuu, upatikanaji wa madawati, maabara na kadhalika vyote
vimefanyika kwa jitihada kubwa ili kumfanya kila mtanzania apate elimu na
imsaidie katika kuliletea taifa maendeleo.
`Pamoja na jitihada hizo, serikali inapaswa kwa umakini na
uzalendo kujifunza kushirikisha wadau wa elimu ya msingi na sekondari ili mkazo
wa kuwa na walimu wazuri na ufundishaji mzuri wa kumwezesha mwanafunzi
kujifunza vizuri(emphasis should be on excellence in teaching and learning)’,aliongezea
dokta Kitima.
Cha kuangaliwa ni: je ufundishaji na
weledi wa waalimu unakidhi vigezo?, mazingira ya kujifunzia ni rafiki?,
je, vifaa na vitabu vya kiada, maabara , wanafunzi wa sekondari za kata
wanapata mlo wa mchana ili waweze kumudu masomo kwa siku nzima , na je wazazi
wanachangia kiasi gani kuisaidia serikali kutoa elimu msingi? Hayo na mengine vipo vya kutosha?, haya ndiyo yanayotakiwa ili
kuifanya falsafa ya hayati Mwalimu ya elimu ya kujitegemea irejee katika
historia ya Tanzania.”
Zaidi ya hapo dokta Charles Kitima ametahadharisha kuwa
falsafa ya elimu ya kujitegemea ya Baba wa Taifa inaweza kufutika hasa kwa
vizazi vijavyo endapo watanzania hawataendeleza kupitia mfumo wa elimu, mambo
ya msingi yaliyoliletea taifa uhuru na misingi ya taifa( founding Principles of Tanzania)
iliyolijenga taifa ambayo ni: Mshikamano wa Kitaifa, Umoja na Amani ,Hisitoria yetu ,Utamaduni wetu(mf.lugha ya Kiswahili ) na falsafa ya Kujitegemea.
“ Nchi nyingi zilizoendelea haziwezi kuchezea mambo(founding
principles) yaliyozipatia uhuru na kuudumisha, sisi pia tunatakiwa
kuienzi misingi hiyo hasa elimu ya kujitegemea, nashauri misingi hii iwekwe
katika mitaala ya elimu katika ngazi ya msingi, sekondari na vyuoni, pia walimu waisome na kuielewa vizuri misingi
hii kabla ya kuwafundisha wanafunzi wao”
Dokta Kitima amesema hayati
waziri mkuu Edward Moringe Sokoine
alipambana na rushwa na kwa sasa taifa limepata kiongozi mwingine anayepambana
na Rushwa na ambaye utendaji wake wa kazi unazingatia misingi aliyoiasisi
hayati Baba wa Taifa huku akisisitiza wananchi wampe ushirikiano ili nchi
irejee njia ya kujitegemea na kujenga
uchumi wa Taifa kwa kuongozwa na falsafa ya kujitegemea.
“ Tatizo kubwa lililopo nchini mwetu kwa sasa ni watanzania wengi
kujali maslahi binafsi badala ya kukuza maslahi ya taifa. Uzoefu dunia kote
umeonyesha kuwa maskini wakiwa wengi matajiri
wachache ndani ya nchi hawatafurahia huo utajiri wao. Tabia ya kutanguliza
maslahi binafi ama utamaduni huu
hautatufikisha kwenye Tanzania ya mwaka 2025 ya uchumi wa kipato cha kati, kwa
kifupi nasema tujenge sekta binafsi ya kitanzania inayoshirikiana na serikali
kujenga utajiri wa nchi yetu.”
Makamu mkuu huyo mstaafu wa SAUT ameshauri pia suala la sekta binafsi ya
kitanzania nchini lipewe kipaumbele na liingizwe kwenye mitaala ili kuliletea taifa mafanikio
makubwa kiuchumi kama yalivyo mataifa mengine.
Akigusia mapungufu ya
zamani kitaifa amesema tofauti na miaka ya nyuma ambapo mkazo uliwekwa
zaidi kwenye sekta ya umma, sasa ili kuendana na mfumo wa uchumi wa soko huria,
taifa haliwezi kuwa tofauti na mataifa mengine, wazalendo wapewe fursa na
kuzitumia fursa zilizopo hasa kwenye uwekezaji . Serikali licha ya kusimamia na kuratibu, pia
iweke mazingira mazuri na kuwajengea uwezo kiteknolojia na kimtaji wa wekezaji
wa Kitanzania hali ambayo itawajengea raia wanaothubutu uwezo wa ushindani na
sekta binafsi za mataifa ya magharibi na Asia.
Pia amesisitiza kuwa hali hii ndio pekee itakayokuza uchumi
kwa haraka. Anawaaminisha watanzania kuwa sekta binafsi ya raia unayoratibiwa
vizuri na serikali itakuza ajira na uwezo wa ushindani wa biashara na teknolojia kimataifa.
“ Nchi zilizowekeza katika sekta binafsi za raia wao
zimepiga hatua kubwa hasa katika kujitafutia masoko ya bidhaa zao, wananchi kuuza
wenyewe katika masoko ya dunia, kuwa na mazao na bidhaa zinazomudu ushindani; kwa
hiyo sisi tusihangaike kutazama wawekezaji wa nje tu kuwa ndiyo wawekezaji , wakati hata hapa nyumbani wapo wa
kutosha tukiwajengea mazingira ya mazuri , hayo yakitiliwa mkazo tutakuwa kama
nchi zingine zinazoanza kupiga hatua mfano
ni Rwanda katika zao la kahawa na
maziwa; Kenya katika utalii, chai na usafiri wa anga.
Tanzania ikijipanga vizuri na kurejea kujiamini na kurejesha
falsafa ya kujitegemea, tunao uwezo wa kuwa na sekta binafsi ya kitanzania
itakayoshirikiana na serikali kushikilia utajiri wa Tanzania, ambao utabaki
ndani kwa asilimia kubwa ukirithishwa kizazi hadi kizazi kuliko sasa
unaposombwa na sekta binafi za mataifa ya nje. Hivi ndivyo nchi zenye kutumia
uzalendo na falsafa ya kujitegemea zilivyofanya na zinavyofanya” , Amesisitiza .
Amesema “watanzania
wengi hawaweki utaifa mbele ndiyo maana kila tatizo la kiuchumi, kisiasa na
kijamii lenye kuhitaji utatuzi utasikia
kiongozi akisema ‘tunatafuta mwekezaji ama
mfadhili’. Akaonya falsafa dhaifu ya kujiona ili uendelee lazima mtu
atoke nje ya nchi kuja kusaidia haikuwa na nafasi kwenye uongozi wa Baba wa
Taifa.
Ni kweli tunahitaji kushirikiana na wengine bali sisi tukiwa tumeshikilia msingi wa utajiri na
uchumi wetu”.
Akihitimisha mahojiano na gazeti hili ameshauri watanzania
wanapomkumbuka Baba wa Taifa kila mwaka na kurudia rudia wosia wake kwenye
hafla mbalimbali wawe wa kweli kwenye misingi ya utaifa na hasa kwa yale aliyoyaamini kisiasa,kiuchumi
na kiutamaduni kama yeye mwenyewe
alivyoyaainisha katika hotuba yake ya Mei Mosi 1995, Mbeya.
Ameitaka serikali isikilize maoni ya wazazi, wasomi na
vijana katika kurejesha falsafa ya elimu ya viwango na kujitegemea.
Comments
Post a Comment