Utukufu kwa Mungu juu Mbinguni
HAPANA shaka sote tunaufahamu utenzi huo kwani
tunauimba kila Sikukuu na Dominika isipokuwa Dominika za Kipindi cha Majilio na
Kwaresima. Katika tafsiri mpya ya Kanuni ya Misa kumekuwa na mabadiliko ambayo
tungependa kuyaelezea katika makala haya.
Utenzi wa Doksolojia
Awali
ya yote tuufahamu mfumo wa utenzi wenyewe. Huo ni utenzi wa doksolojia.
Neno doksolojia nalo ni la kigeni; linatoka
katika lugha ya kigiriki au kiyunani ‘doksa’ maana yake utukufu. Doksolojia (kwa kiingereza doxology)
ni sala inayotoa sifa ya utukufu kwa Mwenyezi Mungu, aghalabu kwa nafsi zote tatu.
Tunazo
doksolojia mbalimbali lakini zilizo
muhimu hasa ni hizi zifuatazo: Doksolojia
ndogo, ambayo hutumika mara nyingi
katika Liturujia na hata katika Sala za Ibada mbalimbali ni: Atukuzwe Baba, na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo na sasa na siku zote na milele, Amina. Katika Liturujia, doksolojia hiyo hutumika katika kuadhimisha Liturujia ya
Vipindi, yaani katika kusali Sala ya Kanisa. Husemwa kila baada ya zaburi.
Utenzi
huo wa Utukufu kwa Mungu juu mbinguni
huitwa doksolojia kubwa kutokana na
urefu wa sala yenyewe. Pengine huitwa Utenzi
wa Malaika kwa sababu maneno ya mwanzo wa utenzi huo yaliimbwa na Malaika
wakati wa kutangazwa kuzaliwa kwake Bwana Yesu (Rej Lk 2:14).
Tena,
tuna doksolojia kuu ambayo
inahitimisha Sala Kuu ya Ekaristi wakati wa Misa. Kuhani huinua patena yenye
hostia takatifu na kalisi ya Damu takatifu na kusali: “Kwa njia yake, na pamoja naye,
na ndani yake, Wewe, Mungu Baba Mwenyezi, katika umoja wa Roho Mtakatifu,
unapata heshima yote na utukufu, milele na milele.” Waamini wote
huitikia kwa sauti ya kushangilia: Amina.
Katika
sherehe hutakiwa kuitikia mara tatu kwa kuimba: Amina, Amina, Amina. Hiyo
ni doksolojia
kuu kwa sababu inafungia Sala Kuu ya Ekaristi ambayo ni kiini cha Sala
zote katika kuadhimisha Ekaristi.
Tukirejea
kwenye utenzi wa Utukufu kwa Mungu juu mbinguni, tangu karne za mwanzo za
Ukristo, utenzi huo ni wa kumwabudu na kumtukuza Mungu. Maneno yake ya ufunguzi yaliimbwa na Malaika; una maneno yenye mkazo mkubwa katika kumtukuza,
kumpa Mungu sifa kuu, na heshima kubwa anayostahili, yaani kumwabaudu.
Kwamba
Mungu ni Mfalme mkuu wa ulimwengu ni ukweli ambao Wakristo wanauungama katika
utenzi huu pia. Mungu aliye Mfalme mwenye enzi kuu ndiye pia Baba yetu kama
Kristo alivyotufunulia na kutufundisha kusali:
“Basi ninyi salini hivi: Baba
yetu uliye mbinguni, jina lako litukuzwe, ufalme wako uje ...” (Mt 6:9).
Yesu
anapoweka mkazo kuhusu kusameheana, anasisitiza pia kwamba Mungu ni Baba
yetu aliye mbinguni: “Kwa maana
mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba
yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. Bali msipowasamehe watu makosa yao,
wala Baba yenu hatawasamehe makosa yenu(Mt 6:14-15). Mungu Baba yetu wa
mbinguni atatutendea sisi kama sisi tunavyowatendea wenzetu.
Sehemu
kubwa inayofuata ya utenzi huo hutoa sifa na utukufu kwa nafsi ya pili, Bwana
wetu Yesu Kristo. Wakristo humpa sifa na utukufu Bwana Yesu kama Mungu
anayeokoa kama jina lake Yesu linavyomaanisha. Hukiri imani
kuhusu nafsi ya Yesu kwamba ni Mwana pekee wa Baba, na kwamba siyo tu Mwana wa Mungu bali yeye mwenyewe pia ni
Mungu.
Utenzi
huo umetungwa katika msingi wa Maandiko Matakatifu ambayo humtaja Yesu kuwa ni Mwanakondoo
wa Mungu. Mtunzi ametumia jina Mwanakondoo ambalo Yohane Mbatizaji
alilitumia alipomwonesha Yesu kwa watu kama tunavyosoma katika Injili ya Yohane kwamba Yesu ni
Mwanakondoo anayeondoa dhambi za ulimwengu(
Rej Yn 1:29).
Jina
hilo kwamba Yesu ni Mwanakondoo wa Mungu hudokeza fumbo la Pasaka. Amekuwa
Mwanakondoo halisi wa Pasaka kwa sababu, kwa kufa kwake msalabani ameondoa dhambi za
ulimwengu wote. Katika kitabu cha Ufunuo,
mwandishi hulitumia mara nyingi sana jina hilo, Mwanakondoo, hasa katika
sura ya 5, 7,14 na 21.
Baada
ya kukiri imani hiyo kwamba Yesu ni Mungu anayeokoa, ni Mwanakondoo wa Mungu, ndipo
huja maombi kwamba atuonee huruma na atuondolee dhambi zetu. Tunakumbushwa kwamba katika Liturujia yatupasa
kwanza kukiri imani halafu kutoa maombi yanayojengwa juu ya imani tunayoikiri.
Kabla
ya kutoa sifa kwa Roho Mtakatifu, utenzi hutoa tena sifa na utukufu kwa Yesu
kama zile alizopata Baba. Sifa hizo ni
kwamba yeye ni Mtakatifu na ana enzi
kuu. Yesu anatawala mbinguni pamoja na Roho Mtakatifu katika utukufu uleule wa Mungu Baba.
Tafsiri mpya
Katika
tafsiri mpya tunapaswa kuwa makini sehemu zifuatazo: sehemu ya mwanzo kabisa; na
amani duniani kwa watu aliowaridhia. Katika tafsiri ya zamani tulizoea
kusema: na amani duniani kwa watu wenye mapenzi
mema. Kwa vile mwanzo wa utenzi huo ni wimbo wa Malaika, uamuzi umekuwa
kutumia neno aliowaridhia kama ilivyo katika Biblia.
Hapo
tukumbuke kwamba kuna tafsiri kadhaa za Biblia katika lugha ya Kiswahili.
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania liliamua kutumia katika Maadhimisho ya
Liturujia tafsiri ile iliyotolewa na
Chama cha Biblia Kenya na Tanzania mwaka 2004 na ikachapwa tena na Jimbo la
Bologna, Italia kwa niaba ya Baraza la Maaskofu Tanzania, 1997; Jimbo Katoliki
la Iringa lilipewa dhamana ya kuwasiliana na wachapaji. Kwa sababu hiyo pengine
toleo hilo huitwa Biblia ya Iringa.
Katika
kutoa sifa na utukufu kwa Bwana wetu Yesu Kristo tafsiri ya zamani ilisema: mwenye
kuondoa dhambi za dunia... kumbe katika tafsiri mpya sasa tunasali: mwenye
kuondoa dhambi za ulimwengu, utuhurumie; mwenye kuondoa dhambi za
ulimwengu, pokea ombi letu. Neno
ulimwengu
limetafsiriwa kutoka neno la kilatini: ‘mundus
-i’ kumbe katika tafsiri mpya neno dunia
linabaki kama tafsiri ya neno la kilatini ‘terra -ae’.
Mwishoni
mwa utenzi kuna tofauti ndogo ambayo tunapaswa kuitambua. Katika kutoa sifa za
utukufu na enzi kwa Yesu Kristo tafsiri mpya inasema: Peke yako Uliye juu kabisa, Yesu
Kristo...Kutokana na tofauti hizo Baraza la Maaskofu limechapa Kanuni
ya Misa ndogo kwa ajili ya waamini ili waweze kufuata tafsiri mpya ya Sala hizo
za Misa bila kupishana.
Tafadhali, tafadhali
Tafadhali
sana, tunawahimiza wachungaji kuwahamasisha Wakristo kujinunulia vijibu hivyo
vidogo vya Kanuni ya Misa ili wavitumie katika kushiriki Misa vizuri.
Vinapatikana katika maduka ya vitabu na hasa katika ofisi zetu za Baraza la
Maaskofu Katoliki.
Wengi
wameuliza kwa nini kutafsiri upya sala hizo? Tafsiri hiyo mpya inatolewa
kukidhi agizo la Vatikano kwa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki duniani, kuwataka
kutafsiri Sala za Liturujia kwa makini kama tulivyoeleza katika makala nyingine
huko nyuma. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania halina budi kutekeleza maagizo
hayo ya Vatikano.
Asante sana Mababa kwa ufafanuzi huu mzuri mno.
ReplyDeleteNina swali kidogo tu, kwamba ni kwanini huwa tunainama tunaposali sala hiyo ya Doxolojia ndogo yaan Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu?
Na pia ni kwa nin tunainama pale tunaposali sala iyo ya Malaika pale tunapotamka Neno Yesu Kristo "peke yako Bwana, peke yako uliye juu kabisa YESU KRISTO)?
Na piano pale tunaposali sala ya kanuni ya Imani ya Nicea tukifika kwenye maneno AKATWAA MWILI KWA UWEZO WA ROHO MT KWAKE YEYE BIKIRA MARIA AKAWA MWANADAMU" tunainamisha vichwa, KWA NINI?
Naomba kupata ufafanuzi kitoka kwenu mababa.
Nitashukuru sana na Mungu awabariki.
Hii ya tatu ni agizo limeandikwa kwa Misale kubwa ya Altare. Maanake, ni unyenyekevu wa Yesu
DeleteYa kwanza na ya pili pia ni kwa heshima ya utatu ila haijaandikwa