BENKI YA MKOMBOZI YATOA MSAADA KWA WAATHIRIKA WA TETEMEKO KAGERA
Mkuu wa Mkoa
wa Kagera, Meja Jenerali (mstaafu) Salum Kijuu akipokea msaada wa mabati na
mifuko ya simenti kutoka kwa mwenyekiti wa Bodi ya Mkombozi Commercial Bank
Plc, Method A. Kashonda ili kuwasaidia waathirika wa tetemeko la ardhi
lililotokea katika mkoa wa Kagera. Wengine kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa
benki hiyo Edwina Lupembe na Meneja wa Tawi la Bukoba, James Manyama. Picha kwa
hisani ya Executive Solutions.
Benki ya
biashara ya Mkombozi imetoa msaada wa vifaa mbalimbali kwa waathirika wa
tetemeko lililoukumba mkoa wa Kagera hivi karibuni.
Msaada huo ni
pamoja na mifuko mia mbili( 200) ya
saruji na mabati mia moja (100) ambayo utasaidia kujenga baadhi ya nyumba
zilizoharibiwa na tetemeko hilo.
Mwenyekiti wa
bodi ya benki ya biashara ya Mkombozi bwana Method Kashonda
amesema wameguswa kwa namna ya kipekee na janga hilo hivyo kuamua
kuungana pamoja na watanzania wengine kuwasaidia waathirika wote ili waweze
kurudi katika hali yao ya kawaida.
“Ni jambo la
kuhuzunisha hasa kwa familia zilizopoteza wapendwa wao katika tetemeko hili,
tunawaombea Mungu awape nguvu na kwa waliobaki tunaomba wavute subira kwani janga
hili ni la kila Mtanzania”. Amesema.
Amesema wao
wameathirika moja kwa moja pia kwa sababu benki hiyo ina tawi mjini Bukoba na
baadhi ya wafanyakazi waliguswa moja kwa moja na maafa hayo.
Akipokea msaada
huo, Mkuu wa mkoa wa Kagera, Meja Jenerali (mstaafu) Salum Kijuu ameishukuru
benki ya Mkombozi kwa moyo wa kizalendo na kusema msaada huo utachanganywa na
mingine ili ikasaidie wale walioathirika na tetemeko hilo.
“Mahitaji ni
mengi na tunashukuru kwa muitikio wenu kuja kuungana mkono na watanzania
wengine katika janga hili”. Amesema.
Wafanyakazi wa
benki hiyo pia walipata nafasi ya kutembelea baadhi ya maeneo yaliyoathiriwa na
tetemeko hilo na kuwapa pole baadhi ya waathirika.
Benki ya biashara ya Mkombozi ilianzishwa mwaka 2009
na kanisa Katoliki Tanzania na taasisi zake kwa madhumuni ya kusaidia
wafanyabiashara wadogo, wa kati na wakubwa kupata huduma za kifedha.
Ili kutanua wigo zaidi, waanzilishi wa benki hiyo
walitoa nafasi kwa watanzania wengine wakiwemo wafanyabiashara na wawekezaji
ili kuongeza nguvu.
Benki hiyo ina matawi sita yakiwemo matawi matatu Dar
es Salaam, moja Mwanza jingine Moshi na Bukoba pamoja na vituo vya huduma za
kibenki Morogoro na Tegeta Dar es Salaam.
Na mwandishi wetu
Comments
Post a Comment