PADRI LUKA, LULU YA MAENDELEO ILIYOZIMIKA
Ikiwa ni mwaka mmoja
tangu afariki dunia marehemu Padri Walter Lukewille, Ambapo kwa wananchi wa
mkoa wa Rukwa na Katavi walimzoea kwa jina la Fr.Luka kupitia sherehe za
jubilei ya miaka 25 ya parokia ya Familia Takatifu dominika ya29 ya mwaka c,
wamemshukuru mungu kupitia nafsi ya Padri Luka, Mmisionari aliyekuza imani na
kuleta maendeleo makubwa ya kiroho na kiuchumi katika jimbo la Sumbawanga na
jimbo la Mpanda.
"Marehemu
Padri Luka ni mmisionari ambae kwa kiasi kubwa amekuwa ni kumbukumbu kwa
waamini na wasio waamini wa jimbo la sumbawanga na Mpanda. Padri Lukani lulu ya mkoa wa Rukwa na Katavi kutokana na miradi mbalimbali ya maendeleo aliyoifanya
enzi za uhai wake". Amesema Joseph Msengezi mmoja wa waumini wa parokia ya
familia Takatifu iliyojengwa na Padri Luka iliyotimiza miaka 25 tangu kuanza
kwake.
Mbali ya kufanya
mambo mengi kama padri, mtawa na mmisionari mtiifu mnamo mwaka 1994 baada ya
kifo cha mhashamu Askofu Kaloro Msakila padri Luka aliteuliwa na Vatican kuwa
msimamizi wa kitume wa jimbo katoliki Sumbawanga, na alifanya kazi hiyo kwa
uaminifu mkubwa kwa muda wa miaka mitatu hadi pale baba Mtakatifu Yohane Paulo
wa II alipomteua Askofu Damian Kyaruzi kuwa askofu wa jimbo Katoliki Sumbawanga.
Marehemu PadrI Luka
alizaliwa tarehe 1 february 1930 katika kijiji cha Verl nchini Ujerumani. Baada
ya majiundo yote katika shirika la wamisionari wa Afrika katika malezi ya
kiseminari tarehe 26 Mei 1955 alipata daraja takatifu la upadri na mnamo mwaka
1959 alitumwa rasmi nchini Tanzania Sumbawanga kama mmisionari.
Enzi za uhai wake
marehemu padri Luka alifanya kazi katika
parokia ya chiwanda wakati ule 1959 hadi
1962 (chala) 1971 hadi 1984 (Mamba) 1984 hadi 2002. Na baada ya hapo
akisaidiana na waamini aliweza kuanzisha parokia ya Kristo mfalme, Roho
mtakatifu -malangali na parokia ya familia takatifu ambapo mnamo mwaka 2002
hadi 2004 alisaidia kulijenga kanisa la Mpanda (cathedral) akishirikiana na
marehemu askofu Pascal Kikoti na waamini wa jimbo katoliki Mpanda.
Mnamo mwaka
2004 kwa maamuzi ya wakubwa wa shirika
na kwa vifungo vya utii, padri Luka alirudi ujerumani katika nyumba ya
wamisionari wa Afrika (Afrikanum) iliyoko mjini Kolon. Hapo aliendelea kutoa
huduma ya kiroho kwa jumuiya na kwa waumini ambapo January 2014 alihamishiwa
katika nyumba ya wazee huko Trier ambako aliishi na wazee wengine waliofanya
kazi ya umisionari katika maeneo mbalimbali ya Afrika.
Mwezi Mei 2015
Padri Luka aliadhimisha jubilei ya miaka 60 ya upadri wake na siku chache
baadae alipata shida za kiafya na akagundulika kuwa na saratani ya ini. Ugonjwa
huu ulimletea udhaifu mkubwa wa kimwili, kwa kipindi cha miezi mitano tu tarehe
17 Oktoba 2015 saa 4: 45 asubuhi Mwenyezi Mungu alimwita kwake kuhani, mmisionari
kipenzi cha wanajimbo katoliki Sumbawanga na Mpanda.
Muuguzi aliemuuguza
anasema dakika za mwisho alitamka "Sasa ninakwenda" na kwa uso wa
tabasamu akatoa pumzi yake ya mwisho.
Tarehe 23 Oktoba
2015 Padri Luka alizikwa katika nyumba ya mwisho pamoja na wamisionari wengine
huko Trier Ujerumani. Ibada ya mazishi ilihudhuriwa na umati mkubwa wa
wamisionari wa Afrika wake kwa waume, ndugu jamaa na marafiki pamoja na
wawakilishi wachache kutoka jimbo katoliki Sumbawanga na Mpanda ambako alifanya
kazi takribani miaka 50.
"Mbali ya kazi
za kiroho na ujenzi wa makanisa kama hili ambalo alilijenga Padri Luka na mimi
nikiwa mmoja wa mafundi, Padri Luka pia alikuwa ni mtu wa hali ya juu lakini
hakuwa na matabaka kwa mtu yeyote wala dini wala kabila na alijali maendeleo ya
wananchi wote na kila alipofanya utume aliweza kujenga shule na kituo cha afya
kila mahali ili watu wanufaike. Padri Luka alikuwa ni mtu wa kwanza kuleta maji
ya bomba mkoani Rukwa, hatukuwahi kujua maji ya bomba yalivyo, ameanzisha shule
mbalimbali za chekechea na sekondari, kumbi na nyumba za kufikia wageni pia
tuliokuwa vijana wafanyakazi kwake tuliweza kunufaika sana" amesema Bwana
Didas Lunkonto.
Mbali ya mawazo
tofauti kutoka kwa watu wa dini tofauti kuhusiana na maendeleo yaliyofanywa na
Padri Luka jimbo Katoliki Sumbawanga linajivunia kuwa na kituo cha Radio
ijulikanayo kama Radio Chemchemi ambayo ilianzishwa na Padri Luka na kwa zaidi
ya miaka 20 imekuwa ikitoa huduma kwa jamii ya watu wa mkoa wa Rukwa na Katavi.
Kupitia serikali ya
Jamhuri ya Tanzania Kwa kutambua mchango mkubwa alioufanya Padri Luka enzi za
uhai wake, Raisi wa awamu ya pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndugu Ali
Hasani Mwinyi alimtunuku Padri Luka Tuzo ya Cheti cha mgeni mmisionari kuleta
maendeleo makubwa katika nchi ya Tanzania na kupitia kanisa katoliki jimbo
katoliki Sumbawanga kupitia maadhimisho ya jubilei ya miaka 125 iliyofanyika
mwaka 2011 kwa niaba ya waumini, watawa na mapadri, Askofu Damian Kyaruzi
alimtunuku Padri Luka tuzo ya utume na maendeleo alivyovifanya katika jimbo la
Sumbawanga na kanisa la Tanzania.
Raha ya milele umpe
ee Bwana , Na mwanga wa milele umwangazie apumzike kwa amani Amina.
Na Emmanuel Mayunga, Sumbawanga
Namkumbuka sana aliwahi kutupatia semina nzuri mwaka 1999 familia takatifu iliyo simamiwa na Padri Ediga mbegu. Mungu Amkumbuke kwa namna ambavo alijitoa katika Utume.
ReplyDeleteNakumbuka Mwaka 2004 aliongoza misa ya kutuaga waamini wa Jimbo la Mpanda alipokua anajiandaa kurudi Germany. M/Mungu amrehemu ampe pumziko la amani 🙏🙏🙏
ReplyDeleteTufanye maombi atangazwe kuwa mtakatifu
ReplyDelete