‘TUSIPOKUWA IMARA SAKRAMENTI YA KITUBIO ITAPOTEZA MAANA YAKE’
IMEELEZWA
kuwa changamoto nyingi zinazoikumba Sakramenti ya Kitubio katika ulimwengu wa
leo zinazweza kuwatikisa waamini kiimani iwapo hawatasimama imara.
Hayo yamebainishwa na Sista
Magdalena Laurent, katika Kongamano la Ekaristi Takatifu Jimbo Kuu Katoliki Dar
es salaam, lililofanyika Oktoba 8 katika viwanja vya Msimbazi Center, na
kuhudhuriwa na waamini kutoka parokia mbalimbali za jimbo hilo.
Akielezea juu ya
changamoto kadhaa zinazoikumba imani ya ukristo katika ulimwengu wa leo, Sista
Magdalena amesema kuwa kila Sakramenti ina
changamoto zake, lakini Sakramenti ya
kitubio ina changamoto nyingi kwani watu wengi katika ulimwengu wa leo wanashindwa
kuipokea.
“Katika uhalisia wa
maisha tunazungukwa na imani mbalimbali, tunasoma vitabu na vijarida, mitandao
pia inarusha mafundisho mbalimbali yenye uzushi pia juu ya Sakramenti ya
Kitubio. Tusipokuwa imara changamoto hizi zinaweza kututikisa katika imani hasa
katika kupokea kitubio. Pia kuna mbinu na mitego mbalimbali ya shetani
kutufanya tuone dhambi ni kitu cha kawaida katika ulimwengu wa leo” ameeleza
Sista Magdalena.
Aidha Sista Magdalena
ameonya kuwa kuna hatari ya watu kupuuzia dhambi na neno dhambi kuonekana
kupitwa na wakati, huku wakijaribu kuhalalisha kila kitu.
“Maadili yanamomonyoka
kwa kigezo cha kwenda na wakati. Amri za Mungu tunazirahisisha; Amri ya 1 inageuzwa na kuwa abudu miungu
wengine upate heri duniani, ndiyo maana tunashuhudia kuibuka kwa dini za ajabu,
dini za shetani, na nguvu za shetani katika ushirikina. Amri ya pili inageuzwa
kuwa taja jina la Mungu katika kuficha uovu na kusema uongo. Mungu anatumika katika
kuficha ukweli” ameongeza.
Akitaja hatari nyingine
za kiroho katika ulimwengu wa leo Sista Magdalena ametahadharisha juu ya watu
kukwepa kitubio kwa hofu ya kupoteza uhuru wa kufanya starehe, kutokuamini
huruma ya Mungu ya milele, kutoamini uwepo wa maisha ya baadaye, yaani ponda
mali kufa kwaja.
“Wengi wetu tuna aibu
ya kitubio, tunajihoji kuwa padri atanionaje na siyo Mungu atanionaje. Pia tuna
tabia ya kuziunganisha dhambi ‘najuta na zile nilizosahau’ na kwa kufanya hivyo
tunatenda dhambi nyingine katika kitubio yaani kusema uongo. Kama hatuna aibu
katika kutenda dhambi, kwa nini tunaona aibu kwenda kwenye kitubio” amesema.
Akijibu baadhi ya
maswali kutoka kwa waamini, hasa juu ya changamoto ya wakristo kutetereka
kiimani, Padri John Kulwa amewataka wazazi kuwarithisha watoto wao imani
Katoliki wakiwa bado wadogo ili kuwaimarisha na harati za kiroho.
“Anza na mtoto wako, tangu akiwa tumboni
mfundishe imani, kwa kuishi kiaminifu miguu miwili ndani ya kanisa katoliki.
Ukifanya hivyo, tamaa yako ya kupenda kanisa itatiririka kwa mtoto, na itampa
imani wakati wa majaribu. Mkiona watoto wenu wanalega katika imani jichunguzeni”
ameeleza.
Ekaristi
Takatifu na huruma ya Mungu ndani ya familia
Kwa upande wake Padri
Novatus Mbaula amesema kuwa familia ni jumuiya ya watu wanaounganishwa kwa
upendo wa kiagano, asili ya huruma kati ya mume na mke, na hivyo kuzitaka
familia kuwa chombo cha huruma ya Mungu
kwa wanadamu, kwa kuwa sakramenti zote za Kanisa huanzia nyumbani.
“Ekaristi Takatifu
inatupa changamoto ya kuhurumiana ndani ya familia, yaani kumkaribisha Kristo
katika mahusiano ya wana familia. Kama hakuna umoja na mawsiliano ya kifamilia
hakutakuwa na huruma. Vijana wengi wanaoitwa katika wito wa upadri,
hatuwahurumii badala yake tunawakimbiza katika mambo mengine, hii ni kwa sababu
hatutambui na kuthamini malengo yao na wito wao” amesema Padri Mbaula.
Aidha ameongeza kuwa
familia zinaweza kuwaonea wengine huruma ikiwa tu watayatambua mahitaji yao ya
msingi, ya kimwili na kiroho.
“Upendo na huruma
tunaouonyesha nje ya familia, ni changamoto inayotutaka tufanye hivyo hivyo
ndani ya familia, kadhalika ukarimu wa ndani ni changamoto ya kutoa ukarimu huo
nje” ameongeza.
Comments
Post a Comment