MWONGOZO KATIKA MAZIKO YA WAKRISTO NA UCHOMAJI MIILI YAO
Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, Alhamisi tarehe 25 Oktoba 2016 kwa idhini ya Baba Mtakatifu Francisko, limechapisha mwongozo unaojulikana kama “Ufufuko na Kristo mintarafu maziko ya wafu na utunzaji wa majivu ya wafu” Ad resurgendum cum Christo. Ili kuweza kufufuka na Kristo, lazima kufa pamoja na Kristo ili kujiondoa katika utumwa wa mwili ili kuweza kukaa na Bwana. Uchomaji wa miili na utunzaji wa majivu yake si dhana inayokinzana na Mafundisho ya Kanisa na ikiwa kama tukio hili si kwa ajili ya kupinga Mafundisho tanzu ya Kanisa au chuki dhidi ya Kanisa Katoliki.
Hadi sasa huu ndio msimamo na mafundisho ya Kanisa kuhusiana na maziko na utunzaji wa majivu ya miili iliyochomwa moto, Ibada ambayo kwa sasa imeenea katika mataifa mengi duniani. Kadiri siku zinavyozidi kuyoyoma, kumeibuka pia mafundisho ambayo yanakinzana na imani ya Kanisa. Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa baada ya kupata ushauri kutoka ndani na nje ya Vatican, linaona kwamba, kuna umuhimu wa kutoa Mwongozo ili kubainisha sababu msingi za mafundisho tanzu ya Kanisa na shughuli za kichungaji kwa kwa ajili ya kuwazika wafu pamoja na kutoa mwongozo mintarafu utunzaji wa majivu kwa waamini ambao miili yao imechomwa moto.
Ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu ni kilele cha ukweli wa imani ya Kikristo, inayofundishwa na kuhubiriwa kuwa ni sehemu muhimu sana ya Fumbo la Pasaka ambalo, mafundisho yake, Kanisa limerithi kutoka kwa Mitume wa Yesu, ili hatimaye, kuwawezesha waamini kutembea katika mwanga wa maisha mapya. Kristo mfufuka ni nguzo na chemchemi ya ufufuko wa waamini hapo baadaye, ili kupata maisha mapya kwa Kristo Yesu.
Kwa njia ya Ubatizo, waamini wanaifia dhambi na kufufuka na Kristo Yesu kwa njia ya nguvu ya Sakramenti ya Ubatizo. Ndiyo maana Kanisa katika sala ya utangulizi wa wafu linasali “Ee, Bwana uzima wa waamini wako hauondolewi ila unageuzwa tu. Nayo makao ya hapa duniani yakisha bomolewa, tunapata makao ya milele mbinguni”. Kwa njia ya kifo, roho inajitenga na mwili, lakini kwa njia ya ufufuko, Mwenyezi Mungu anaipatia miili ya binadamu maisha mapya. Ndiyo maana hata katika nyakati hizi, Kanisa linatangaza na kuungama imani katika Fumbo la Ufufuko. Kimsingi, ufufuko wa wafu ni imani ya Wakristo.
Kanisa katika Mapokeo yake, linawahamasisha waamini kuzikwa katika Makaburi au katika maeneo matakatifu kama kumbu kumbu endelevu ya kifo, maziko na ufufuko, mwanga ambao unajionesha kimsingi katika Fumbo la kifo cha Mkristo; imani na matumaini katika Fumbo la ufufuko. Kanisa kama Mama anawasindikiza watoto wake katika maisha ya hapa duniani kwa kuthibitisha imani katika ufufuko wa miili na kutolea sala zake katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, huku akiwa na matumaini ya ufufuko wa utukufu na maisha ya uzima wa milele. Maziko ya Mkristo ni kuthibitisha imani ya ufufuko wa miili pamoja na kuonesha utu wa mwili wa mwanadamu.
Tangu mwanzo, Kanisa halikuruhusu Ibada zinazomfuta mwanadamu mintarafu imani katika ufufuko wa miili na uzima wa milele. Maziko ya waamini katika makaburi na maeneo matakatifu ni kielelezo cha ibada na heshima kwa miili ya waamini waliotangulia mbele ya haki; waamini ambao miili yao ilikuwa ni Hekalu la Roho Mtakatifu, uliyowawezesha kufanya matendo mema wakati wa maisha yao hapa duniani. Ndiyo maana kuzika wafu ni sehemu ya matendo ya huruma kimwili na kwamba, waamini wanahimizwa kuwakumbuka marehemu wao pamoja na kuwaheshimu wafiadini na watakatifu, kielelezo cha umoja kati ya waamini walio hai na wale waliofariki dunia.
Pale ambapo kutokana na sababu mbali mbali maziko yanafanyika kwa njia ya kuchoma miili kama si kinyume cha utashi wa mwamini mwenyewe, Kanisa halina pingamizi kwa miili ya waamini kuchomwa moto, kwani hata katika tukio hili nguvu ya Mungu itaweza kuwafufua kwa wafu. Kanisa linaendelea kuhimiza waamini wazikwe na kwamba waamini hawazuiwi kuchoma maiti ya Wakristo, ikiwa kama si kinyume cha Imani ya Kikristo na wala tukio hili lisiwe ni kikwazo kwa imani ya watu!
Majivu ya miili ya waamini yanapaswa kutunzwa katika makaburi, Makanisa au katika maeneo matakatifu yanayosimamiwa na kuratibiwa na viongozi wa Kanisa, ili Jumuiya ya waamini iweze kuwaombea; makaburi yao yawe ni mahali pa sala, kumbu kumbu na tafakari juu ya Fumbo la kifo. Kanisa linaamini na kufundisha kuhusu Kanisa linalosafiri hapa duniani na Kanisa linalotakaswa pamoja na Kanisa la watakatifu wa mbinguni, ambao wote kwa pamoja wanaunda Kanisa moja la Kristo. Lengo la kutunza majivu ni kuendeleza ibada ya sala na heshima kwa wafu pamoja na kuepuka majivu haya kutumiwa kwa ibada na imani za kishirikina.
Baraza la Kipapa la Mafundisho tanzu ya Kanisa linasema, kimsingi, ni marufuku kuhifadhi majivu ya waamini marehemu majumbani. Ruhusa inaweza kutolewa na Askofu mahalia kwa makubaliano ya Baraza la Maaskofu mahalia au Sinodi ya Maaskofu wa Makanisa ya Mashariki. Majivu haya hayawezi kugawanywa miongoni mwa ndugu na jamaa ya marehemu.
Majivu haya pia hayapaswi kumwaga hewani, kutupwa baharini au kugeuzwa na kuwekwa kwenye vito vya thamani kama kumbu kumbu endelevu, kwani matukio kama haya yanaweza kupelekea uchomaji wa maiti kujikita zaidi katika masuala ya kiuchumi. Pale ambapo mwamini atakwenda kinyume cha Sheria, Kanuni na Mapokeo ya Kanisa mintarafu maziko ya Kikristo, basi atakosa haki ya maadhimisho ya Ibada ya wafu! Mwongozo huu umetiwa sahihi na Kardinali Gerhard Muller, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho tanzu ya Kanisa pamoja na Askofu mkuu Luis F. Ladaria, Katibu mkuu wa Baraza.
Kwa msaada wa Vatican Redio
Comments
Post a Comment