UTAKATIFU WA NYERERE, MCHAKATO UNAENDELEA
IKIWA WATANZANIA wanaadhimisha
kumbukumbu ya miaka 17 tangu kufariki kwa muasisi na Rais wa Kwanza wa
Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Kanisa Katoliki nchini linaendelea
na mchakato wa kumtangaza Mwenyeheri na baadaye Mtakatifu.
Wakizungumza na gazeti hili kuhusu mchakato huo, baadhi ya
Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini wameeleza kuwa, Kanisa halijanyamaza,
halijalegea wala kupuuzia zoezi hilo, bado linaendelea na mchakato huo ambao
wameeleza kuwa unahitaji muda kuukamilisha.
Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki Musoma ameeleza
kuwa awali Jimbo la Musoma ambalo ndilo jimbo Mama la Mwalimu Nyerere lilianza
kufanya maandalizi ya awali ya mchakato huo lakini Kanisa liliona ni vyema
kuhamishia mamlaka ya mchakato huo katika Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam
likishirikiana na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) kwakuwa zaidi ya
nusu ya maisha ya mwalimu Nyerere yalikuwa Dar es Salaam ambako aliishi na
kufanya kazi.
“Mamlaka ya mchakato wa kumtangaza mwalimu Nyerere Mtakatifu
yalihamishiwa Dar es Salaam huku Msemaji Mkuu akiwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu
Dar es Salaam Mwadhama Polycarp Cardinali Pengo ambaye ana mamlaka kamili ya kuratibu
na kuteua mahakama (tribunal) za kushughulikia mchakato huo akishirikiana na
TEC.
Kwetu sisi tunasubiri barua rasmi ya kusema kuwa Mahakama (tribunal)
ya Mchakato wa Kumtangaza Nyerere Mtakatufu katika Jimbo la Musoma imepewa mamlaka
ya kuwa sehemu ya mchakato huo ili
tuendelee na hatua nyingine. Tukishapata kibali hicho rasmi tutashirikiana na
mahakama nyingine ambazo zimeundwa (zimepewa kibali rasmi) ili tuendelee na
hatua nyingine.
Waamini waendelee kusali kwani Kanisa linaendelea na mchakato
huo tukiamini kuwa utakamilika kwa wakati,” ameeleza Askofu Msonganzila.
Askofu
Nzigirwa aeleza
Kwa upande wake Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es
Salaam Mhashamu Euzebius Nzigilwa ameeleza kuwa, Kanisa linaendelea na mchakato
huo hususani kwa upande wa Dar es Salaam ambapo Msemaji Mkuu wa Mchakato huo ni
Mwadhama Polycarp Cardinali Pengo ambaye kwa sasa anaendelea na matibabu ya
afya yake.
“Ninachokifahamu ni kwamba ni kweli mchakato ulianzia jimboni
Musoma na baadaye ukahamishiwa Dar es Salaam. Mwadhama anaendelea kuratibu
shughuli zote ikiwemo kuunda mahakama (tribunal) za mchakato huo ili pamoja na
ile ya Musoma zipewe mamlaka kamili ya kuendelea na hatua nyingine ikiwemo
utafiti kwa watu mbalimbali ndani na nje ya nchi ambao wanamfahamu vizuri
mwalimu Nyerere aidha kwa kuishi ama kufanya pamoja naye,” amesema Askofu
Nzigilwa.
Katibu Mkuu wa Baraza wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania
(TEC) Padri Raymond Saba ameeleza kuwa, ni kweli Mamlaka ya kusimamia na
kuratibu mchakato huo (Competence Forum) ilihamishiwa Dar es Salaam na Baraza
la Maaskofu lilikubali kushirikiana na Jimbo Kuu Dar es Salaam ili kufanikisha
zoezi hilo.
Rais
Mgufuli anamuenzi Nyerere kwa vitendo
Pamoja na juhudi hizo za Kanisa za kumtangaza Nyerere Mtakatifu,
Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki Bukoba Mhashamu Methodius Kilaini ameeleza
kuwa, Mwalimu Nyerere anakumbukwa na watanzania kwa tunu alizoziacha
ziliendeshe taifa hili hususani, umoja wa kitaifa, uadilifu, mapambano dhidi ya
rushwa, ubinafsi na ufisadi.
“Jambo mojawapo alilisema Julai 29 Julai, 1985, kwamba: “Kazi
iliyokuwa muhimu kuliko zote kwangu mimi, ilikuwa ni kujenga Taifa lenye umoja
kwa msingi wa heshima na usawa wa binadamu.”
Lakini yapo mambo mengine ya uongozi wake ambayo tunapaswa
kuyakumbuka na kuyaenzi , hususan suala la uadilifu katika uongozi (au maadili
ya uongozi), Azimio la Arusha, miiko ya uongozi, mapambano yake dhidi ya
rushwa, ufisadi na mengineyo.
Hayo ndyo pia yanalisaidia taifa hili kukua na kusonga mbele
licha ya changamoto mbalimbali tulizo nazo,” amesema Askofu Kilaini.
Ameeleza
kuwa, rais wa sasa John Magufuli anafanya juhudi za kurudisha heshima katika
uongozi. Hilo ni jambo muhimu katika nchi iliyo na maadili na yenye uchu wa
maendeleo. Ndiyo maana akikuta kiongozi anayefanya kazi kinyume na taratibu
anamfukuza kwasababu anajua miiko ya uongozi.
“Kuna
wakati nchi hii kiongozi akiiba ama akifanya kazi kinyume na taratibu
anahamishiwa katika wizara nyingine. Kumbe anaenda kuiba sehemu nyingine.
Nyerere hakufanya hivyo kamwe na ndio maana Rais Magufuli atachukiwa na wengi
kwasababu ya kusimamia miiko ya uongozi. Hata Nyerere alichukiwa lakini
alikumbukwa baadaye.
Rais wa
sasa aendelee kufanya kazi kwa kusimamia misingi ya taifa hususani kujali
wanyonge. Nchi isitawaliwe na matajiri wanaokwepa kodi halafu mnyonge
anyanyasike. Asimamie uadilifu na kujenga taifa moja lenye amani na maendeleo
kama alivyokuwa Baba wa Taifa,” amesisitiza.
Nitapeleka
ushahidi Roma kuhusu maisha ya Nyerere - Museveni
Wapo wengi wanaoguswa na maisha ya
Mwalimu Nyerere katika Nyanja mbalimbali. Ndiyo maana baadhi wanaguna kuchelea
kutangazwa Mtakatifu hadi leo.
Ibada ya Misa
Takatifu ya kumuombea Baba wa Taifa ilifanyika katika Kanisa la Mashahidi wa Uganda,
Namugongo Uganda Juni 1 mwaka 2014 ambapo ibada hiyo iliendeshwa na Askofu Mkuu
wa Jimbo la Kampala, Dk. Cyprian Kizito Lwanga.
Hiyo ilikuwa ni
mara ya nane ibada ya kuombea mchakato wa kumfanya baba wa Taifa kuwa
Mwenyeheri na hatimye mtakatifu unafanyika katika kanisa hilo nchini Uganda
ambapo mchakato huo ulianza mwaka 2006.
Katika ibada
hiyo ambayo ilihudhuria na maelfu ya Watanzania, pamoja na mataifa mbalimbali
duniani, pia ilihudhuriwa na familia ya Marehemu Baba wa Taifa, Waziri Mkuu wa
Uganda Amama Mbabazi (Wakati huo) mawaziri na wabunge kutoka Uganda, ambapo
Tanzania iliwakilishwa na Balozi wa Tanzania nchini Uganda.
Mwandishi Paul
Mallimbo, aliandika hotuba ya Rais Museven aliyehudhuria Ibada hiyo ya Misa
Takatifu huku akijawa na maneno mazito yaliyosababisha baadhi ya waamini
kububujikwa na machozi kwa jinsi alivyomzungumzia Mwalimu Nyerere.
Rais Yoweri
Museveni, alisema kiongozi bora ni yule anayefuata maagizo ya Mungu na
kuwatumikia binadamu wote kwa usawa na haki.
Alisema hata kwenye
maandiko matakatifu ya Biblia kuna mistari inayomtaka binadamu ampende binadamu
mwenzake kama anavyojipenda yeye;
“Kwenye biblia kuna
sehemu inauliza kuwa utampendaje Mungu ambaye hujawahi kumuona, na ushindwe
kumpenda binadamu mwenzako,” Alisema kwa sababu aliwahi kufanya kazi na Mwalimu
Nyerere, anaweza kutoa ushahidi kwamba mwalimu alifanya yote mawili, kumtii
Mungu na kuwatumikia binadamu.
Mojaya sababu iliyomfanya Marehemu Papa Paulo
II kutangazwa mtakatifu ni pamoja na kuisaidia Ulaya Mashariki, ambayo wananchi
wake walikuwa hawamwamini Mungu. “Marehemu Papa Paulo II alisaidia kuikomboa
Ulaya Mashariki kutoka kwenye ukomunisti, wananchi walikuwa hawaamini kuna Mungu,
lakini kwa juhudi zake aliwafanya wamwamini na kumpenda Mungu,”alisema.
Rais Museveni alisema anatarajia kupeleka
ushahidi kwa Papa Benedict (Kwa wakati huo sasa ni Papa Fransisko) kwamba
Mwalimu anasifa za kutangazwa kuwa mtakatifu kwa sababu alimtii Mungu na
kuwatumikia binadamu. “Mimi nitapeleka ushahidi kwa Papa, kwamba mbali na
mwalimu kumtii Mungu na kuwpenda binadamu wote, pia aliwakomboa Waafrika kutoka
Ruvuma mpaka Capetown, huu ni ukweli siyo hadithi,alisisitiza Rais
Museveni.
Kufuatia hatua hiyo
ya kwenda Roma kutoa ushahidi, Rais Museveni alisema katika maadhimisho ya
kuombea mchakato wa Mwalimu kuwa Mtakatifu yatakayofanyika mwakani (wakati huo),
ameahidi kuwaita maraisi wote waliowahi kufanya kazi na Mwalimu Nyerere ili
kuuthibitishia ulimwengu kuwa Marehemu Baba wa Taifa ameweza kuwaunganisha waafrika.
Alifafanua kuwa Mwalimu ametoa mchango mkubwa
wa ukombozi kwa nchi za Msumbiji, Zambia, Zimbabwe, Namibia, Angola, Afrika
Kusini, Uganda na Tanzania yenyewe. Hivyo kuja kwa viongozi hao kushiriki ibada
hiyo itakuwa baraka kubwa.
“Jitihada za
mwalimu kuikomboa Uganda, ndipo nasi tulipoweza kuzisaidia nchi za Rwanda,
Sudan Kusini na Congo kujikomboa na kuongeza kuwa kama si juhudi za mwalimu tusingekuwa
na uwezo wa kuwasaidia wengine.
Upande wa viongozi
weusi, hakuna kiongozi ambaye ametoa mchango mkubwa kama Marehemu Mwalimu
Nyerere.
Hapa Duniani sidhani kama kuna mtu mweusi
mwingine ambaye ametoa mchango kama mwalimu, na hili nimelishudia mwenyewe
sikuambiwa na mtu. Hata mzee wetu Nelson Mandela alifanya kazi kubwa Afrika ya
Kusini lakini Mwalimu alifanya kazi kubwa zaidi ya ukombozi wa Afrika,
Alisema.
Mwalimu aliikomboa
Tanzania na kuwafundisha dini ya Kristo, kwa vitendo siyo kwa maneno. Nchi
nyingine za Afrika zimepatwa na machafuko ya ukabila na dini kutokana na msingi
mbaya wa viongozi waliotangulia.
Tanzania ni nchi ya
Wakristo, Waislamu na wale wengine wanaoamini dini za kienyeji lakini mwalimu
aliwafundisha Watanzania fikra za kizalendo za umoja.
Uganda haikupata
elimu nzuri juu ya jambo hilo, viongozi wa kwanza wa taifa letu waliwapandikiza
wananchi chuki, kwamba dini ni kumchukia mwenzako, waumini wa dini moja
kuwachukia waumini ya dini dini nyingine na matokeo yake ni umwagaji wa damu.
Biblia inasema kile
unachopanda ndicho unachovuna, kwa hiyo sisi hapa tulipanda mbegu mbaya na
tukavuna umwagaji wa damu.
Tanzania haijawahi
kuona umwagaji mkubwa wa damu zaidi ya ajali za magari na ile ya kipindi kile
wakati askari wa Tanzania walipokwenda Uganda kupigana na Idd Amin. Nadhani hii
ndiyo damu pekee mmeona.
Mpaka 1986 wakati naingia
madarakani raia 800,000 wa Uganda walikuwa wamekufa kutokana na chuki za udini
na ukabila. “Uganda imeshuhudia umwagaji mkubwa sana wa damu, Congo
wameona damu, Sudan, Somalia, Kenya, Rwanda na Burundi ni Tanzania pekee ambayo
imekuwa kama kisiwa cha amani, hii yote ni kutokana na mchango wa mwalimu
Nyerere ambaye alidumisha amani, umoja na maendeleo kwa watu wake.
Sababu mojawapo ya
kumfanya mtu awe mtakatifu ni watu kutoa ushahidi wa matukio mbali mbali
yaliyofanywa na mtu huyo wakati wa uhai wake.
Nitakwenda Roma
kutoa ushahidi kuhusu matendo ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere.
Nikienda kwa Baba Mtakatifu nitatoa ushahidi
mzuri juu ya marehemu Mwalimu Nyerere tena nitatoa kwa maandishi siyo kwa
maneno pekee yake.
Na Sarah Pelaji,
Dar es Salaam
Comments
Post a Comment