Watanzania wengine watunukiwa nchini Kenya
CHUO Kikuu
cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki na Kati, (AMECEA-CUEA), kimewatunuku
Mapadri Watanzania wawili ambao ni wahadhiri wanaofundisha katika chuo hicho
baada ya kutambua mchango wao wa kitaaluma kwa jamii.
Imekuwa ni furaha, hamasa na changamoto kwa
Wahadhiri na wanafunzi hasa Watanzania wanaosoma chuoni hapo baada ya wahadhiri
hao wawili kutunukiwa hadhi ya juu ya kitaaluma “Profesa” wakiwa wamekidhi
vigezo na masharti vinavyomwezesha mhusika kufikia hatua hiyo.
Aliyekuwa Makamu Mkuu wa Chuo katika Utawala, (
DVC) Padri Profesa Juvenalis Baitu, amewatangaza rasmi katika tafrija
iliyoandaliwa na Umoja wa wanafunzi Watanzania wanaosoma CUEA - UTASCU ( Union
of Tanzania Students CUEA), na kuwatambulisha maprofesa wapya waliotunukiwa
hadhi hiyo kuwa ni Padri Profesa Nicholaus Segeja kutoka Jimbo Kuu Katoliki
Mwanza na Padri Profesa Richard Rwiza, Padri wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha.
Kama ilivyo desturi ya Umoja wa wanafunzi Watanzania
wanaosoma CUEA – UTASCU kukutana kila muhula mpya wa masomo kuwakaribisha
wanafunzi wapya waliojiunga chuoni hapo, kwa namna ya pekee mhula huu,
wamekutana kwa lengo la kuwapongeza na kuenzi kazi njema na hatua waliofikia
Wahadhiri wao wanaotoka Tanzania, pamoja na kuwaaga viongozi waliomaliza muda
wao madarakani na kuwakaribisha viongozi wapya.
Akizungumza katika hafla hiyo Aliyekuwa Makamu
Mkuu wa Chuo katika Utawala, ( DVC) Padri Profesa Juvenalis Baitu Mtanzania
anayetoka Jimbo Katoliki Bukoba, amesema ni vema wanafunzi wakajikita katika
kutumia muda vizuri wawapo masomoni na wakishamaliza warudi mara nchini Tanzania
kutumia taaluma waliyoipata.
Aidha amewataka wanafunzi wawapo chuoni kutambua
kuwa wamebeba dhamana ya watu wengi wakiwemo wazazi, wafadhili wao, jumuiya na
mikoa watokayo nchini Tanzania na dhamana ya maisha yao wenyewe, hivyo wanapaswa
kuwa mabalozi wema kila wakati katika kuiwakilisha vyema Tanzania nchini Kenya
kwa uwepo wao.
“Utanzania na Uzalendo utuunganishe bila
kujali protokali tulizonazo” Amesema Profesa Baitu.
Akizungumza kwa niaba ya mwenzake kwenye hafla
hiyo, Padri Nicholaus Segeja amemshukuru
Mungu aliyewawezesha kufikia hatua hiyo na pia Umoja wa Watanzania kwa kuandaa
tafrija hiyo ili kutambua hatua waliyofikia, na kwa kujumuika pamoja kama
familia ya Watanzania, hivyo amepongeza uongozi ulitoka madarakani kwa kazi
nzuri na kuwakabidhi uongozi mpya kwa furaha.
“Tangu mlipochaguliwa mmeulinda umoja huu
haukufia mikononi mwenu, kadhalika nanyi mnaopokea jitahidini umoja huu usifie
mikononi mwenu” amesema Profesa Segeja.
Ili kufikia mafanikio, Profesa Segeja
amesisitiza kufanya kazi kwa umoja, mshikamano na kushirikishana siri ya
mafanikio bila kujali tofauti za rika na nyadhifa, huo ndiyo ukarimu
unaotutambulisha Watanzania.
Katika mahojiano na KIONGOZI, Profesa Segeja
amesema amekuwa Profesa katika masuala yahusuyo Teolojia ya Kichungaji.
Naye Mwenyekiti mpya wa UTASCU, Padri Onesmo
Shingelwa kutoka Jimbo Kuu Katoliki Mwanza, amemshukuru Mungu na wanaumoja huo
kwa kumwamini na kumchagua kuwa Mwenyekiti.
“Umoja wa
Watanzania utajengwa na Watanzania wenyewe, hivyo kila mmoja ajisikie huru
kujiunga” amesema Padri Shingelwa. Padre Onesmo Shingelwa, ameahidi kuimarisha
umoja zaidi na amesema furaha yake itakamilika kuona umoja huo unasonga mbele.
Comments
Post a Comment